Habari

Jumamosi, 9 Novemba 2013

SHUTUMA ZA WAZIRI LUKUVI KWA CUF NI ZA KIPUUZI NA HAZINA MSHIKO;

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI;

09 Novemba 2013.

SHUTUMA ZA WAZIRI LUKUVI KWA CUF NI ZA KIPUUZI NA HAZINA MSHIKO;

Nikiwa hapa Johannesburg nikihudhuria mafunzo maalum ya usimamizi wa uchaguzi, nimejulishwa kwamba huko nyumbani Tanzania(bungeni), waziri wa sera, bunge na uratibu mhe. Lukuvi ameishutumu CUF kuwa ndiyo ilipendekeza tume ya warioba ivunjwe mara baada ya kukabidhi andiko la katiba kwa bunge la katiba. Kulingana na umuhimu wangu katika mchakato huu nikikiwakilisha chama changu mara kadhaa, nimeona nijitokeze kueleza ukweli uliopo katika jambo husika, hivyo Naomba kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo;

1. Awali, maoni ya namna hiyo yalitolewa na chama chetu mbele ya rais mwaka 2011 ambapo viongozi wa chama chetu wakiongozwa na makamu mwenyekiti taifa na mie mwenyewe nikiwepo, walikutana na rais Ikulu jijini DSM mwishoni mwa mwaka 2011. 

Mantiki ya maoni ya chama chetu wakati huo ilikuwa kwamba, nini itakuwa kazi ya tume ikishawasilisha andiko lake kwa bunge la katiba ? Serikali haikuwa na majibu, maoni yetu yakawa kwamba tume imalize muda wake kuliko kuendelea kulipwa mabilioni ikiwa serikali inajua hakutakuwa na kazi.

Maoni haya yalikuwa na lengo hasa la kuhakikisha tunapata katiba mpya lakini pia matumizi ya fedha yasiyo ya msingi tunaachana nayo.

2. Tokea tulitoa maoni ya namna hiyo, hatukuwahi kukosolewa na chama chochote, taasisi yoyote au vyombo vya habari. Ikumbukwe maoni tuliyoa ikulu hayakuwa siri, tuliyasema wazi ba tuligawa nakala kwa vyombo vya habari. 

Baadaye mwaka 2012 mwezi wa Septemba, serikali ilipokuwa inahitaji maoni juu ya sheria ya mabadiliko ya katiba, wanasheria wa chama chetu walihakiki maoni tuliyoyatoa ikulu mwaka 2011 na bado wakaona maoni ya ukomo wa tume ya katiba yalikuwa na mashiko. Waraka huu wa maoni uliopelekwa mara ya pili ulipokamilishwa na hatua zote za chama niliusaini mimi mwezi Septemba 2013.

Na mwezi wa tatu mwaka 2013 serikali ilipoomba maoni(mimi sikuwepo ofisini wakati huo), mwanasheria wa chama chetu Twaha taslima aliwasiliana na mwanasheria wetu wa Zanzibar na wakapitia maoni ya Desemba 2011 na yale ya Septemba 2012 na kufanya mabadiliko kadhaa, suala ukomo wa tume likabakia kuwa maoni yetu na mhe. Taslima alisaini waraka kwenda serikalini kuhusu jambo hili.

Wakati tumetoa maoni haya mara zote hatukuwahi kupingwa na mtu hata yalipoandikwa na vyombo vya habari.

3. Mjadala wa tume ikome au iendelee, tutakubaliana ulianza kwa nguvu katikati ya mwaka huu 2013 kabla ya bunge lililoenda kupitisha muswada mbovu. Katikati ya mwaka huu ndipo chama chetu kilijiridhisha kuw mchakato wa katiba unatekwa na vigogowa CCM na kwamba tume ikivunjwa patakuwa na madhara makubwa sana.

Mwisho wa Mwezi mei 2013, chama chetu kilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kikiwashutumu watu wanaoiponda tume ya katiba na kutaka iachwe ifanye kazi zake kwa uhuru, ni wakati huo pia ndipo chama kilieleza waziwazi kuwa tume ina umuhimu wa kubaki ili kusimamia na kuwa sehemu ya mchakato uliobakia ili kuondoa kabisa uwezekano wa vigogo wachache kuuhodhi mchakato huu.

4. Baadaye katika bunge la lilipotisha marekebisho miezi michache iliyopita, vyama vya CUF,CHADEMA na NCCR vilishirikiana na kupinga masuala kadhaa likiwemo hili la tume kuvunjwa.kama chama chetu kibgetaka ivunjwe hata sasa kingesema, lakini hivi sasa tumeona umuhimu wa tume kuwepo na tumesema hivyo na kupigania hivyo, siyo dhambi hata kidogo.

Nani anataka chama chetu kiwe na mawazo yaleyale kila wakati na kujifunga na ukake katika jambo ambalo tumlipima na kuona madhara yake? 

Msimamo wetu wa kutaka tume ibakie umekuwepo tokea mwezi Mei mwaka huu na ni kabla ya ushirikiano wa bungeni na tulipokaa na wabunge wetu kabla ya bunge lile waliekezwa kwenda kupigania tume iendelee kuwepo, na ndiyo maana ilikuwa rahisi kushirikiana na CHADEMA na NCCR kwa sababu tayari pana masuala mengi tulijikuta tuna mtizamo unaofanana.

5. Maneno haya aliyosema Lukuvi jana bungeni alianza kuyasema siku wakuu wa vyama sita vyenye wabunge walipokuwa Ikulu kuonana na rais. Wakati rais anafafanua hoja ya uwepo au ukomo wa tume ya katiba ambapo alianza kueleza umuhimu wa tume kuendelea kuwepo, Lukuvi aliingilia kutaka kumtoa rais kwenye hoja yake, Lukuvi akajenga hoja kuwa CUF ndo walipendekeza tume ivunjwe. Rais alimkataza Lukuvi na akamwambia kuwa hayo yalikuwa maoni ya chama na yalishapita, kwa sasa tuangalie hoja zilizoko mezani na hasa hoja ya vyama vyote kuwa tume iendelee kuwepo.

Lukuvi aliendelea kujenga hoja kuwa hata kipengele "hatari" cha kupitisha vipengele vya katiba kwa kutumia wingi mdogo(simple majority) ulipendekezwa na CHADEMA kupitia kwa Halima Mdee ambaye alipigania utaratibu huo na kamati ya bunge ikaukubali na kuupitisha.

Lukuvi alipokaa kitako na nyaraka zake mie nikapewa nafasi na nikaeleza kikao msingi wa maoni yale na nikasisitiza kuwa "yalishapitwa na wakati" na nikaeleza kwa nini hivi sasa tunataka tume iendelee kuwepo na nikatoa sababu tunazosimamia.

Mimi na Mnyika tuliongoza mazungumzo ya kamati ya vyama na ile ya serikali ambapo upande wa serikali waliongozwa na Lukuvi na kuna masuala ambayo tulikubaliana na kuna yale ambayo hatukukubaliana. Kwa mfano hili la ukomo wa tume sisi tumepigania tume iendelee lakini kamati ya serikali ikakataa kata kata, sasa kama wanasema wanataka ivunjwe kwa sababu CUF ilishauri, je mbona CUF inaposema isivunjwe wao wanakomalia kuivunja? Huu ni uchuro.

5. Watu wanataka kuleta hoja hii iliyopitwa na wakati leo hii. Ikiwa tunahukumiana kwa maazo tuliyowahi kutoa, mbona serikali kila kukicha inakuja na mawazo mapya kupinga mawazo ya zamani? Mbona kila mara wanakuja na sheria mpya kuondoa na kupinga za zamani? 

Na kama tunahukumiana, mbona CHADEMA wameoigania mfumo wa serikali za MAJIMBO tangu wamekuwa chama cha siasa, lakini hivi sasa wameona mfumo huo sio muhimu na wanasimamia mfumo wa serikali tatu. Je ni nani anayetaka vyama vya siasa na viongozi wake, wajifunge kwenye ukale na wasifikiri kwa mujibu wa wakati uliopo?

6. Hoja hii ya Lukuvi inaweza kuwa na lengo la kuupotosha umma na kuwagawa watanzania na hasa kugawa "spirit" ya vyama vya upinzani na wananchi kwa ujumla, kuwa CUF ilikuwa na lengo la kuhujumu mchakato wa katiba, jambo ambalo ni upuuzi usiopaswa kufikiriwa.

CUF imekuwa ni chama pekee kilichopigania mabadiliko ya katiba ya nchi hii kwa kuungana na vyama, taasisi na wafau wote bila kusita, tangu chama kilipoanzishwa, na tutasimama imara kuendeleza mapambano hayo bila kuangalia nyuma.

Suala la hoja fulani kuwahi kupendekezwa namna fulani na chama fulani wakati fulani na kwamba hivi sasa chama husika kinashikilia hoja nyingine ni jambo endelevu na si jipya(mawazo ya vyama vyote duniani) hubadilika kulingana na mahitaji ya wakati husika.

Kwa sasa mawazo na maoni ya CUF juu ya uwepo wa tume ya katiba yako wazi sana. TUNATA TUME IENDELEE KUWEPO na tumependekeza juzi katika majadiliano na serikali kuwa WAJUMBE WA TUME WOTE AU BAADHI YAO KWA KADRI ITAKAVYOONEKANA INAFAA wawe sehemu ya wajumbe wa bunge la katiba.

Ikiwa LUKUVI ati anatuhukumu kwa maoni ya kale atakuwa ni waziri na kiongozi wa serikali mwenye maono, busara na uwezo wa kufikiri mdogo sana. Asitumie mwanya huu ambao uko wazi kujaribu kuichonganisha CUF na watanzania ambao wanategemea sana mchango wa CUF katika ustawi wa demokrasia ya kweli na maendeleo ya nchi yetu.

Julius Mtatiro,
Naibu Katibu Mkuu,
Chama Cha Wananchi CUF Tanzania Bara,
(Safarini JOHANNESBURG-Afrika ya Kusini),
09 Novemba 2013.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni