Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa vyama vya siasa vya CCM, Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi, TLP na UDP wamekubaliana mambo mawili makubwa baada ya kuweka pembeni tofauti za kiitikadi na kutanguliza masilahi ya taifa walipokutana jana Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliitishwa na Rais Kikwete ili kuondoa sintofahamu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa Septemba na Bunge lilipokutana mjini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana jioni ilisema katika mkutano huo ilikubaliwa kwamba vyama vyote vya siasa nchini vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba viwasilishe mapendekezo yao haraka serikalini ili ifatutwe namna ya kuyashirikisha mapendekezo hayo katika marekebisho ya sheria hiyo.
Pia Rais na vyama hivyo walikubaliana kwamba vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba Mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano kwa lengo la kusukuma mbele mchakato huo kwa masilahi mapana ya nchi yao na mustakabali wa taifa.
“Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimepewa jukumu la kuratibu jambo hilo ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini,” iliongeza taarifa hiyo.
Viongozi wa vyama vyama vya siasa waliohudhuria mkutano huo ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, Isaack Cheyo ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo na Nancy Mrikaria ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema. Cheyo na Mrema wako nje ya nchi.
Wengine ambao waliambatana na wenyeviti wao ni Mohamed Mnyaa na Julius Mtatiro wa CUF, Tundu Lissu na John Mnyika wa Chadema na Martin Mng’ongo wa NCCR-Mageuzi.
Vicheko Ikulu
Vicheko na bashasha vyatawala Ikulu
Ilikuwa fursa kwa Rais Kikwete kukutana na viongozi hao baada ya kipindi cha miezi miwili cha kurushiana maneno baina ya viongozi wa Bunge, Serikali, CCM waliokuwa wakivutana na viongozi wa vyama vitatu vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi.
Kama mtu yeyote angeulizwa kutabiri katika tukio lililotokea jana lingetokea basi angekuwa na wakati mgumu kutokana na ukali wa maneno na malumbano katika kipindi chote baada ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge wa Septemba.
CHANZO- MWANANCHI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni