Habari

Jumanne, 15 Oktoba 2013

UVCCM wamvaa Maalim Seif

15th October 2013
Chapa
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.
Umoja  wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Zanzibar, umedai kuwa viongozi watatu wa Chama cha Wananchi (CUF) wanahatarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja jana, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka aliwataja viongozi wengine kuwa ni wajumbe wa Baraza Kuu la CUF Ismail Jussa Ladhu na Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Aboubakari Khamis Bakari.

Alidai viongozi hao wamekuwa wakiwashambulia wenzao katika SUK na wakati mwingine kutoa siri za vikao vya serikali.

Shaka alisema lengo la mkutano wake na waandishi wa habari ni kutoa tamko la kukemea kitendo cha Umoja wa Vijana wa CUF kuwataka wanachama waanze kufanya mazoezi ya viungo kauli ambayo inaweza kuhatarisha uvunjifu wa amani na kuvuruga malengo ya kuanzishwa kwa SUK Zanzibar.

Alisema wazo la kuundwa kwa SUK lilitokana na CCM bila ya kulazimishwa na mtu yeyote, hivyo kama mambo yatakwenda kombo wananchi wanaweza kuamua kuvunja mfumo uliopo na kurudisha ule wa zamani.

Shaka alikilaumu kitendo cha Maalim Seif kusema atashirikiana na Rais Mstaafu Dk. Amani Karume kusaka mamlaka kamili ya Zanzibar katika  mfumo wa muungano badala ya Rais aliyemteua na kumuapisha kiapo cha kisheria Dk. Ali Mohamed Shein.

Alisema tokea kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa wananchi wameshuhudia kukithiri vitendo vya uvunjifu wa amani, ubaguzi na kusababisha hali ya wasiwasi kwa wananchi hasa vitendo vya uhalifu wa kutumia tindikali bila ya viongozi wa upinzani kuonekana kukemea.
 
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni