Habari

Ijumaa, 22 Novemba 2013

Wachina wanaswa na Kiganja cha Binadamu huko Mabibo jijini Dar es salaam.

Dar es Salaam 

Raia wawili wa China wanashikiliwa na polisi kwa kosa la kukutwa na mkono wa mmoja wa mfanyakazi wao kwenye kiwanda cha Urafiki Plastic Bags Ltd.
  
Raia hao, Yu Xiawey na Li Shilin walikamatwa jana kiwandani hapo eneo la Mabibo jijini Dar es Salaam baada ya polisi kupewa taarifa kuwa kuna mkono wa mtu umefukiwa katika eneo hilo.
Akizungumzia tukio hilo lililotokea saa 3 usiku, Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kinondoni, Camilius Wambura alisema Novemba 18 mwaka huu, mfanyakazi katika kiwanda hicho, Jumanne Rashidi alikatwa mkono wa kulia wakati akisafisha mashine ya kutengenezea mifuko ya plastiki.
Wambura alisema kuwa wakati Rashidi akiifanyia usafi mashine hiyo, ghafla Mchina anayedaiwa kuwaambia wafanye usafi, aliwasha mashine iliyomjeruhi vibaya na kutenganisha mkono na mwili.
“Tunawashikilia wamiliki wa kiwanda, tunafanya uchunguzi kujua kama ilikuwa ajali ya kawaida au kuna kitu kingine kimetokea. Pia tumemhoji mtu anayedaiwa kuufukia mkono huo, tutakapomaliza upelelezi tutawafikisha kwa wakili wa Serikali,” alisema.
Akizungumza na gazeti hili kiwandani hapo, Asha Abdallah mmoja wa wafanyakazi, alisema kuwa siku ya tukio Rashidi ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, aliombwa na bosi wake asafishe mashine, lakini alipoingiza mkono mashine iliwashwa na kumjeruhi.
Baada ya kujeruhiwa alipelekwa hospitali, lakini mkono wake ulihifadhiwa katika sehemu ambayo haikufahamika hadi ilipobainika jana kuwa ulikuwa umefukiwa nje ya kiwanda hicho.
Mkono umefukuliwa leo (jana) ulikuwa umefukiwa pale kwenye kifusi, ulikuwa umeanza kuharibika kabisa,” alisema Asha.
Aliongeza kuwa siku moja baada ya Rashidi kukatwa mkono, ndugu zake walifika kiwandani hapo kuonana na wamiliki wa kiwanda hicho ili wakabidhiwe mkono wakauzike, lakini kulitokea kutokuelewana baina yao, hivyo wakaamua kwenda polisi.
Bado tunajiuliza kwa nini waliamua kuufukia mkono badala ya kuwakabidhi ndugu zake, tukio hili linatupa hofu sana, lakini hatuna namna ya kufanya tunasubiri tuone mwisho wake,” aliongeza.

Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (Moi), Patrick Mvungi alisema hajapata taarifa za kuwapo kwa mgonjwa aliyekatwa mkono katika kiwanda cha Urafiki Plastic Bags Ltd, badala yake bosi huyo alimtaka mwandishi wa habari kwenda hospitalini hapo siku iliyofuata kwa kuwa alikuwa ameshatoka ofisini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni