Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema jana ameangukia pua baada ya Bunge kukataa mapendekezo ya Serikali ya kubadili baadhi ya vipengele vya Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, ya kuongeza adhabu kwa waandishi wa habari watakaopatikana na hatia ya makosa ya uchochezi.
Kukataliwa kwa mapendekezo hayo ni pigo kwa Serikali na Jaji Werema ambaye juzi wakati akijibu hoja za wabunge alijigamba kwamba yeye anasimamia amani ya nchi kwa hiyo vifungu hivyo haviwezi kuondolewa, kwani anafanya kazi kwa masilahi ya taifa na hategemei magazeti kwa ajili ya kuwa mbunge.
“Sitegemei magazeti kuwa mbunge nafanya kazi ya taifa. Walio wangu watanikataa na wasiokuwa wangu watanikataa. Nipo kwa ajili ya taifa sitamwangukia mtu yeyote miguuni,” alisema Werema, kauli ambayo iliwachefua wabunge.
Hata hivyo, jana baada ya Spika kuwahoji wabunge na kukataa mapendekezo ya Serikali, Jaji Werema alionekana kukereka hivyo alisimama na kutaka Spika aruhusu kura zihesabiwe katika kifungu hicho.
“Mheshimiwa Spika, nimesimama kuona hata wa upande wangu wamenisaliti, duh, basi naomba kura zihesabiwe kwa kuita majina mmoja, mmoja ili tujiridhishe,” alisema Werema.
Hata hivyo, Spika alikataa na kusema: “Kama kuna eneo ambalo tumefanyia utani Serikali ni katika eneo hili, naomba Serikali mtuletee muswada bungeni siyo porojo za maneno.”
Katika marekebisho hayo, Serikali ilikuwa ikipendekeza katika sheria hiyo mabadiliko ya kuongeza adhabu kwa waandishi wa habari watakaopatikana na hatia ya kuandika habari za uchochezi, kutoka faini ya Sh15,000 hadi kiasi kisichozidi Sh5 milioni.
Hata hivyo, wakati Bunge lilipoketi kama kamati wabunge walikataa kupitisha marekebisho hayo ambayo yalikuwa sehemu ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2013, wakisisitiza kwamba Serikali ipeleke bungeni muswada wa sheria ya habari.
Moto wa wabunge
Moto wa wabunge hao uliwashwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), ambaye alipendekeza sehemu ya nane ya muswada iliyokuwa na vipengele vya 39, 40 na 41 iondolewe ili kuishinikiza Serikali kupeleka bungeni sheria nzima inayohusu vyombo vya habari.
Mbunge huyo alisema kuwa sehemu hiyo na vipengele vyake kama vingepitishwa vingeifanya Serikali kuwa kimya na kushindwa kupeleka bungeni Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari kama ilivyoahidi kwa muda mrefu.
CHANZO- GAZETI LA MWANANCHI.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni