Edson Kamukara
SIAMINI kama wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wanatumwa na chama chao kufanya matendo haya ya aibu bungeni au ni uduni wa fikra ndio unaowasukuma kupitisha hata mambo ya hovyo hovyo ili mradi tu wameletwa na serikali yao.
Kwa wapenzi wa hadithi, bila shaka wanakumbuka ile ya sungura mjanja ya ‘sizitaki mbichi hizi’. Mnyama huyo mjanja alitamani kula ndizi lakini kwa habati mbaya mkungu ulikuwa juu sana kwenye mgomba.
Aliporuka na kuambulia patupu, akaamua kujifariji akidai: “Sizitaki mbichi hizi!” Hizi ni dalili za kutokubali kushindwa, maana tangu anazirukia alifahamu kuwa ni mbichi.
Laiti kama angezifikia bila shaka angezifakamia kwa hasira kutokana na nguvu nyingi alizotumia kuzihangaikia.
Wabunge wa CCM, wengi wao wana akili za sungura, wanafanya mambo ya ajabu na hatari kwa uhai wa chama chao huku wakifahamu fika baadaye mambo yanapoharibika wanageuka na kulamba matapishi yao kwa kukubali jambo lilelile walilokataa awali.
Wabunge hao, wakiongozwa na mawaziri wao, wameligeuza Bunge kama sehemu ya mzaha kwa kupitisha mambo bila kuyafanyia uchanganuzi wakidhani kwa kuitikia ndiyooo wanawakomoa wapinzani.
CCM wamefikia hatua ya kutotazama ubora wa hoja bali wanamtazama mtoa hoja, kama ni mbunge wa upinzani, hata hoja yake iwe nzuri kiasi gani hawawezi kuiunga mkono, isipokuwa ile ya kutoka kwa mbunge mwenzao itashabikiwa hata kama haina mashiko.
Wabunge hawa walishangaza umma pale walipopitisha muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2003, baada ya wapinzani kuususia wakiainisha kasoro zilizomo.
Yaani baada ya wapinzani wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kutoka nje, wabunge wote wa CCM waliopata nafasi ya kuchangia hoja hawakujikita kujadili mantiki ya muswada badala yake walikuwa wakitoa matusi na kejeli kwa wenzao waliotoka.
Hawa kwa fikra zao hawakuona kama Zanzibar haikushirikishwa, hawakuona umuhimu wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuongezwa zaidi ya 166 waliokuwa wanapendekezwa, hawakuona Tume ya Mabadiliko ya Katiba inavyonyongwa na kasoro ngingine chungu tele?
Nakumbuka wabunge hawa na mawaziri wao walivyokuwa wakitamba na kuwabeza wenzao bungeni baada ya kupitisha muswada wao huo wenye kasoro kibao, wakisema kuwa milango ya Ikulu imefungwa kwa wapinzani kuzungumza na Rais.
Kama haitoshi, wakasema eti wapinzani watamani kwenda Ikulu tena kwa Rais Jakaya Kikwete ili kunywa juisi na chai na ikafikia mahali mawaziri Wiliam Lukuvi, Mathias Chikawe na Stephen Wassira wakaanza kumlisha maneno mkuu huyo wa nchi.
Wassira ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), alisema Rais hana sababu za kutousaini muswada huo kuwa sheria bila mabadiliko yoyote, kwamba ulikidhi hatua zote na kuwa eti wapinzani wanafanya fujo tu hawana hoja.
Baadaye Waziri Chikawe naye aliibuka akisema kuwa atamshangaa Rais kama hatausaini muswada huo kuwa sheria, kwamba vinginevyo atakuwa ametangaza mgogoro na Bunge lililoupitisha.
Zilikuwepo na kauli nyingi za kuwabeza wapinzani kutoka ndani ya CCM kwa ujumla, meza ya Spika hasa naibu wake aliyelivuruga Bunge siku hiyo hadi kusababisha fujo lakini tambo hizo zilizimwa na kimbunga cha mkutano wa hadhara wa vyama hivyo vitatu katika uwanja wa Jangwani.
Siku hiyo, viongozi hao walitangaza kuanza ziara ya nchi nzima kufanya mikutano ya kuwahamasisha wananchi, ndipo Rais Kikwete akatambua hoja zao na kuamua kuwaomba wasitishe maandamano yao waje mezani wazungumze na serikali.
Lakini kama nilivyosema mapema kuwa wabunge wa CCM ni kama sungura aliyekosa ndizi, ndivyo walivyogeuka baada ya mwenyekiti wao kuwaaibisha na kukutana na wapinzani hao katika kikao alichowaalika pia viongozi wa chama chake.
La ajabu Wassira, Lukuvi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, waliodai wapinzani wanakwenda kunywa chai na juisi Ikulu, nao bila aibu walishiriki mazungumzo waliyoyakebehi kuwa milango yake imefungwa.
Baada ya hapo Rais aliusaini muswada kuwa sheria kisha yakafanyika marekebisho ya kuondoa kasoro zilizopingwa na wapinzani na kurejeshwa bungeni chini ya hati ya dharura.
Bila hata aibu, Chikawe huyohuyo alisimama bungeni kusoma upya marekebisho mapya yaliyomo kwenye muswada walioupitisha hovyo na wana-CCM wenzake huku wakijiapiza kuwa usingelirudishwa, safari hii akisema serikali ilikubali kuongeza mambo matano.
Mapendekezo hayo ni kuongeza idadi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka 166 hadi 201.
Pendekezo jingine ni kuweka kiwango cha chini na cha juu cha idadi ya watu wanaopendekezwa kwa ajili ya kuteuliwa na Rais.
Pia kutoa ruhusa kwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Katibu wa Baraza la Wawawakilishi kufanya maandalizi yote muhimu kwa ufanisi wa Bunge Maalumu.
Kisha nikamuona Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana, ambaye awali alilidanganya Bunge kuwa Zanzibar ilishirikishwa safari hii akiwa na kauli tofauti ya kuunga mkono mabadiliko ambayo aliyakataa mwanzo.
Nimesema awali kuwa shida ya wabunge wa CCM si hoja, bali mleta hoja. Kwani mapendekezo hayo ya serikali ndiyo yalikuwa madai ya wapinzani tangu mwanzo, kwa nini kiti cha Spika, serikali na wabunge wa CCM hawakuyakubali na mchakato ukaendelea?
Ni kweli hawana uelewa wa kuchambua miswada na kufanya maboresho hadi ifike kwa mwenyekiti wao kwanza ndipo afanye kazi hiyo na wapinzani au ni kutojitambua wako bungeni kufanya kazi kwa maslahi ya nani?
Tafakari!
Tafakari!
Chanzo: Tanzania Daima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni