SIKU chache baada ya serikali kusitisha Opereshini Tokomeza Ujangili kutokana na wabunge kuilalamikia wakidai inakiuka haki za binadamu na mifugo mingi imeuawa, siri imefichuka kwamba baadhi ya wabunge na vingozi wa serikali wanatumiwa na majangili kudhoofisha vita dhidi ya ujangili.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu kutoka bungeni na serikalini, majangili hao wamegawanyika katika makundi sita. Wamo wafugaji, wakulima, watalii, wamiliki wa vitalu vya uwindaji, wabunge, na viongozi wa serikali ambao wameibuka na kuingilia kati baada ya kuhisi kwamba wanakaribia kukamatwa.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa zaidi ya sh milioni 200 zimechangwa na majangili hao kwa ajili ya kufanikisha mkakati wa kuzima opereshini hiyo.
Baadhi ya wabunge wanatumiwa bila kujua, huku wengine wakifanya hivyo kwa hiari na makusudi ya kunusuru majangili.
Tayari kuna mpasuko mkubwa serikalini na ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na baadhi ya watendaji kubaini mbinu chafu za kutaka kuzima operesheni hiyo ili kuwanufaisha vinara wa ujangili.
“Hawa watu wana mtandao mkubwa, baada ya kubaini wanakaribia kunaswa, sasa wameingia bungeni kwa kuwatumia baadhi ya wabunge ili waipinge operesheni hiyo,” kilisema chanzo.
Taarifa za uhakika kutoka serikalini zinasema kuwa majangili hao wamekuwa na jeuri kutokana na kuwazunguka viongozi wa chini na kuwasiliana moja kwa moja na kigogo, ambaye bila kujua amekuwa akizunguka viongozi wa wizara, na kukingia kifua majangili.
Baadhi ya vyanzo hivyo vilieleza kushangazwa na hatua ya baadhi ya wabunge kutetea uhai wa ng’ombe na kushindwa kulinda uhai wa tembo wanaouawa na kung’olewa pembe.
Mwishoni mwa wiki, Bunge liliazimia kuunda kamati teule ili kuchunguza suala hilo huku Waziri Mkuu na mawaziri wanne wakisulubiwa kwa madai kuwa wameshindwa kuwajibika ipasavyo.
Mbali na Pinda, wamo pia Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), David Mathayo David (Mifugo na Uvuvi) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa).
Hata hivyo, gazeti hili limedokezwa kuwa kwa vyovyote iwavyo serikali haitakuwa tayari kukubali kamati teule hiyo iundwe kwani ripoti yake inaweza kumng’oa Pinda na hivyo serikali kuanguka.
“Kinachofanyika sasa ni kuletwa kwa taarifa ya dharura bungeni ya kuonyesha serikali inapendekeza njia mbadala ya kushughulikia suala hilo ili badala ya kamati teule, iundwe tume huru itakayoongozwa na jaji kama ambayo CHADEMA wamekuwa wakipendekeza muda mrefu.
“Vita hii ya ujangili ni pana, imeingia hadi kwenye siasa za makundi ya urais ndani ya CCM, na hivyo kundi moja linataka kumng’oa Makinda kwenye uspika kwa hofu kuwa anawasikiliza sana wabunge na mawaziri wa kundi jingine,” kilisema chanzo hicho.
Kwamba Oparesheni Tokomeza Ujangili inapingwa baada ya vinara hao kubaini wanakaribia kunaswa, na sasa wanataka kuvuruga ili kazi hiyo irudi nyuma na hata ikiendelea basi wako radhi kutajana kwa majina kwani miongoni mwao wamo pia wabunge na viongozi wengine.
“Hawa majangili wana jeuri, wao wanazungumza kwa simu moja kwa moja na mmoja wa vigogo wa ngazi za juu serikalini, na huko wanasikilizwa. Serikali nayo inajua kuwa operesheni ikisimama tembo wanakwisha na vile vile kamati teule wakiikubali serikali inaanguka,” kinasisitiza chanzo.
Vyanzo hivyo vinaainisha kuwa hata mchakato wa kutaka kumwondoa Makinda kwenye uspika ambao ulikuwa umeanza kupitia kwa Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla kukusanya kura za wabunge uliingiliwa na majangili hao.
Vyanzo vya habari vinasema hoja ya Kigwangalla inasukumwa na wakubwa kadhaa mashabiki wa mmoja wa mawaziri waandamizi wanaotajwa kutaka kugombea urais 2015, ambao wanaona Makinda anapendelea wabunge wanaoshabikia kambi ya kigogo mwingine anayesemekana kutaka urais kwa udi na uvumba.
Habari zinasema kundi la waziri huyo linaungwa mkono na kigogo mmoja mwandamizi ambaye hataki kabisa kuruhusu swahiba wake wa zamani agombee urais; na sasa wamedhamiria kumwangusha Makinda.
Hata hivyo, kabla hoja yao haijashika kasi, wakati wakiendelea kukusanya sahihi za kutosha kumwondoa Makinda, majangili nao wakapata upenyo kwa kuathiri mwelekeo wa Bunge, na Makinda anaruhusu mjadala wa ujangili, ambao iwapo kamati teule itaundwa na kufanya kazi yake barabara, serikali inaweza kuangushwa kabla ya spika huyo kuondolewa.
“Hoja ya Makinda imezimwa, sasa wabunge wanazungumzia operesheni ya ujangili. Hapa wanajua kuwa spika hawezi kukubali hoja hiyo iendelee, hivyo naye ataipa kipaumbele kamati teule ili kuonyesha serikalini kuna tatizo.
“Wanajua hawawezi kumfukuza spika katika kikao hiki, lakini wakati huo Kamati ya Bunge itakuwa imekamilisha mchakato na kutoa uamuzi dhidi ya Pinda na mawaziri wenzake, jambo ambalo linaweza kumnusuru Makinda na kuiangusha serikali,” kilisema chanzo chetu.
Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM), ndiye alitaka Bunge lijadili kuhusu migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, huku Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), akitaka Bunge lijadili vitendo vinavyofanywa na watendaji katika Operesheni Tokomeza Ujangili.
Lugola alidai watendaji wamekuwa wakiwaua kwa risasi ng’ombe waliowakamata kwenye operesheni hiyo pamoja na kuwatesa wamiliki wasiotoa fedha zinazohitajika.
Kutokana na hoja hizo, Makinda alitoa fursa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mathayo, kuelezea Operesheni Tokomeza Ujangili na migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Kagasheki ndiye aliyekuwa wa kwanza kueleza operesheni hiyo inaendelea. Alisema inalenga kutokomeza ujangili ulioshamiri hapa nchini kiasi cha kutishia sekta ya utalii na tembo.
Hata hivyo, Kagasheki alisema kutokana na malalamiko ya watu mbalimbali juu ya mwenendo wa operesheni hiyo, serikali imeamua kuisitisha ili kufanya tathmini.
Waziri huyo pia alisema mifugo yote iliyokamatwa ndani ya hifadhi kabla na baada ya operesheni hiyo iachiliwe bila gharama yoyote na watu wenye ushahidi wa ng’ombe wao waliouawa kwa risasi wawasilishe vielelezo ili achukue hatua zaidi.
Waziri Mathayo alitoa taarifa kuhusu migogoro kati ya wafugaji na wakulima. Aliwaomba radhi waliopata hasara ya kujeruhiwa, kupoteza mifugo au vifo katika operesheni hiyo.
CHANZO- TANZANIA DAIMA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni