Na Khatib Suleiman – Zanzibar
WAZIRI wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Abubakar Khamis Bakari ameliambia Baraza la Wawakilishi kwamba muswada wa mabadiliko ya Katiba, uliyopitishwa na Bunge na kuzusha malumbano kwa Wabunge wa upinzani, Zanzibar haikushirikishwa katika marekebisho ya vifungu 12 vilivyoingizwa baadaye.
Abubakar alisema hayo wakati alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu ushirikishwaji wa Zanzibar katika mchakato wa marekebisho ya Katiba, ambao katika siku za hivi karibuni umezusha malumbano zaidi kwa kambi ya upinzani.
Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Unguja Ismail Jussa (CUF), alimtaka Waziri wa Katiba na Sheria kufafanua kuhusu kauli zinazotofautiana kuhusu Zanzibar, kushirikishwa au kutokushirikishwa katika mchakato wa Katiba.
Akifafanua, Waziri Bakari alisema awali muswada huo uliletwa serikalini na kufanyiwa marekebisho katika maeneo ya mambo manne ambayo Zanzibar, iliyatolea mapendekezo yake na kupelekwa mbele.
“Marekebisho ya awali yaliletwa serikalini…ambapo mimi binafsi nilitoa mapendekezo kwa niaba ya serikali katika maeneo manne,” alisema Waziri Bakari.
Hata hivyo, alisema ilipofika mwezi wa Mei, kulikuwa na utaratibu mwingine wa kuongeza jumla ya vifungu 12 ambavyo hivyo Zanzibar, haikushirikishwa:
“Mimi Abubakar Khamis Bakari…Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria katika marekebisho ya muswada huo ambapo jumla ya vifungu 12 viliingizwa…sisi Zanzibar hatukushirikishwa,” alisema Waziri Bakari.
Alisema alifanya juhudi za kutafuta muswada huo uliopitishwa Bungeni na kuona mabadiliko hayo ambayo Zanzibar, haikushirikishwa pamoja na kuingizwa kwa vifungu 12 vipya ndani ya Katiba.
Waziri huyo alisema Septemba 13, mwaka huu alimuandikia barua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balosi Seif Ali Idd ambaye naye, aliandika barua kwa ofisi ya Waziri Mkuu, lakini hakuna majibu yaliyotolewa.
Waziri Bakari alisema amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kuwepo kwa kauli mbalimbali zenye utata, ambapo baadhi ya watu pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, wamekuwa wakipotosha ukweli huo katika majukwaa ya kisiasa.
Chanzo: HABARILeo
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni