Habari

Jumatatu, 21 Oktoba 2013

Tume ya Warioba yaomba muda zaidi


Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeomba kuongezewa muda wa mwezi mmoja kutokana na ugumu wa kazi ya uchambuzi wa maoni yaliyotolewa na wananchi na asasi mbalimbali.
Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba ilitakiwa kufanya kazi kwa miezi 18 kwa mujibu wa Sura ya 83 ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Maana yake ni kuwa Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 1, mwaka jana  ilitakiwa kukamilisha kazi yake Novemba 1, mwaka huu.
Ikiwa maombi hayo ya Tume yatakubaliwa ina maana watatakiwa kukabidhi ripoti yake Desemba 1, mwaka huu.
Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Augustine Ramadhan aliliambia gazeti hili kwa simu jana kuwa wamepeleka serikalini maombi ya kuongezewa muda wa kufanya kazi.
Hata hivyo, Jaji Ramadhan alisema kuwa wameomba muda zaidi kutokana na kukabiliwa na kazi kubwa ya kuchambua maoni hayo.
Alisema hakuwa na taarifa ya majibu ya kama ombi lao limekubaliwa au la.
“Hatukuomba miezi miwili kama sheria inavyotuelekeza, tumeomba mwezi mmoja na mpaka Ijumaa nilipotoka ofisini sikuwa na taarifa kama kibali kilikuwa kimetolewa, labda kesho (leo) nikienda ofisini nitafuatilia kufahamu kama kimetoka,” alisema Jaji Ramadhan.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alikiri kuwa tume hiyo imeomba kuongezewa muda.
“Ni kweli barua ya Tume imeletwa, tumeipokea na inafanyiwa kazi,” alisema Rweyemamu kwa kifupi.
Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe akizungumza kwa njia ya simu; baada ya kuulizwa ikiwa Serikali imetoa kibali hicho au la alisema, “Sizungumzi na waandishi leo.” Simu ikakatika.
CHANZO- MWANANCHI.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni