Habari

Jumanne, 15 Oktoba 2013

JK, Mbowe, Lipumba,Mbatia wakubaliana

NA MUHIBU SAID

16th October 2013
Chapa
Rais Jakaya Kikwete, akiagana na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, Ikulu jijini Dar es Salaam jana baada ya mazungumzo na viongozi vyama vya upinzani. Nyuma kushoto ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Professa Ibrahim Lipumba.
Rais Jakaya Kikwete jana alikutana na viongozi wa vyama sita vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, Ikulu, jijini Dar es Salaam na kukubaliana mambo makuu mawili.

La kwanza, vyama vyote vya siasa vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013, kuyawasilisha haraka serikalini ili kutafuta namna ya kuyashirikisha katika marekebisho ya sheria hiyo.

La pili, vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano wa jinsi kwa pamoja vitakavyosukuma mbele mchakato mabadiliko ya katiba ya nchi kwa maslahi mapana ya nchi na mustakabali wa taifa.

Katika makubaliano hayo, Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimepewa jukumu la kuratibu jambo hilo, ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, mkutano kati ya Rais Kikwete na viongozi ulimalizika jana jioni na pande mbili hizo kukubaliana mambo hayo.

Viongozi wa ambao Rais Kikwete alikutana nao jana kwa mazungumzo hayo wanatoka vyama vya CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, TLP na UDP.

Viongozi hao walianza kuwasili kwa nyakati tofauti, kuanzia saa 6:00 mchana jana na kupokelewa na maofisa usalama wanaotoa huduma mapokezi, Ikulu, kabla ya kuelekezwa kwenye chumba maalumu kilichoandaliwa kwa ajili ya mazungumzo kati yao na Rais Kikwete.

Walioanza kuwasili Ikulu katika muda huo, ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia, akiongozana na Martin Mng’ong’o kutoka chama hicho.

Baada ya Mbatia kuwasili Ikulu muda mfupi, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alifika ambaye ndiye msemaji wa viongozi hao.

Profesa Lipumba aliongozana na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, Julius Mtatiro na Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Habib Mnyaa.

 Dakika chache baadaye, aliwasili Mwenyekiti wa Chadema, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe.

Mbowe aliongozana na Mkurugenzi wa Katiba na Sheria wa Chadema, ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi hiyo na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.

Viongozi hao walifuatiwa na wenzao kutoka CCM, UDP na TLP kuwasili Ikulu muda mfupi baadaye.

Hao ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula; Isaack Cheyo, aliyemwakilisha Mwenyekiti wa UDP, ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo.

Wengine ni Nancy Mrikaria aliyemwakilisha Mwenyekiti wa TLP, ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema.

Ujumbe wa serikali pia iliwahusisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, baadaye jana jioni, Cheyo na Mrema wako nje ya nchi.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa viongozi hao walikutana na Rais Kikwete, Ikulu katika mazingira ya maelewano na mwafaka.

Katika mazungumzo hayo, vyama vitatu vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi viliwasilisha waraka wa ushirikiano wa vyama vya upinzani kwa Rais Kikwete.

Waraka huo unamshauri Rais Kikwete kutumia mamlaka yake ya Kikatiba kukataa kuukubali muswada huo, ambao vyama hivyo viliulalamikia kuwa una kasoro.

Muswada huo uliopitishwa na Bunge Septemba 6, mwaka huu, unasubiri kusainiwa na Rais ili uanze kutumika kama sheria rasmi.

“Ushauri wetu unatokana na imani yetu kwamba endapo muswada huu utapata ridhaa yako na kuanza kutumika kama sheria utakuwa na madhara makubwa kwa mchakato mzima wa utungaji wa Katiba Mpya na kwa amani na utulivu wa nchi,” inaeleza sehemu ya waraka huo uliosainiwa na Mbowe, Profesa Lipumba na Mbatia.

USHIRIKISHWAJI HAFIFU WA WANANCHI

Waraka huo unataja sababu mbalimbali za tishio hilo kuwa ni pamoja na ushirikishwaji hafifu wa wananchi, hasa wadau wa kitaasisi au binafsi kutoka Zanzibar katika kuuchambua na kuutolea maoni muswada huo.

USHIRIKISHWAJI HAFIFU WA SMZ
Sababu nyingine ni ushirikishwaji hafifu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, Abubakar Khamis Bakari, aliwahi kukaririwa akisema hadharani kwamba ushirikishwaji wa SMZ ulihusu vifungu vinne tu vya muswada huo.

Lakini akasema vifungu vingine vyote vya muswada vilivyopitishwa na Bunge havikupelekwa Zanzibar na kwa hiyo, SMZ haikushirikishwa kwenye kuvitolea maoni na msimamo.

BUNGE MAALUMU LA KATIBA
Waraka huo unadai kuwa muswada huo umefanya mabadiliko makubwa kuhusu utaratibu wa kuunda Bunge Maalumu la Katiba, ikiwamo Rais kuwa na mamlaka kisheria ya kuteua wajumbe 166 wa Bunge hilo wasiokuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Pili, siyo lazima tena kwamba wajumbe hao 166 watokane na makundi ya kijamii.

“Mabadiliko haya hayakuwapo kwenye Muswada uliosomwa kwa mara ya kwanza Bungeni mwezi Mei mwaka huu, na wala hayakutolewa maoni na wadau walioalikwa mbele ya Kamati. Aidha, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikujulishwa juu ya marekebisho haya na wala haikuyatolewa maoni na msimamo wake,” unaeleza waraka huo.

IDADI YA WAJUMBE WA BUNGE MAALUMU
Waraka huo unasema Bunge hilo litakuwa na wajumbe 604, yaani wabunge 357, wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar 81 na wajumbe wengine 166.

“Hali hii isiporekebishwa itakuwa na maana kwamba Katiba Mpya itatokana na matakwa ya vyama vya siasa ambavyo idadi ya jumla ya wanachama wao haifiki milioni kumi kati ya Watanzania zaidi ya milioni 45 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012,” unaeleza waraka huo.

Mengine yanahushu uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge Maalumu la Katiba, utaratibu wa kupitisha Katiba Mpya kwenye Bunge Maalumu, ukomo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuingizwa kwenye muswada mambo ambayo hayakujadiliwa wala kupitishwa na Bunge.

“Kwa ajili hiyo, tunakuomba utumie mamlaka yako kama Rais na Mkuu wa Nchi yetu chini ya ibara ya 97(2) ya Katiba, ukatae kuukubali muswada huu na badala yake uelekeze urudishwe Bungeni kwa sababu ambazo tumezieleza katika maelezo yetu haya,” unaeleza waraka huo.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni