Habari

Jumamosi, 26 Oktoba 2013

JK: CCM inaweza kung’oka 2015

Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete amesema kama rushwa haitakomeshwa ndani ya chama hicho, katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015 kitaanguka vibaya na iwapo kitanusurika hakitapita kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amempa jukumu la kushughulikia viongozi wa CCM wanaokula rushwa, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philipo Mangula.


Rais Kikwete, alitoa onyo hilo juzi usiku, alipokuwa akifunga mafunzo maalumu ya siku nne kwa makatibu wa mikoa, makatibu na wenyeviti wa wilaya wa chama hicho nchini.
“Kama hatutabadilika katika suala la rushwa mwaka 2015 tutakuwa na wakati mgumu sana na kama mwaka huo tutafanikiwa kuishika Serikali, basi mwaka 2020 hatutarudi tena madarakani.
“Najua rushwa ipo na mnaendelea kupokea shilingi laki mbili za airtime (muda wa mawasiliano), ndugu zangu hatutafika ama wengine watavuka na wengine kukwama,” alisema Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete.
Hii ni kauli ya kwanza nzito ya Rais Kikwete ya hivi karibuni ya kukionya chama hicho kuhusu uimara wake wa kuendelea kushika dola.
Aliendelea kusema kuwa tatizo la rushwa kwa viongozi wa chama hicho linazidi kuwa kubwa kila siku, hali ambayo inawapotezea imani wananchi ambao ndio wapiga kura wao.
“Viongozi wa chama ndio mmekuwa mawakala wa kusambaza rushwa bila hata aibu. Nawaombeni tubadilike, kama tutaendelea hivi hali yetu itakuwa ngumu sana katika chaguzi mbalimbali, nawaambieni,” alisema Rais Kikwete ambaye alitumia muda wa saa mbili kufunga mafunzo hayo.
Aliwaambia kuwa siku hizi watu wana mbadala wa vyama vingine na siyo CCM peke yao.
Aidha, Rais Kikwete alisema viongozi ambao wanajihusisha na vitendo vya rushwa waondolewe mara moja katika nafasi zao, ili kuwaweka watu watakaokisaidia chama kupata mafanikio.
“Tuna vijana wengi kutoka katika vyuo mbalimbali ambao wanaweza kufanya kazi kwa uadilifu wa hali ya juu, hivyo hatuna budi kuachana na hawa wala rushwa ambao watatupotezea sifa yetu kwa wananchi.
“Tukipoteza urais ndiyo tumekwisha na chama kinaweza kufa.”
CHANZO- MWANANCHI.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni