Wahamiaji haramu wasiopungua 50 wamepoteza maisha yao hapo jana baada ya meli waliyopanda kuzama karibu na kisiwa cha Sicily kusini mwa Italia. Taarifa iliyotolewa na kikosi cha uokoaji cha jeshi la majini la Italia imeeleza kuwa, kikosi hicho kimefanikiwa kuwaokoa wahajiri haramu 200 waliozama majini katika eneo la baina ya kisiwa cha Sicily nchini Italia na Tunisia.
Msemaji wa jeshi la majini la Italia amesema kuwa, mara baada ya kuzama meli iliyowabeba wahajiri hao haramu, jeshi la wanamaji la nchi hiyo kwa kutumia helikopta lilianzisha operesheni kamambe ya kuwaokoa wahajiri hao. Hadi sasa haijajulikana wahajiri hao wanatoka nchi gani.
Tukio hilo limetokea takribani wiki moja tu baada ya kufariki dunia wahajiri haramu 319 kutoka nchi za Eritrea na Somalia, baada ya meli yao kuzama karibu na kisiwa la Lampedusa kusini mwa Italia. Imeelezwa kuwa, mamia ya maelfu ya wahajiri haramu hupanda meli kuukuu na zisizokuwa na suhula zozote za kujiokoa kwa shabaha ya kuingia pwani ya kusini mwa Italia kinyume cha sheria, na matokeo yake hukumbwa na majanga ya kuzama kwa meli hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni