Utaifa Au Uislam?
Muhammad Baawazir Mafundisho na ujumbe aliokuja nao Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni mafundisho ya mwisho na yaliyokamilika, kwani Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Mtumwisho kama anavyoamini kila Muislamu kwa mujibu wa Qur-aan na Hadiyth.
Pamoja na kuwa Mitume wote waliotangulia walikuja na ujumbe wa kiislamu, yaani tawhid, kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kuwakataza watu na kuabudu asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), isipokuwa ujumbe wa Mitume hiyo iikuja kwa watu maalum na zama maalum.
Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametumwa kwa watu wote wa zama zote akiwa na mafundisho yaliyokamilika yasiyohitaji nyongeza wala kurekebishwa.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika Qur-aan Tukufu 5:3: {{… leo nimekukamilishieni dini yenu na kutimiza neema zangu…}} tafsiri.
Kwa mujibu wa Aayah hii ambayo ni miongoni mwa Aayah za mwisho kabisa kushuka, Uislamu umekamilika na ndio neema kuu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na Allaah Ameridhia uislamu kuwa ndio njia yetu ya maisha.
Aidha mfumo huu uliokamilika ambao ndio neema kubwa kuliko zote kwa Muislamu umeletwa ili uwe juu na ushinde mifumo yote mingine.
Allaah Anasema:
{{Yeye Ndiye Aliyemtuma mjumbe wake kwa uongofu na dini ya haki ili iweze kushinda mifumo (dini) zote nyingine hata kama makafiri watachukia}} Aayah nyingine {hata kama mushrikina watachukia} 61:9 tafsiri.
Uislamu umekuja kwa ajili ya watu wote wa rangi zote na mataifa yote, wa lugha zote na wa zama zote. Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kumwambia Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Qur-aan 34:28 {{kwa hakika Tumekutuma wewe kwa watu wote…}} tafsiri.
Moja miongoni mwa maradhi makubwa ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyakuta na akayapiga vita kwa nguvu zake zote ni maradhi ya UKABILA, UTAIFA na UZAWA miongoni mwa Waarabu. Na Aayah nyingi ziliteremka kutibu maradhi hayo na kuwapa Waislamu mtazamo sahihi juu ya suala hilo.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika Qur-aan 49:13 {{Enyi watu, hakika Tumewaumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke na Tumewajalieni Mataifa na Makabila ili mpate kujuana, hakika mbora wenu mbele ya Allaah ni yule mchaji Mungu zaidi}} tafsiri
Haya yalikuwa ni mapinduzi makubwa sana ya kimtazamo, na huo ni msingi mkubwa wa mahusiano na haki za binadamu ambao umedumu kwa karne 14 na utaendelea kudumu hadi siku ya mwisho.
Undugu Wa Kiimani
Moja miongoni mwa misingi mikuu ya imani ya Kiislamu ni kuamini kuwa WAISLAM WOTE NI NDUGU, na undugu huu wa imani una uzito mkubwa kuliko undugu wa damu, pale ambapo imani za ndugu wa damu zitakapotofautiana.
Aidha undugu huu wa kiimani ni mkubwa zaidi kuliko koo, kabila, taifa, rangi, lugha, n.k. pale ambapo imani zitakuwa tofauti. Hii inamaanisha kuwa waislamu wote ulimwenguni ni ndugu kwa mujibu wa imani yao, bila kujali misingi ya kilugha, jiografia, rangi, utaifa wa mipaka ya kikoloni ambao walikuwa ni maadui namba moja wa dini hii kama historia inavyoonyesha.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika Qur-aan 49:10 {{Hakika Waumini ni ndugu…}} tafsiri.
Pamoja na kuwa suala la kuondoa kasumba ya ukabila lilikuwa ni gumu sana, lakini kutokana na Tawhiyd na imani iliyokita nyoyoni mwa Waumini, wao waliweza kulivuka tatizo hilo, Kwao Uislamu ukawa ndio msingi mkuu wa undugu na mapenzi na waliwaona wasio kuwa Waislamu hata kama walikuwa na nasaba (ujamaa) nao, kuwa ni watu wasiofaa kuwakumbatia, na kuwafanya marafiki wa karibu. Mifano mingi ipo katika Siyrah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake watukufu kuhusu hilo. (Musw’ab bin ‘Umayr na kaka yake, ‘Umar bin Al-Khattwaab na mtoto wake, na wengine wengi) kwa namna walivyoelewa mafunzo ya Uislam juu ya undugu wa imani na umoja wa dhati.
Dola ya Kiislamu iliendelea kuwa na nguvu na mshikamano katika kipindi chote ambacho undugu wa kiimani ulidumishwa kuliko mahusiano mengine, na udhoofu ulianza kudhihiri pale ambapo ‘aswabiyyah (kasumba) na‘unsuriyah (ubaguzi), ulipoanza kudhihiri upya.
Moja ya sababu iliyosababisha kuangushwa kwa dola ya Kiislam huko Uhispania, basi ni ‘aswabiyah (uzalendo) naqabaliyah (ukabila). Mwaka 1924 Uislamu ulishuhudia kuangushwa kwa utawala wa Kiislamu Istanbul, kwa msaada wa baadhi ya majimbo ya waarabu yaliokuwa yanapinga kiongozi kuwa Mturuki. Na wakasahau wasia wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliotuusia kuhusu kiongozi, kuwa tumtii kiongozi wa aina yoyote na kabila lolote na rangi yoyote hata kama akiwa ni mtumwa wa kihabashi! Na maafa kama haya yanatutokea sisi kwa sababu kuu ambayo ni kuasi mafundisho ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Sumu hiyo mbaya kabisa ya ukabila, utaifa, ubaguzi ilizidi kuenezwa kwa kasi kubwa na maadui wa Kiislamu baada tu ya utawala kuangushwa, kuhakikisha kuwa Waislamu hawarudi kuwa kitu kimoja kama ilivyokuwa awali.
Na hapo ndio mwanzo wa kudhihiri kwa serikali za kisekula (kilimwengu zisizotaka dini) zenye mielekeo ya kitaifa na uzalendo katika mashariki ya kati mpya iliyokuwa hapo mwanzo ikijulikana kama (Otoman Empire). Mfano mzuri ni yale yaliyojitokeza katika uliokuwa mji mkuu wa dola ya Kiislamu, Istanbul – Uturuki. Kwa kuzuiwa kudhihirishwa athari zote za Kiislamu, kuanzia lugha, kwa kubadilishwa herufi za kiarabu kwenda kwenye kilatini, kuzuia kuvaa mavazi yenye athari za kidini, sherehe za kidini, kuadhini kwa kutumia lugha ya Kiarabu na badala yake iadhiniwe kwa Kituruki, na mambo mengi mengine yaliyokuwa yakiwaunganisha Waturuki na ndugu zao wa Kiislamu ulimwenguni kote!
Fitna ya utaifa, uzalendo, ukabila, ulugha, ni miongoni mwa fitna kubwa zilizoufikisha ummah wetu hapa tulipo leo. Na hii ni bid’ah kubwa inayopasa kupigwa vita na kila Muislamu mwenye wivu na dini yake.
Katika zama tuliyonayo, Muhammad kutoka Misri, atakuwa karibu zaidi na atampenda zaidi, na atamfanya msiri na mshauri wake kuwa ni George (mkiristo) kutoka Jordan (kwa sababu ya uarabu) kuliko Muhammad (ambaye ni Muislam) kutoka Pakistan (kwa sababu si mwarabu)! Vilevile Makame atamthamini zaidi Vuai kutoka Zanzibar hata kama hajaisimamisha misingi ya dini vizuri, kuliko atakavyomthamini Kitwana ambaye anachunga mipaka ya Mola wake zaidi, kwa sababu tu ni Mbara!!
Na hivyo hivyo Kindamba (Muislam) atamthamini Mkapa (Mkiristo) zaidi kwa sababu ni M’bara mwenzake kuliko atakavyomjali ‘Umar kwa sababu ni Mzenji pamoja na kwamba ni Muislam!! Na hali kadhalika Katika siasa za kijahiliya vile vile mambo ni kama hayo kubaguana kwa misingi ya kisiasa Utakuta watu wana mapezi na ukaribu na kina John eti kwa sababu chama chao ni kimoja na kuwachuchukia kina ‘Abdullah kwa sababu si wafuasi wa chama chao.
Mapenzi yetu yamekuwa si kwa ajili ya Allaah, bali kwa ajili ya dunia, chuki zetu si kwa ajili ya Allaah, bali kwa ajili ya dunia, mitazamo imebadilika, na vipimo vimebadilika. Iko haja kubwa ya kurejea upya kupandikiza mitazamo sahihi ya Kiislamu na kuimarisha Tawhiyd katika nyoyo za Waumini.
Katika Sunan Abi Daawuud, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
(Si katika sisi atakayelingania katika ‘asabiyah (kasumba za ukabila, utaifa, rangi n.k), na si katika sisi atakayepigana katika ‘aswabiyah, na si katika sisi atakaekufa katika ‘aswabiyah).
Na anasema katika Hadiyth nyingine sahihi kuwa:
(…na yeyote atakayelingania kwa mwito wa kijahili basi huyo ni mzoga wa jahanamu, akaulizwa: Ewe Mjumbe wa Allaah, hata kama anaswali na anafunga? Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Hata kama akiswali na akifunga na akidai kuwa yeye ni Muislamu. Jiiteni kwa mlinganio wa Allaah aliyekuiteni Waislamu waumini waja wa Allaah’.)
Anasema Shaykhul Islaam Ibn Taymiyah: (Chochote kilichotoka katika ulinganio wa Kiislamu na Qur-aan kwa nasaba au nchi au asili au mad’hab au njia, basi hilo ni katika mambo ya kijahiliya, kwani walipokhitalifiana Muhajiruun na Answaar akasema Muhajir: Enyi Muhajirina, na akasema Muansaar, enyi Maanswari, akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘‘ Mnaitana kijaahliya hali ya kuwa mimi nipo pamoja nanyi’’?!) Na akachukizwa sana.
Na haya tunayaona leo, Waislam wanachukiana na kugawana kiutaifa na kisiasa. Katika upande wetu haswa wa Tanzania na Afrika ya Mashariki! Utakuta Waislam wamegawanywa na siasa na vyama vya kitwaghuut hadi imefikia Waislam wanahasimiana na kuchukiana kwa sababu hawa ni wafuasi wa chama hiki na wale ni wa chama kile, hawa wanawadharau hawa na wale wanawadhalilisha wale!
Mfano mzuri ni leo hii tunaona kuna Uzanzibari na Ubara au ‘Uzanzibara’ na haikuishia hapo hata hao wa sehemu moja tu ya visiwani, wamegawanyika! Kuna Uunguja na Upemba, Uswahili, Ungazija na Uarabu, Umjini na Ushamba! Imefikia hata hiyo dini inakwenda kikabila!! Yaani mwelekeo wa dini unafuatwa na watu wenye asili fulani, na unakwenda vizazi hadi vizazi, bila huyo mwenye kuufuata kutojua anachokifuata kama kina ushahidi kisheria au la!
Hali hii inasikitisha mno kwa Waislam! Nako ndugu zetu wa Somalia hali kadhalika, wale waliozaliwa huko wanawadharau waliotoka Tanzania au Kenya, na hawa nao wanawaponda wale vilevile na haijaishia hapo tu, bali kabila hili likawa bora kuliko lile… Hadi kukaishia kwenye vita visivyojulikana mwisho wake na hali wote wanakiamini kitabu (Qur-aan) kimoja na wanaelekea Qiblah kimoja na hata kiitikadi ni wamoja.
Mwenyeezi Mungu Anatuonya katika Qur-aan 49:11, Anasema:
{{Enyi mlioamini! Watu (taifa, kundi, kabila) wasiwadharau wenzao; huenda wakawa bora kuliko wao. Wala wanawake wasiwatusi wanawake wenzao; huenda wakawa bora kuliko wao. Wala msitukanane kwa UKABILA, wala msiitane MAJINA MABAYA (ya kudharauliana): jina baya kabisa kuambiwa mtu ni ‘asi baada ya kuwa ni Muislam. Na wasiotubu, basi hao ndio madhalimu.}}
Huu ni msiba mkubwa, na unazidi msiba huu kila tutakapochukuliwa na malengo mengine yasiyokuwa ya ‘La ilaaha illa Allaah, Muhammadun Rasuulu Allaah’! Tumejitenga na ‘mambo mawili’ (QUR-AAN NA SUNNAH) ambavyo Mtume alituachia na kutusisitiza navyo, sasa matokeo yake ndio huku tunapoishia.
Jamii yetu ya Kiislamu hivi leo, inalichukuliya suala hilo la Ubaguzi, Utaifa, Ukabila, Uzawa na Rangi, kuwa ni muhimu sana, na hasa wale ambao wapo ugenini! Wamekuwa wanashikana na kushirikiana kwa misingi ya maeneo walikotoka, Utaifa n.k. Hadi imefikia shughuli mbalimbali kuendeshwa kwa misingi hiyo pamoja na shughuli hata za dini ambazo hazipaswi kuwa na ubaguzi ndani yake!!
Na pia kumeanzishwa kumbi (groups) nyingi katika mtandao (Internet) ambazo zimeanzishwa na Waislam lakini si kwa misingi ya dini bali Utaifa! Na baadhi yake wanachama ni wale tu waliotoka katika eneo hilo hata kama si Muislam, na hakubaliwi mtu kuwa mwanachama kama katoka eneo/taifa jingine hata kama ni Muislam.
Pamoja na kuwa si kosa watu wa sehemu moja kushirikiana na kuwa pamoja muda wa kudumu wote ni Waislamu, lakini si tabia ya kuiendekeza na kuishabikia, kwani inaweza kujenga hisia mbaya na mgawanyiko kwa ndugu wengine wa Kiislam ambao wanatoka sehemu zingine. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza watu wawili wasinong’one pakiwa na mwenzao wa tatu! Hii yote ni kufunga milango ya dhana ambayo inaweza kuleta mianya na mgawanyiko katika undugu wa Kiislamu ambao ndio msingi mkuu.
Ni muhimu wale viongozi wa dini au wenye kuyasimamia mambo ya dini wasishiriki katika kuimarisha hali hiyo ya Utaifa, Ukabila, na Urangi! Ni jambo la kusikitisha sana kuona baadhi ya wasomi wa dini wamelinyamazia jambo hilo na hali wanaliona mbele ya macho yao na kusikia likizungumziwa na zaidi ni kuwa kuna hata kati yao wenye kushiriki katika kuihamasisha na kuikuza hali hiyo.
Kwa hivyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu, kuyapiga vita kwa nguvu zote kila ambapo tutaona mambo haya yanajitokeza. Na khasa kwa wale viongozi na wasomi wa kidini wahakikishe mambo haya hayapewi nafasi kwani ni adui wa dini yetu na dunia yetu, na sio wao kuwa wa mbele kuyashabikia au kuyanyamazia.
Tumuogope Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na tumtii Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala tusitangulize letu dhidi yao kama Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alivyotuonya tumweke yeye mbele kuliko hata nafsi zetu wenyewe, achilia mbali kabila, taifa, rafiki au chama.
Kwa hiyo ndugu zangu katika imani kila mmoja wetu ajitathmini katika maisha yake ya kila siku anayoishi, je, hana maradhi haya ya Ukabila, Uzawa, Urangi na Utaifa?
Na kama anayo, nini afanye? Jibu ni kwamba hakuna jingine isipokuwa ni kuyaacha mara moja ikiwa anamtaraji Allaah na siku ya mwisho.
Na pia tujiulize vipi tutaraji nusra ya Allaah wakati sisi wenyewe hatustahiki kupata nusra kwa kuwa na mambo kama haya?
Tuangalie waliopita kabla yetu ambao walipata nusra kutoka kwa Allaah, je, walikuwa na sifa kama hizi tulizonazo sisi hivi sasa?
Kwa hiyo ndugu zangu kwa kuendelea kushikamana na uvundo huu na maradhi haya ya u-’assabiyah wa Utaifa, Ukabila na Uzawa, hatutofika popote. Na ni vizuri tuangalie kwa muda wote huo ambao tulioshikamana na uvundo huu hadi leo hii, ni kipi tulichovuna na kuambulia zaidi ya fitna, majungu, chuki na kuhusudiana.
Kwa kumalizia niwakumbushe Allaah Anachotuambia katika Kitabu Chake Kitukufu- Qur-aan- 47:7 {{ Ikiwa mtamnusuru Allaah Naye Atakunusuruni na Atazithibitisha nyayo zenu.}} (Na kumnusuru Mwenyeezi Mungu ni kuinusuru dini yake na si vingine bali kufuata maamrisho yake na kuacha makatazo yake.)
Wa Allaahu A’alam
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni