Habari

Jumatano, 10 Desemba 2025

ZANZ ADAPT ILIVYOBADILISHA MATUMIZI YA MITANDAO NA KUWA FURSA KWA BIKOMBO FAKI

.
Na  Is haka Mohamed Rubea.
    KATIKA kijiji cha Kiuyu Minungwini, Pemba wilaya Wete , ndiko maisha halisi anayoishi anaishi Bikombo Faki Ali, mwanamke jasiri, mkulima wa kilimo mseto, mfanyabiashara mdogo na mwanaharakati wa masuala mbali mbali ya kijamii. 
Safari yake ya maisha imekuwa kielelezo cha mfano wa kuigwa  na  mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi  wanawake na uongozi, ZANZ ADAPT  unaotekelezwa na  Jumuia ya uhifadhi wa misitu Pemba C FP, Jumuia ya uhifadhi wa misitu kimataifa CFI, na TAMWA  ZNZ unaofadhiliwa na Canada Global Affairs, ulivyoweza kubadilisha  maisha katika kilimo , siasa za kijamii na kiuchumi kwa wanawake vijijini. 
Mradi huu, kwa kushirikiana na Community Forests Pemba na Community Forests International, umefungua milango mipya ya fursa kwa wanawake  akiwemo Bikombo, hususan katika matumizi ya mitandao ya kijamii kama WhatsApp na Facebook.
MWANZO WA SAFARI
Bikombo Faki Ali alikulia katika mazingira ya kijijini ambapo kilimo ndicho uti wa mgongo wa familia nyingi Ikiwemo familia yake yenye jumla ya watoto nane  na baba wa familia hiyo. Akiwa mkulima wa kilimo aliebadilisha maisha yake ya kilimo kutoka kilimo cha mazoea alichokuwa akilima hadi kulima kilimo  mseto,mara baada ya kupata fursa ya kushiriki mafunzo yamradi huo wa ZANZ ADAPT  alijikita katika mazao ya chakula miti ya matunda huku nje ya kilimo anaendelea na  biashara ndogo ndogo ili kuendesha maisha ya familia yake.
 Bikombo Alitamani kushiriki katika uongozi wa kijamii na kisiasa, akiamini kwamba sauti ya mwanamke ni muhimu katika maamuzi ya maendeleo ya jamii.
Mnamo septembe Mwaka huu  2025, Bikombo alijaribu kugombea nafasi ya udiwani katika wadi yake ya Kiuyu, kupitia CCM Ingawa hakufanikiwa kushinda,wala kupita katika hatua zake za awali  hatua yake ilibaki kuwa alama ya ujasiri na uthubutu wa mwanamke kijijini kuingia katika ulingo wa siasa. Changamoto alizokutana nazo zilimfundisha kuwa siasa si rahisi, hasa kwa wanawake wanaotoka vijijini, lakini pia zilimpa msukumo wa kutafuta njia mpya za kushirikiana na jamii yake.
MAFUNZO YA TAMWA ZANZIBAR
Mabadiliko makubwa yalikuja baada ya Bikombo kushiriki mafunzo yaliyotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar, huko Mkanjuni  Chake chake Kupitia mradi wa Zanz Adapt, alijifunza kuhusu uongozi, usawa wa kijinsia, na namna ya kutumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, kama nyenzo ya kuelimisha na kushirikisha jamii,kujifunza kutafuta elimu kutoka kwa wengine jambo ambalo awali halikuwa katika akili yake kutumia mitandao ya kijamii .
 Mafunzo haya yalikuwa na lengo la kuwajengea wanawake uwezo wa kushiriki kikamilifu katika uongozi na kupaza sauti zao katika masuala ya kijamii na kisiasa na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Kwa Bikombo, mafunzo haya yalikuwa kama mwanga mpya, alianza kutumia mitandao ya kijamii  kujifunza ,na kuiga manendeleo ya wakulima na wafanya biashara wanawake walioko nje ya  Tanzania na akiamini kuwa mitandao ya kijamii siyo tu mahali pa mawasiliano ya kijamii, bali ni jukwaa lenye nguvu la kuhamasisha, kuelimisha na kushirikisha jamii katika mijadala ya maendeleo. 
WhatsApp na Facebook, ambazo awali alizitumia kwa mawasiliano ya kifamilia na biashara ndogo ndogo, sasa zikawa nyenzo za harakati na uongozi.

MITANDAO YA KIJAMII KAMA FURSA
Baada ya mafunzo, Bikombo alianza kutumia WhatsApp na Facebook kwa njia mpya, Aliunda vikundi vya WhatsApp vya wakulima na wanawake wajasiriamali wadogo, ambapo walijadiliana kuhusu changamoto za kilimo, masoko ya bidhaa, na mbinu za kuongeza kipato. Kupitia Facebook, alishiriki simulizi za maisha ya wanawake wa Kiuyu, akihamasisha jamii kuhusu umuhimu wa usawa wa kijinsia na nafasi ya mwanamke katika uongozi.
Ambapo  kwa mtandao wa kijamii wa facebook anajulikana kama KIUYU JITENGE.
Mitandao hii ilimsaidia kuunganisha wanawake wenzake na wadau wa maendeleo,Aliweza kufikisha ujumbe wake kwa haraka na kwa uwazi, na kwa mara ya kwanza alihisi kuwa sauti yake inasikika zaidi ya mipaka ya kijiji chake.
 Hii ilikuwa hatua kubwa ya kuondoa vikwazo vya kijamii vilivyokuwa vinawazuia wanawake kushiriki kikamilifu katika mijadala ya maendeleo.

Mwanamke Mkulima, Mfanyabiashara na Mwanaharakati
Mbali na siasa, Bikombo aliendelea na shughuli zake za kilimo mseto. Alilima mazao mbalimbali kwa ajili ya chakula na biashara, akitumia mitandao ya kijamii kutafuta masoko mapya. Kupitia WhatsApp, aliweza kuwasiliana na wateja na wauzaji wa pembejeo, jambo lililomsaidia kupunguza gharama na kuongeza faida.

Aidha, kama mfanyabiashara mdogo, alitumia Facebook kutangaza bidhaa zake, kuanzia mazao ya shambani hadi bidhaa ndogo ndogo alizokuwa akiuza sokoni. Hii ilimsaidia kupanua wigo wa biashara yake na kujenga mtandao wa wateja wapya. Mitandao ya kijamii ikawa daraja la kumtoa kijijini na kumfikisha sokoni kwa urahisi.
CHANGAMOTO NA MAFANIKIO
Safari ya Bikombo haikuwa rahisi. Alikumbana na changamoto za kijamii, ikiwemo mitazamo ya baadhi ya watu waliodhani kwamba mwanamke hawezi kushiriki kikamilifu katika siasa au uongozi. 
Pia, alikabiliana na changamoto za kiuchumi na ukosefu wa rasilimali za kutosha kuendesha kampeni zake za kisiasa. Hata hivyo, kupitia mafunzo na msaada wa mradi wa Zanz Adapt, alijifunza mbinu za kushinda changamoto hizi.

Mafanikio yake yalionekana katika namna alivyoweza kuhamasisha wanawake wenzake kushiriki katika mijadala ya kijamii na kisiasa. Ingawa hakushinda nafasi ya udiwani, alibaki kuwa kiongozi wa kijamii, akihamasisha na kuelimisha jamii kupitia mitandao ya kijamii. Alikuwa mfano wa kuigwa kwa wanawake wengine wa Kiuyu na Pemba kwa ujumla.

ATHARI ZA MRADI
Mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya wanawake na uongozi umeleta mabadiliko makubwa kwa wanawake vijijini. Kwa Bikombo, mradi huu umemsaidia kubadilisha mtazamo wake wa maisha na kumpa ujasiri wa kushiriki kikamilifu katika uongozi na maendeleo ya jamii. Kupitia mitandao ya kijamii, amekuwa daraja la kuunganisha wanawake na wadau wa maendeleo, na sauti yake imekuwa ikisikika zaidi ya mipaka ya kijiji chake.
Kwa sasa Bikombo anaendelea kusubiri ,mafanikio makubwa katika kilimo mseto ambacho alianza hivi karibuni  mara baada ya kuzinduliwa kulima kilimo kinachokabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi na programu hiyo ya zanz adapt.
mwisho

Hitimisho
Simulizi ya Bikombo Faki Ali ni ushuhuda wa nguvu ya elimu, mafunzo na teknolojia katika kubadilisha maisha ya wanawake vijijini. Kutoka kuwa mkulima wa kilimo mseto na mfanyabiashara mdogo, amekuwa mwanaharakati na kiongozi wa kijamii anayehamasisha wanawake kushiriki kikamilifu katika uongozi. Mitandao ya kijamii, hususan WhatsApp na Facebook, imekuwa nyenzo muhimu ya kufanikisha harakati zake.

Ingawa hakufanikiwa kushinda nafasi ya udiwani, Bikombo amefanikiwa kushinda mioyo ya wanawake na jamii yake kwa ujumla. Ameonyesha kwamba uongozi si lazima uwe na vyeo, bali ni uwezo wa kuhamasisha na kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Mradi wa Zanz Adapt, kwa msaada wa TAMWA Zanzibar na wadau wake, umeandika historia mpya ya wanawake vijijini kama Bikombo, historia ya ujasiri, uthubutu na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi.

Bikombo  Faki Ali  anaejivunia kujengewa uwezo wa kuvitumia vyombo vya Habari  ,waandishi  na mitandao ya kijamii kwa Matumizi Sahihi  ili kuendeleza harakati zake anazozifanya za kupambana na athari za mabadiliko ya  ambae  anaamini  ndio fursa pekee iliyobaki kwakwe kujikomboa na shughulo zake bila woga.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni