Habari

Jumapili, 13 Oktoba 2013

Maalim Seif : Hatujaunganisha vyama, tumeunganisha nguvu kupinga muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba

Monday, October 14, 2013

 Mfuasi wa CUF akifuatilia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Jadida Wete, wakati Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad akihutubia
 Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (CUF) Salim Bimani akitoa dondoo kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika viwanja vya Jadida Wete.
 Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Hamad Massoud Hamad, akitoa dondoo kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika viwanja vya Jadida Wete.
 Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wafuasi wa Chama hicho kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Jadida Wete.
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wafuasi wa Chama hicho kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Jadida Wete. (picha na Salmin Said, OMKR).
 
Na Hassan Hamad OMKR
 
Wakati viongozi wa vyama vya upinzani wakijiandaa kukutana na Rais Jakaya Kikwete tarehe 15 mwezi huu, Chama Cha Wananchi (CUF) kimesema hakijaungana na chama chochote cha siasa.
 
Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad amesema walichofanya ni kuunganisha nguvu za kupinga muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba, na wala sio kuunganisha vyama kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
 
Maalim Seif ametoa kauli hiyo katika viwanja vya Jadida, Wilaya ya Wete Pemba, wakati akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama hicho.
 
Amefahamisha kuwa kila chama kina sera zake na malengo yake, na kamwe vyama hivyo havijaungana isipokuwa kuunganisha nguvu kwa lengo la kupinga muswada huo ambao unadaiwa kupitishwa na kukosa ridhaa ya wabunge wa vyama vya upinzani.
 
Hivi karibuni vyama vya upinzani vya CUF, CHADEMA, na NCCR Mageuzi, vilitoka katika kikao cha Bunge vikipinga kupitishwa kwa muswada huo na baadaye kuamua kuunganisha nguvu kwa lengo la kutetea hoja yao.
Hata hivyo Maalim Seif amesema vyama hivyo vitaendelea kumshauri Rais Jakaya Kikwete asitie saini muswada huo, na badala yake urejeshwe Bungeni ili ujadiliwe upya.
 
Akizungumzia kuhusu uchumi, Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amewata wananchi kushiriki kikamilifu kuliokoa zao hilo ambalo ndio tegemeo la uchumi wa Zanzibar.
 
Aidha amewahimiza wakulima wa zao hilo kutumia vifaa vinavyokubalika   wakati wa kukausha karafuu hizo ili kudhibiti ubora wa zao unaosifiwa duniani kote.
 
Amewaagiza wakulima wa zao hilo kuuza karafuu zao katika vituo vya shirika la biashara la Zanzibar (ZSTC), na kuepuka kabisa vitendo vya kuuza karafuu kwa njia za magendo.
 
Amesema katika kuwahamasisha zaidi wakulima kuuza karafuu zao katika vituo vya ZSTC, Serikali inakusudia kuviimarisha vituo vya ununuzi wa karafuu, ikiwa ni pamoja na kuweka vikalio pamoja na viburudishaji.
 
Wakati huo huo Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Hamad Massoud Hamad amesema chama hicho kinakusudia kuwafungulia mashtaka masheha watakaowanyima wananchi vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZAN ID), bila ya kuwepo sababu za msingi.
 
Amesema Chama hicho kitalazimika kutafuta mawakili kwa gharama zozote kuendesha kesi hizo, ili kuhakikisha kuwa Wazanzibari wenye sifa hawanyimwi haki ya kupata vitambulisho hivyo na kupiga kura.
 
Kwa upande mwengine Mhe. Hamad Massoud amewasisitiza wananchi wa kisiwa cha Pemba waliotimiza masharti kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uandikishaji wapiga kura wapya linaloendelea katika Wilaya nne za Pemba.
 
Zoezi hilo limeanza rasmi katika Wilaya ya Micheweni na litaingia katika Wilaya ya Wete kuanzia tarehe 19 hadi 24 mwezi huu.
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni