Habari

Jumatatu, 14 Oktoba 2013

UVCCM: viongozi CUF wanahatarisha SUK

na Mwandishi wetu, Zanzibar

UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umewatuhumu baadhi ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kuhatarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Viongozi wanaotuhumiwa ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Ismail Jussa Ladhu, na Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, Aboubakari Khamis Bakari.
Tuhuma hizo zilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Shaka Hamdu Shaka alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi Kuu ya Jumuia Maisara mjini Unguja.
Alisema viongozi hao wamekuwa na tabia ya kuwashambulia wenzao walio kwenye serikali hiyo ya umoja wa kitaifa sambamba na kuvujisha siri za vikao mbalimbali.
Shaka alisema pia wamesikitishwa na tamko la Umoja wa Vijana wa CUF kuwataka wanachama wao waanze kufanya mazoezi ya viungo.
“Tamko la vijana wa CUF linaweza kuhatarisha uvunjifu wa amani na kuvuruga malengo ya kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, sisi tunalikemea,” alisema.
Alibainisha kuwa kuundwa kwa serikali hiyo kulilenga kudumisha amani, utulivu na mshikamano baina ya wananchi wa visiwa hivyo pamoja na vyama vya CCM na CUF.
Shaka alimlaumu Maalim Seif kwa kukiri kuwa mtiifu kwa Rais mstaafu Dk. Amani Karume huku akiahidi kushirikiana naye kusaka mamlaka kamili ya Zazibar katika mfumo wa muungano badala ya Rais aliyemteua na kumuapisha kiapo cha kishesria Dk. Ali Mohamed Shein.
Shaka alisema tangu ianzishwe SUK vitendo vya uvunjifu wa amani pamoja na ubaguzi vimekithiri kiasi cha kusababisha hali ya wasiwasi kwa wananchi.
Chanzo Tanzania daima

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni