Chama Cha Wananchi CUF kimesema kitaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuwaunganisha wananchi ili kuhakikisha kuwa Wazanzibari wanakuwa kitu kimoja.
Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad amesema iwapo wazanzibari wataondosha tofauti zao na kusimamia maslahi ya nchi, maendeleo makubwa yanaweza kupatikana ikiwa ni pamoja na kuwakomboa vijana kutokana na ukosefu wa ajira.
Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameeleza hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Fumba Wilaya ya Magharibi Unguja, ikiwa ni kuhitimisha ziara yake ya kichama kwa majimbo tisa ya Wilaya hiyo.
Amesema kutafuta suluhisho la ukosefu wa ajira kwa vijana ni kipaumbele chake nambari mbili katika uongozi wake wa kisiasa, baada ya kuwaunganisha wananchi kuishi kwa umoja na mashirikiano.
Amefahamisha kuwa zipo njia nyingia za kuwakomboa vijana kutokana na tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo ili waweze kuajiriwa katika viwanda vidogo vidogo na vya kati kupitia kwa wawekezaji wa sekta ya viwanda, pamoja na kuwaelekeza kujishughulisha na uvuvi wa bahari kuu.
Eneo jengine alilolitaja kuweza kuwasaidia vijana kuondokana na ukosefu wa ajira ni sekta ya kilimo ambayo itawasaidia wananchi wengi kwa wakati mmoja kuondokana na tatizo hilo.
Amefafanua kuwa kitu cha msingi ni kuwajengea uwezo katika maeneo hayo ili kuweza kukidhi ushindani wa soko la ajira, sambamba na kuwawezesha kuwekeza katika kilimo cha kisasa ambacho kitakuwa na tija zaidi kwa wakulima.
Akizungumzia kuhusu uhai wa Chama hicho Maalim Seif amesema hali ya chama katika Wilaya hiyo inaridhisha hasa kutokana na kuendelea vyema kwa chaguzi za chama katika ngazi za matawi.
Amewataka wanachama kuwachagua viongozi wazuri watakaoweza kusimamia maslahi ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Katika hatua nyengine Maalim Seif amekemea tabia ya baadhi ya viongozi kuendeleza chuki na uhasama miongoni mwa wananchi, jambo ambalo amesema halitoisadia nchi kutimiza malengo yake ya amani na maendeleo.
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu (CUF) akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa Chama hicho katika viwanja vya Fumba, Wilaya ya Magharibi Unguja.Picha zote na Salmin Said, OMKR.
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Haki za Binadamu (CUF) Salim Bimani, akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa Chama hicho katika viwanja vya Fumba, Wilaya ya Magharibi Unguja
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Haki za Binadamu wa CUF Salim Bimani, amesema wanakusanya ushahidi wa watu wanaonyimwa haki ya kupatiwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZAN ID), ili waupeleke kwa Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein.
Amesema lengo la kukusanya ushahidi huo ni kuthibitisha madai yao kwa Mhe. Rais kuwa bado baadhi ya wananchi wananyimwa vitambulisho hivyo kinyume na sheria, ili hatimaye waweze kupatiwa vitambulisho hivyo na kuandikishwa kuwa wapiga kura.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu (CUF) uzalendo wa kweli unahitajika katika kuondoa kero za kimaisha zinazowakabili vijana na taifa kwa ujumla.
“Huwezi kuwa mwana wa nchi ikiwa huna uchungu na nchi yako”, alisema Jussa akikariri maneno ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Katika mkutano huo CUF kilivuna wanachama wapya 144, sambamba na kukabidhiwa kadi 19 kutoka kwa wanachama wa NCCR Mageuzi na kadi 7 kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni