MOJA ya taarifa ambazo zilinishtua ni ile aliyotoa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Seif Sharif Hamad, ya kutangaza azima yake ya kuendelea kugombea urais visiwani humo pamoja na ukatibu mkuu wa Chama chake cha Wananchi (CUF).
Nasema ilinishtua kutokana na kauli yake kutoa tafsiri kuwa CUF haina watu walio na uwezo wa kuongoza nafasi hiyo wakati ninaamini wapo wengi, tena wanaoweza kusababisha chama hicho kung’ara.
Hamad alitangaza msimamo huo alipokuwa akizungumzia miaka mitatu ya utendaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Awamu ya Saba, katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View.
Alisema kuwa atastaafu siasa pale atakapoishiwa nguvu mwilini, kwamba licha ya watu kumuona kuwa ni kizingiti kwa matakwa yao, hataacha nia yake hiyo ya kuongoza Wazanzibari.
“Hamuwezi kwa matakwa yenu kuona Seif ni kizingiti niondoke, siondoki! Mimi nitaendelea kuwatumikia Wazanzibari, ndiyo ahadi yangu niliyotoa labda nipate maradhi au niishiwe nguvu,” alisema Hamad baada ya kuulizwa swali kuwa anafananishwa na Robert Mugabe wa Zimbabwe kwa kung’ang’ania madaraka.
Kuhusu kugombea tena nafasi yake ya ukatibu mkuu katika uchaguzi wa CUF utakaofanyika mwakani na urais wa Zanzibar mwaka 2015, Seif alisema kuwa atatoka tu endapo wanachama watakapofanya uamuzi wa kutomchagua.
Mfukunyuku anajua kuwa uchambuzi huu unaweza kumletea upinzani mkubwa sana kwa baadhi ya watu ambao hawataki kusikia mtu akimsema kwa hoja Maalim Seif.
Kwa bahati mbaya hao wanaoweza kupinga ni wale wanaompenda kiongozi huyo kutokana na muonekano wake au utendaji wake katika chama na siasa lakini hawana hoja zenye mashiko juu ya kiongozi huyo.
Ninaweza kuwa mmoja wa wale wengi wasiokubali Maalim Seif kuendelea kuomba kuongoza nchi kwa nafasi ya urais, sitaki kuzungumzia kichama, inawezekana ana uwezo ingawa hata kwa utafiti mdogo utaona wazi kuwa hana nguvu tena za kutakiwa kuwania nafasi hata hiyo ya ukatibu mkuu kwa kuwa chama hicho kimeshindwa kupigania kuwa na wabunge wengi Bara ukiacha huko Zanzibar.
Ni muhimu kwa taifa letu hasa katika kipindi tunachoelekea cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kuwa na mijadala mipana kuhusu watu wanaotaka kugombea nafasi kubwa na nyeti hapa nchini kama urais.
Rais hawezi kuchaguliwa eti kwa vile ametoka katika chama fulani, dini fulani, ana mwonekano mzuri au kabila fulani au ana nguvu kama zile alizosema Maalim Seif.
Mfukunyuku anaona kuwa ni muhimu rais akachaguliwa kutokana na ajenda anazoleta mezani. Tunakumbuka Rais wa Marekani, Barack Obama alikuja na sera za mabadiliko (change) na Wamarekani watamhukumu kwa hilo. Rais Jakaya Kikwete alikuja na ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania’ na ndiyo maana Watanzania wamekuwa wakihoji juu ya hilo kwa kuwa hadi sasa bado Watanzania wengi ni maskini.
Wengi hawana kipato cha uhakika, ajira zimekuwa ni tatizo sugu ambalo limekosa ufumbuzi, yupo Mtanzania ambaye hana uhakika na mlo wake. Hivyo tunapomuona Rais Kikwete tunahoji juu ya utekelezaji wa kaulimbiu yake ya Maisha bora kwa kila Mtanzania ameweza kuitekeleza kwa asilimia ngapi.
Hivyo tunapokuja katika hoja ya Maalim Seif ni lazima tujiulize maswali ya aina hiyo, Maalim Seif pamoja na kusema kuwa atagombea hadi pale wananchi watakapomchoka lakini atawasilisha hoja gani mezani? Isije ikawa ni aina ya kiongozi kama Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe.
Ndiyo si tunaona Mugabe alivyoendelea kung’ang’ana na urais kama vile hakuna Mzibabwe anayeweza kuongoza katika nafasi hiyo, lakini yote hiyo inatokana na ubinafsi na ulevi wa madaraka.
Cha Muhimu ni lazima Maalim Seif aoneshe ni kitu gani atakachoifanyia Tanzania kama akifanikiwa kuukwaa urais ili Watanzania kwa ujumla wawe na hoja za msingi za kumuuliza lakini si hizo hoja dhaifu alizoibuka nazo.
Ndiyo naziita dhaifu kwa kuwa sitaki kuamini kuwa CUF haina watu walio na uwezo huko Zanzibar wa kuwania nafasi hiyo. Ninaamini kuwa wapo wengi wasomi wanaoweza kuibadilisha CUF na kuwa bora zaidi ya hapo ilipo.
Mfukunyuku anataka kufahamu kuwa mwaka 2015 si mbali, na kwa mara nyingine tena Watanzania tutapata fursa ya kutumia haki yetu ya kikatiba kuchagua viongozi ambao tunaamini kwamba watatufaa kutuongoza kama taifa katika hiki kipindi kigumu cha uchumi kinachotuathiri kwa miaka zaidi ya 51 sasa.
Baadhi ya wachambuzi wa siasa wamekuwa wakimuona Maalim Seif, kama ni mwanasiasa asiyetabirika, asiyefahamika analenga jambo lipi na kwa wakati upi, zaidi akiwa na tabia ya kutokubali kubaki nyuma ya mwingine au kupingwa kwa fikra zake.
Ni muhimu Maalim Seif akafahamu kuwa chama hicho kina wenyewe na hao ndiyo wenye uamuzi wa kutaka nani awanie urais na nani hafai, hivyo hatua ya yeye kung’ang’ania nafasi hiyo tunaweza kuifananisha na uroho wa madaraka na kiongozi wa aina hiyo hafai kupendekezwa kuwania nafasi hiyo, kwa kuwa anaweza kusababisha mgogoro kichama hata kitaifa.
Kiongozi makini mara zote anapaswa kuwapa nafasi wananchi waaamue na si yeye kung’ang’ania apendekezwe katika nafasi ya urais. Hivyo Maalim Seif ni mgeni mwalikwa ndani ya CUF, nasema hivyo kwa kuwa wapo waanzilishi wa chama hicho ambao hawajawahi kung’ang’ania kuongoza nafasi zozote ndani ya chama hicho kama ilivyo kwa mgeni mwalikwa Maalim Seif.
Historia ya chama hicho inasema kuwa kazi kubwa ilifanywa na kina Shaaban Khamisi Mloo , Ali Haji Pandu, Hamad Rashid Mohamed, Dk. Maulid Makame na Soud Yussuf Mgeni, ambao walianzisha vuguvugu la Kamahuru wakati wa chama kimoja na baadaye CUF.
Inaelezwa kuwa wakati juhudi za kuleta mageuzi ya kisiasa na kidemokrasia visiwani zikifanyika kwa njia za siri, Maalim Seif alikuwa kizuizini na hakujua kilichokuwa kikiendelea. Lakini kutokana na chama kumuamini na kumpa nafasi ya uongozi katika ngazi za juu akajiona kuwa ni mwenyeji ndani ya chama hicho na kufikiri kuwa hakuna wengine wenye uwezo wa kuwania nafasi za juu hasa urais, hilo atakuwa anajidanganya na anakosea.
Mfukunyuku anaona kuwa wakati umefika kwa CUF pamoja na Watanzania kwa ujumla kutafuta viongozi walio na staha na walio tayari kuchukua ushauri wanaopewa kuliko kwa Maalim Seif ambaye baadhi ya watu wameondolewa chamani na wengine kukihama kutokana na kutoa ushauri wa kuboresha chama hicho ambapo Maalim Seif aliwaona kama vibaraka.
Hivyo Maalim Seif hafai kupewa fursa nyingine ya kuwania nafasi hizo kwani hayupo tayari kuchukua ushauri wa wananchi wake. Ifike mahali kiongozi huyo akubali kuwa wapo Wana CUF walio na uwezo wa kuleta mabadiliko ndani ya chama na chama kikaweza kufanya vema.
Kitendo cha kutangaza kuwania nafasi hiyo ni kuonekana kuwa mbinafsi na mtu asiyependa mabadiliko, vema akawaachia Wana CUF wakaamua wanayemtaka wa kutaka kuongoza nafasi hiyo kwa kuwa uongozi ni sehemu ya kupokezana vijiti.
CHANZO- TANZANIA DAIMA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni