Shughuli ilianza kwa tafrija fupi ambayo ilitoa ukaribisho kwa wageni waalikwa kupata wasaa wa kujuana na kuzungumza mawili matatu, kabla mbunifu Doreen hajapanda jukwaani na kueleza dhamira yake ya kuwaleta pamoja wadau hao wa mitindo ndani na nje ya nchi.
Onyesho lilianza mapema saa moja na nusu jioni, ambapo watu walikuwa wakipata kinywaji na vitafunwa maalumu, vilivyotengenezwa katika mahadhi ya kiitaliano.
Tofauti na maonyesho mengine onyesho hili lilikuwa na steji ndogo kuliko ilivyozoeleka. Si hivyo tu hata mtindo uliotumika kuwakilisha kazi hizo za ubunifu ulikuwa ni wa kipekee wenye utofauti mkubwa.
Kulikuwa na wanamitindo watano ambapo kila mmoja alionyesha umahiri wake katika kulitawala jukwaa. Wote walikuja na mavazi ya kisasa wakiwa na mitindo rahisi ya nywele.
Wanamitindo waliingia na kutoka wakionyesha mavazi mbalimbali ya wanawake. Magauni marefu na mafupi pamoja na jumpsuit yalitawala onyesho hilo.
Kwa upande wa mitindo ya nywele warembo hao walipambwa kwa maweaving, rasta za kawaida pamoja na mawigi huku mapambo yao yakikamilishwa na ‘make’ up ya aina yake.
Wanamitindo waliokuwepo katika onyesho hilo ni Suzane Manoko, Joselyne Mrashi na Anna Gura wote kutoka Tanzania na Dianne Nyanzwa na Suzanne Anyango kutoka Kenya
Kila mmoja alionyesha umahiri wake katika kunadi vazi alilovaa, vilevile kuonyesha uhusiano ulioko kati ya urembo na mapambo yaliyotumika kunakshi mitindo yao.
Mbunifu Doreen Mashika alikuwa na kazi moja tu ya kuonyesha kipaji alichonacho katika ubunifu wa mitindo. Hivyo alipata wasaa wa kuwapamba wanamitindo wake kwa kutumia mapambo ya kiafrika yaliyotengenezwa kwa mikono.
Mashika hakusita kuelezea sababu hasa inayotofautisha kazi zake na watu wengine pale alipobainisha kuwa asilimia kubwa ya kazi zake hizo ni za mikono. Na ni za kitanzania halisi. Wakati anaingia jukwaani Mashika aliingia na mtaalamu wa vipodozi na urembo kutoka nchini Afrika Kusini, Swiss Reto Camichel aliyekuwa na kazi moja tu ya kuwabadilisha mitindo ya nywele wanamitindo waliokuwa jukwaani hapo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni