NA HELLEN MWANGO
14th October 2013
B-pepe
Chapa
Hatua hiyo ilifikiwa na TRAB baada ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kukubaliana na kampuni za huduma za simu za mkononi kwa kufikia uamuzi wa pamoja kusimamisha utekelezaji wa taarifa yake kuzitaka kampuni hizo kuwasilisha makusanyo ya kodi hiyo. Oktoba Mosi, mwaka huu TRAB ilisimamisha utekelezaji wa sheria hiyo baada ya makubaliano kati yake na kampuni za simu nchini.
Septemba 25, mwaka huu, TRA iliziandikia barua kampuni hizo ikizitaka ziwasilishe makusanyo ya kodi ya simu kutoka kwa wateja wake ya mwezi Julai pamoja na riba kwa kuchelewa kuwasilisha kodi hiyo.
Aidha, taarifa hiyo ya TRA dhidi ya kampuni hizo ilikuwa ni utekelezaji wa Marekebisho ya mwaka 2013 ya Sheria namba 4 ya Fedha, yaliyoelekeza kila kadi ya simu kutozwa kodi ya Sh. 1,000 kwa mwezi.
Hata hivyo, kampuni hizo zilikata rufaa katika TRAB zikipinga utekelezaji wa sheria hiyo, pamoja na mambo mengine zikipinga kutupiwa jukumu la kukusanya kodi hiyo kutoka kwa wateja wake. Mbali na rufaa hiyo, pia kampuni za simu ziliwasilisha maombi ya zuio la muda la utekelezaji wa sheria hiyo, kama barua ya TRA ilivyozitaka, ili kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa rufaa zake, katika bodi hiyo. Kutokana na rufaa na maombi hayo ya kampuni za simu, TRA kupitia kwa mwanasheria wake, Juma Beleko, na wakili wa kampuni hizo, Rosan Mwambo, walikubaliana TRA kusitisha utekelezaji wa madai yake hayo.
Makubaliano mengine yaliyofikiwa na pande zote ni warufani kuondoa maombi yao ya zuio la muda la utekelezaji wa sheria hiyo, rufaa za kampuni zote kuunganishwa na kuwa moja, na kutokuwa na amri ya gharama za maombi hayo
Hata hivyo, TRAB iliridhia makubaliano hayo na kuwa amri yake halali, huku ikiagiza usikilizwaji wa rufaa hizo ufanyike kwa njia ya maandishi ambapo pande zote zimeamriwa kuwasilisha hoja zake za maandishi, na kisha kusubiri hukumu.
Pamoja na TRA na kampuni hizo kufikia uamuzi huo huko TRAB, Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imepanga kusikiliza maombi ya TCAS ya zuio la muda la utekelezaji wa sheria hiyo kodi za simu, Oktoba 21, mwaka huu.
TCAS ilifungua maombi hayo ya zuio la muda la utekelezaji wa sheria hiyo, kusubiri hukumu ya kesi yao ya Kikatiba waliyoifungua mahakamani hapo dhidi ya Waziri wa Fedha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
Katika kesi hiyo TCAS kinapinga Sheria hiyo ya kutoza kodi ya Sh 1,000 kwa kila mwenye kadi ya simu inayotumika, kila mwezi, wakidai kuwa sheria hiyo ni kandamizi na kinyume cha Katiba kwa kuwa itawanyima wengi haki ya mawasiliano.
Mahakama hiyo tayari imesharuhusu makampuni matano ya huduma za simu za mkononi, ya Tigo, Aitel, Vodacom, TTLC na Zantel, kuunganishwa katika kesi hiyo, upande wa walalamikaji.
Kesi hiyo inasikilizwa na Jopo la majaji watatu, linaloongozwa na Mwenyekiti Jaji Aloyisius Mujuluzi, akisaidiana na Lawrence Kaduri na Salvatory Bongole.
CHANZO: NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni