PAMOJA na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema kujiapiza kuwa kamwe asingekifuta kifungu cha mapendekezo ya serikali katika muswada wa marekebisho ya sheria ya magazeti ya mwaka 1976 sura 229, Bunge jana liligoma kupitisha kifungu hicho.
Badala yake, Bunge kwa kauli moja limeitaka serikali kuwasilisha bungeni muswada wa sheria ya magazeti.
Marekebisho hayo yaliyokataliwa, yalionekana ‘kuvitia kitanzi’ vyombo vya habari na waandishi wa habari wanaodaiwa kuchapisha habari zenye uchochezi au uvunjifu wa amani.
Adhabu kwa vyombo vya habari na waandishi watakaobainika kutenda makosa hayo, ilikuwa inapendekezwa kutozwa sh milioni tano au kifungo cha miaka mitano au vyote kwa pamoja.
Mapendekezo hayo yalipingwa vikali na msemaji mkuu wa kambi ya upinzani kwa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu na wabunge wengi, wakidai kuwa adhabu hiyo inalenga kuua tasnia ya habari.
Jana, wakati Bunge limekaa kama kamati kupitia vifungu mbalimbali vya muswada wa merekebisho ya sheria hiyo, mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), aliwasilisha mapendekezo ya kutaka kifungu hicho kifutwe akidai kuwa sheria hiyo inalenga kuwakandamiza waandishi wa habari.
Alisema hakuna sababu ya kuleta kipengele kimoja badala ya kuleta muswada mzima wa habari ambao ulikuwa ukidaiwa kuletwa bungeni kwa muda mrefu na serikali, lakini haijawai kufanya hivyo.
Mbunge huyo alianza kuwashambulia baadhi ya wabunge waliowakejeli wakidai kuwa wanaopinga sheria hiyo wachunguzwe pasi zao za kusafiria, akisema ni mawazo potofu kuona wanaopinga hawastahili.
Licha ya kutowataja kwa majina wabunge hao, lakini Serukamba alimlenga Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba, kwani ndiye aliyewashambulia wale waliokuwa wakipinga kipengele hicho.
Serukamba aliungwa mkono na Mbunge wa Paramiho, Jenister Muhagama (CCM) na Ester Bulaya wa Viti Maalumu (CCM), wakisema inasikitisha kuona serikali inakuja na mapendekezo ya kuweka adhabu kwa wanahabari wakati Bunge limekuwa likipiga kelele kwa ajili ya kutaka muswada wa sheria uletwe bungeni, lakini haijafanyika hivyo.
“Naishanga serikali kuna tatizo gani la kuwa na kigugumizi katika kuleta muswada wa sheria bungeni, wamepita mawaziri wangapi, lakini hatujawai kuletewa muswada wa sheria ya habari. Mimi sikubaliani na marekebisho ya sheria hiyo, bali nataka iondolewe ili muswada wa sheria ya habari uletwe hapa bungeni,” alisema Muhagama.
Baada ya hoja za wabunge hao, Spika Anne Makinda alihoji Bunge kama linakubaliana na mapendekezo hayo ya kufutwa kwa kifungu hicho, ambapo wote waliitikia ndiyo.
Msimamo huo ulionekana kumchanganya Jaji Werema, ambaye alijaribu kusimama kutaka kutoa ufafanuzi, lakini spika alimkatalia na kisha akapigilia msumari wa moto kwenye hoja za wabunge.
Spika alisema kuwa hata yeye anatamani kuuona muswada huo wa sheria ya habari ukiletwa bungeni ili iwe sheria kamili.
“Tumefanya utani katika sheria hii kwa muda mrefu, sitaki utani, serikali leteni muswada wa sheria ya habari. Mnajua nyinyi serikali hawa mmewaacha ndiyo maana wanakiuka,” alisema.
Spika alieleza kushangazwa na hatua ya serikali kupiga danadana katika kuleta muswada huo bungeni kwa kutoa sababu kila mara, akisema sasa wafanye haraka uletwe.
Mapema katika kupitia kifungu cha mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya filamu na michezo ya kuigiza ya mwaka 1976 sura 230 toleo la 2002 ibara ya 26, wabunge wametaka adhabu iliyopendekezwa na serikali ibaki pale pale ya sh milioni tatu badala ya tano.
Mapema mwishoni mwa wiki, Lissu katika maoni yake alisema sheria ya magazeti ilitungwa kwa mara ya kwanza na dola ya kikoloni mwaka 1928 na haikuwa na vifungu vya jinai za kashfa na uchochezi.
Aliongeza kuwa vifungu hivyo viliingizwa katika sheria za Tanzania mwaka 1953 na vililenga kuwadhibiti wakosoaji na wapinzani wa sera na dola ya kikoloni waliokuwa wameanza kujitokeza katika miaka hiyo.
Alibainisha kuwa muathirika wa kwanza wa vifungu hivi alikuwa Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere, wakati huo akiwa rais wa chama cha siasa cha upinzani, Tanganyika African National Union (TANU) na wenzake wawili.
CHANZO- TANZANIA DAIMA.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni