Posted by: Sweetbert Abednego in Matukio ya siku 46 mins ago 0 2 Views
28 Oktoba mwaka 2013 Miladia. Siku kama ya leo miaka 521 iliyopita, Christopher Columbus aligundua pwani ya mashariki mwa Cuba na hivyo kufungua mlango wa kuingia wanajeshi wa Uhispania katika kisiwa hicho sambamba na kuanza kuwakoloni wakazi wa eneo hilo na kupora utajiri wao. Katika kuimarisha satwa yake, Uhispania ilianza kuwauwa kwa umati Wahindi Wekundu ambao ndio wakazi asili wa ardhi hiyo.
Hata hivyo uasi mkubwa uliofanywa na wananchi wa Cuba dhidi ya wakoloni wa Uhispania, uliibua harakati ya ukombozi wa wananchi wapigania uhuru dhidi ya nchi hiyo. ***
Miaka 73 iliyopita katika siku kama ya leo, kikosi cha askari laki mbili wa Italia kiliishambulia Ugiriki kwa amri ya Benito Mussolini Rais wa wakati huo wa serikali ya Kifashisti ya nchi hiyo. Mashambulio hayo ya Italia dhidi ya Ugiriki yalifanywa wakati wa kupamba moto Vita Vikuu vya Pili vya Dunia huko barani Ulaya. Hata hivyo, wananchi wa Ugiriki walisimama kidete na kukabiliana na shambulio hilo la Italia na hatimaye wakaibuka na ushindi. ***
Katika siku kama ya leo miaka 1374 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Maytham Ibn Yahya al-Tammar mmoja wa masahaba na wafuasi wa Mtume (saw) aliuawa shahidi. Awali Maytham al-Tammar alikuwa mtumwa, lakini Imam Ali bin Abi Talib (as) akamnunua na kumuachilia huru. Imam Ali alikuwa akimpenda na kumthamini mno Maytham al-Tammar kama ambayo Maytham pia alikuwa na mapenzi makubwa na Imam Ali. Hatimaye katika siku kama ya leo, sahaba huyo wa Mtume (saw) aliuawa kinyama na watawala wa Bani Umayya kwa kosa la kuwapenda na kuwaunga mkono Ahlul Bayt (as) na hivyo kufa shahidi katika siku kama ya leo. ***
Na miaka 193 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria, kulianza duru ya pili ya vita kati ya Iran na Russia. Chanzo cha kuzuka vita hivyo ni hatua ya majeshi ya Russia ya kuvamia maeneo ya mpakani ya Iran. Licha ya jeshi la Iran kujitolea mno katika vita hivyo, lakini Iran ilishindwa kutokana na udhaifu wa serikali kuu na vile vile kutowasili kwa wakati kwa vikosi saidizi. Vita hivyo vilimalizika kwa kutiwa saini mkataba wa Turkmanchai. Kwa mujibu wa mkataba huo, sehemu kubwa ya Azerbaijan ya Iran ikadhibitiwa na Russia na kwa msingi huo Iran ikawa imepata hasara kubwa isiyofidika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni