Ismail Aden Rage. |
MWENYEKITI aliyesimamishwa Simba, Ismail Aden Rage, ameanza kupata wakati mgumu baada ya kutishiwa kuuawa endapo ataendelea kung’ang’ania madarakani.
Rage amethibitisha kuhusiana na hilo jana wakati akizungumza kwa mara ya kwanza tangu kamati ya utendaji ya klabu hiyo, kutangaza kumsimamisha katika nafasi hiyo, katika kikao chao kilichofanyika mapema wiki iliyopita jijini Dar ambapo tukio la kushangaza ni kitendo cha mwenyekiti huyo kukataa maswali yoyote kutoka kwa waandishi.
Rage amesema kufuatia vuguvugu linaloendelea sasa baina yake na kamati ya utendaji, amepokea simu inayomtaka kuachana na nafasi hiyo, ambapo endapo ataendelea kung’ang’ania atapoteza uhai wake mara moja.
“Nimeshangazwa sana, sasa hivi endapo kama unaweza kufanya vitu vya namna hiyo, ni wazi utashikwa kirahisi, tayari mtu huyo tumeshapata jina lake, nimewasiliana na jeshi la polisi ili kuweza kumsaka na kumtia hatiani,” alisema Rage.
Aidha, katika mkutano wake huo wa jana, Rage ameonyesha kupingana na maamuzi ya Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kufuatia rais Jamal Malinzi kumpa siku 14 za kuitisha mkutano mkuu wa dharura.
“Nimeshangazwa na kusikitishwa sana na ujumbe huu ambao TFF imenitumia, nilitegemea kwanza wangeanza kwa kukemea juu ya hili la kufanyiwa mapinduzi, lakini badala yake wamenitaka kuitisha mkutano mkuu wa dharura, kitendo ambacho ni kuniingilia majukumu yangu.
“Katiba ya Simba inasema wazi katika ibara yake ya 22 kwamba mwenyekiti na kamati ya utendaji wanaweza kuitisha mkutano mkuu wa dharura endapo wataona haja ya kufanya hivyo. Mimi sioni haja ya kufanya hivyo kwa sasa, nasema sitaitisha mkutano na kama watanilazimisha nitajiuzulu.”
Kuhusiana na hilo, Malinzi alisema watasubiri barua kutoka kwa Rage kuhusiana na kulipinga hilo halafu watalifanyia kazi.
“Suala lile halikuamliwa na Malinzi, ni Kamati ya Utendaji ya TFF. Hivyo tutasubiri barua kutoka kwa Rage halafu tutakaa tena na kulifanyia kazi,” alisema Malinzi.
Wakati Rage akitangaza hayo, amefanya uteuzi mwingine wa viongozi katika uongozi wake, ambapo amemteua Rahma Al Kharusi maarufu kama Malkia wa Nyuki kuwa Mjumbe wa Bodi ya Udhamini ya Simba na Michael Wambura akichukua nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji iliyoachwa na Malkia.
“Nilipokea maombi ya Malkia wa Nyuki, akiniomba nimuondoe katika nafasi ya awali ya kamati ya utendaji, kutokana na kuzidiwa na majukumu yake ya kikazi, lakini bado tunamhitaji,” alisema Rage.
Kuhusiana na Rage kukataa kuitisha mkutano mkuu wa dharura, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Zakharia Hans Pope, alisema watakaa katika kikao na kulijadili hilo, kisha kutoa tamko la pamoja.
Akizungumza kutoka Dubai, Hans Pope, alisema ndani ya kikao hicho, pia ataeleza hatima yake ya kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni