Habari

Jumapili, 27 Oktoba 2013

Walimu wakuu wabovu wanavyoua elimu Tanzania


Wakati Serikali ikiendelea kuikalia ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matokeo ya Kidato cha Nne iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda mapema mwaka huu, baadhi ya wajumbe wake wameanika madudu mengi yaliyobainika katika uchunguzi huo.


Mmoja wa wajumbe waliounda Tume hiyo ameliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa waligundua mambo mengi yanayodhihirisha udhaifu mkubwa katika uendeshaji wa sekta ya elimu nchini, ikiwa ni pamoja na kubaini kuwa idadi kubwa ya wakuu wa shule hawana elimu ya shahada.
Alieleza kuwa kiutaratibu mkuu wa shule anatakiwa kuwa na elimu isiyopungua shahada pamoja na mafunzo ya uongozi na usimamizi. “Kumbukumbu zilionyesha kuwa elimu ya sekondari ya kawaida ina jumla ya shule 4,528. Wakuu wa shule 1,498 wana shahada ya kwanza au zaidi, 1,703 wana stashahada, 33 wana sifa nyingine” alisema.
Sehemu kubwa ya matokeo ya uchunguzi huo inasemekana yamejikita zaidi katika kuzitupia lawama taasisi za Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) na Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE).
Udhaifu wa kiutendaji kati ya taasisi hizo mbili unadaiwa umechangia kwa wanafunzi wengi kufanya vibaya kwenye mitihani ya kidato cha nne mwaka jana, kiasi cha kuilazimisha Serikali kuunda tume kuchunguza tatizo kutokana na kilio kikubwa cha wadau wa elimu na wananchi.
Matokeo hayo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana yanaonyesha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 walipata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 wakiwa wamepata daraja la nne.
Katika mtihani huo, watahiniwa 397,136 walikuwa wa shuleni na 68,806 wa kujitegemea.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu Pinda aliamua kuunda Tume iliyoanza kufanya kazi kuanzia Machi hadi Juni mwaka huu. Tume hiyo iliyokuwa inaongozwa na Profesa Sifuni Mchome ilimkabidhi Waziri Mkuu ripoti Juni 15, mwaka huu.
Hata hivyo, ripoti hiyo haijawahi kutolewa hadharani baada ya Tume kumaliza kazi yake, huku Profesa Mchome ambaye alikuwa Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Vyuo Vikuu Tanzania akipandishwa cheo na kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Kauli ya Profesa Mchome
Profesa Mchome alipotafutwa jana kuzungumzia kuhusu upatikanaji wa wakuu wa shule alisema, “Mimi hivi sasa ni katibu mkuu wa wizara siwezi kuzungumzia hilo, kwanza sijaiona hiyo ripoti. Ukitaka ufafanuzi mzuri mtafute Kamishna wa Elimu.”
Gazeti hili lilimtafuta kamishna huyo pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Philipo Mulugo bila mafanikio kwani simu zao zilikuwa zikiita bila majibu.
CHANZO- MWANANCHI.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni