Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, amesema anatarajia Katiba Mpya itabainisha umri wa msichana kuolewa ni miaka 18 na kuondoa utata wa kisheria na kukomesha ndoa za utotoni.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika kikao cha wadau mbalimbali kujadili namna ya kukomesha ndoa za utotoni ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike Duniani.
Waziri Chikawe alisema kwa sasa kuna mkanganyiko wa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inayobainisha kuwa mwanamke na mwanaume wawe wametimiza umri wa miaka 18 ili wafunge ndoa, hata hivyo mwanamke anaweza kuolewa akiwa na umri wa chini ya miaka18 lakini siyo chini ya miaka 15 kama atapata idhini ya wazazi au kama wote wamefariki idhini itatolewa na mlezi wa binti huyo.
“Kisheria mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 hawezi kuingia kwenye mkataba. Na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998 (SOSPA) inatamka wazi kuwa mwanamume atajayejamiiana na msichana mwenye umri chini ya miaka 18 hata kama ameridhia ni mbakaji na atahukumiwa kwa mujibu wa sheria.Huu ni mgongano wa kisheria,”alisema.
Alisema hatua hiyo itasaidia kujenga mazingira mazuri ya kukomesha ndoa za utotoni na kuwapa fursa wasichana kukua vyema na kupata elimu ambayo ni haki yao ya msingi.
Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa),Valerie Msoka alisema anatiwa moyo na hatua hiyo ya serikali, lakini akatoa angalizo kwamba kuwa na sheria nzuri ni jambo na utekelezaji ni jambo jingine “tunataka kuona utekelezaji wa vitendo ili kuwanusuru wasichana na ndoa za utotoni,” alisema.
Mke wa Rais wa Afrika Kusini, Graca Machel, katika ujumbe wake kwa nijia ya video alisema ni muhimu kukaimarisha usajili wa ndoa na vifo vya wasichana wadogo ili ukubwa wa tatizo lifahamike na kuhakikisha kuwa watoto wanapata fursa ya elimu, kuondoa umaskini na haja ya kukomesha ndoa za utotoni.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye kiwang cha juu cha ndoa za utotoni duniani na inakadiriwa kuwa wasichana wawili wa Tanzania kati ya watano watakuwa wameolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.Kiwango hiki cha juu kinachangia kukwamisha wasichana kupata elimu, kupata mimba na kuhatarisha maisha yao kutokana na matatizo ya afya ya uzazi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni