Habari

Jumatatu, 14 Oktoba 2013

Meli kubwa iliyotinga Dar yakoroga wamiliki

jumanne, 15 Oktoba 2013.
na Mwandishi wetu
MELI kubwa ya mizigo ya Maersk Line iliyotia nanga kwa saa chache katika Bandari ya Dar es Salaam, imezua kizaazaa baada ya wenye meli duniani kuitaka Tanzania kuboresha kina cha bandari zake ili kuweza kunufaika na biashara ya meli kubwa za aina hiyo.
Wamiliki wa meli duniani walipopata taarifa za kutia nanga kwa meli hiyo kubwa yenye urefu wa mita 249 ya kwanza kutia nanga katika bandari ya Dar es Salaam, walidhani kina cha bandari ya Dar es Salaam kimeongezwa lakini walipopata taarifa sahihi walitaka Tanzania kuboresha bandari zake.
Baada ya kuingia kwa meli hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande, walitangaza kwamba sasa Tanzania inaweza kupokea meli kubwa yenye uwezo mkubwa na kuwataka wamiliki wa meli kuanza kuleta meli zao.
“Kuingiza meli yenye urefu huu na yenye uwezo wa kubeba kontena 4,500 za futi 20 (teus) si jambo la msingi hasa ukizingatia meli zinazojengwa kwa teknolojia ya sasa hivi.
“Jambo la msingi ni je meli hii inaweza ikaingia na mzigo wote wa kontena 4,500 katika bandari ya Dar es Salaam kwanza kabla ya kwenda kwingine?
“Jibu ni hapana! Ni lazima kuwa na kina chenye mita 12.5 na kuendelea ili iweze kuingia,” anasema Emmanuel Mallya, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Meli Tanzania (Tasaa).
Mallya ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya EB Maritime Limited alisema biashara ya meli duniani ni nyeti inayohitaji umakini wa hali ya juu katika kuiendesha na si vyema kutoa kauli zinazoweza kuwavuruga wadau hasa kampuni za kimataifa ambazo zinafuatilia kila kinachoendelea katika bandari zote duniani.
“Biashara ya meli ni ya kimataifa na ni nyeti sana hivyo matamshi yanayohusu urekebishaji kwenye bandari mbalimbali lazima kuwe na umakini mkubwa.
“Kauli ya Waziri Mwakyembe na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Madeni Kipande, kuwa mawakala wa meli walete meli kubwa na TRA wafanye kazi kwa masaa 24 kuzihudumia inaweza ikapokelewa kwa hisia tofauti kutokana na uhalisia wa kina cha maji kwenye gati za TPA.
“Kwa sasa makampuni mengine makubwa kama Mediterranean Shipping Line, CMA CGM, EVERGREEN, COSCO, EMIRATES Shipping line, na mengine mengi yameanza kuulizia kama kina kwenye bandari ya Dar es Salaam kimeongezeka na kupokea meli kubwa zilizobeba kontena 4,500 na kushusha bila wasiwasi.
Jibu hapa ni kwamba kuna kikwazo cha kina ambacho ni mita 10.5 pamoja na kupwa kwa maji ambayo unaweza kuhimili mita 11.5 tu,” anasema Mallya.
Baharia mmoja mzoefu aliyejitambulisha kwa jina la Mzee Hassan alisema unaweza kuingiza meli yenye urefu wa mita 149 kwa teknolojia ya sasa kama iliyoingia wiki iliyopita na kuweza kuingia bila kuiwekea ‘tug’ ya kuisukuma.
Alisema meli hizo za kisasa huwa zinawekewa kitu kinachoitwa ‘Bothruster’ inayosaidia meli igeuke au ijiegeshe kwenye gati bila msaada wa tug kama malori au mabasi aina ya Scania ya kisasa yanavyoweza kupinda kona kwa haraka kwa kuwa usukani wake ni wa kisasa.
“Hii meli imekuja kama majaribio ya kuangalia namna ya kuingia bandarini Dar es Salaam kutokana na urefu wake.
“Wenye meli huangalia bandari za Dar es Salaam na Mombasa kama block moja. Kila kinachotokea upande mmoja huathiri upande wa pili. “Mombasa juzi walifungua gati namba 19 lenye kina cha mita 12.5 hivyo kuweza kupokea meli kama hii.
“Meli hii itapakia kontena 4500 za Mombasa na Dar es Salaam na kushusha kwanza Mombasa na baadaye Dar,” anasema Mzee Hassan.
Kwa upande wake Mallya ambaye ana uzoefu wa miaka mingi katika uendeshaji wa shughuli za meli, alisema kwa sasa changamoto kubwa kwa TPA na serikali ni kuongeza kina kwa kuwa matakwa ya soko ni kuwa na meli kubwa kulingana na ukuaji wa biashara.
Meli hiyo ilitia nanga kwa mbwembwe na kuondoka siku hiyohiyo jioni ikiwa imepakia kontena 77 badala ya uwezo wake wa kontena 4,500.
Maelezo ya wizara na uongozi wa TPA yalikuwa kwamba kuna propaganda kuwa bandari ya Dar es Salaam haina uwezo wa kupokea meli zenye ukubwa huo wenye kubeba makontena 4,500 kutia nanga.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni