Na Othman Ame USA.
Watanzania waishio na kuendesha maisha yao Nchini Marekani wameawa kuwa makini katika kuutumia vyema muda wao wa maisha Nchini humo kwa kufikiria mbinu za kujiwekea mitaji itakaowajengea hatma njema hapo baadaye endapo watafikia maamuzi ya kurejea kuishi nyumbani siku zijazo.
Watanzania waishio na kuendesha maisha yao Nchini Marekani wameawa kuwa makini katika kuutumia vyema muda wao wa maisha Nchini humo kwa kufikiria mbinu za kujiwekea mitaji itakaowajengea hatma njema hapo baadaye endapo watafikia maamuzi ya kurejea kuishi nyumbani siku zijazo.
Nasaha hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizungumza na Wanachama wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi katika Mji wa Seattle ndani ya Jimbo la Washington kwenye tafrija maalum iliyoandaliwa na wana jumuiya hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Ramada Tukwila Mjini Seattle.
Balozi Seif alisema wapo baadhi ya Watanzania waliobahatika kupata fursa na nafasi nzuri za kuendesha maisha katika Mataifa mbali mbali ya nje hasa ya ulaya lakini wengi kati yao wameishia kuwa na maisha mabovu kwa kukosa kujiwekea misingi mizuri.
Alisema tabia ya kuendelea na kuendekeza starehe sambamba na matumizi ya kifahari kwa msingi wa kutaka sifa hutoa sura mbaya kwao lakini kinachoumiza zaidi ni kile kizazi chao kinachowategemea.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba wana Jumuiya hiyo ya Watanzania wanaoshi Mjini Seattle kuzingatia na kuheshimu sheria na taratibu za nchi wanayoishi ili kulinda desturi na ukarimu walionao.
Amewapongeza wana jumuiya hiyo ya Watanzania wanaoishi Mjini Seattle kwa umoja na ushirikiano waliokuwa nao bila ya mgongano na ubaguzi wa uzawa ambao ndio utanaowasaidia katika kuimarisha mila na silka zao.
“ Ukweli sifa tulizokuwa nazo sisi Watanzania hatufanani na wenzetu wa mataifa mengine . Hivyo Utanzania wetu ni vyema tukauendeleza kwa kusaidiana na ofisi za balozi zetu zilizo karibu “. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Akijibu baadhi ya maswali alioulizwa na Wanajumuiya hiyo ya Watanzania waishio Mjini Seattle Balozi Seif aliwatoa hofu wanajumiya hao kwa kuwaeleza kwamba Zanzibar na Tanzania kwa ujumla hivi sasa inaendelea kuwa shwari licha ya vituko vinavyotokea katika baadhi ya wakati hasa vile vilivyokuwa vikiwatia hofu wananchi vya kumwagiwa watu tindikali.
Alieleza kwamba Serikali iko makini katika kuhakikisha vitendo vya uvunjaji wa amani havipewi nafasi na tayari vyombo vya ulinzi vinaendelea na operesheni za kuwasaka watu wenye tabia kama hizo zinayotishia maisha ya Jamii.
Akijibu swala la operesheni kimbunga iliyowakumba watu waliokuwa wakiishi kinyume na taratibu za uhamiaji Nchini Tanzania Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali iliamua kufanya operesheni hiyo baada ya kugundua wahamiaji haramu ndio wanaohusika na masuala ya ujambazi Nchini.
Alifahamisha kwamba watu wote walioondoshwa Nchini Tanzania kupitia operesheni Kimbunga hiyo wamebainika kutokuwa na kibali jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa mfumo na taratibu za uhamiaji Kimataifa.
Hata hivyo Balozi Seif alifafanua kwamba Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuheshimu haki za Binaadamu haijamkataza mtu wa nchi yoyote Duniani kuishi Tanzania endapo atazingatia sheria za Nchi zilizopo.
“ Serikali imelazimika kuwa makini katika kulinda usalama wa wananchi baada ya kugundua kwamba wengi wa wahamiaji haramu ndio waliokuwa wakihusika katika masuala ya ujambazi na matukio ya hatari hapa Nchini “. Alisema Balozi Seif.
Wakitoa salamu zao kwa wanajumiya hao Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mh. Nassor Ahmed Mazrui wamewashauri wanajumuiya hao kuzitumia fursa za mitaji zilizopo nchini humo kwa kuanzisha miradi Nchini Tanzania.
Mawaziri hao walisema mitaji hiyo ambayo fedha zake hazina masharti makubwa zinaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa ajira hasa kwa vijana pamoja na kuongeza vipato vyao vitakavyopunguza umaskini.
Walieleza kwamba wanajumiya hayo ni vyema wakaitumia Diasfora wakielewa kwamba Tanzania ni yao na kwame bila ya wao hakutakuwa na mgeni atakayeweza kuweka misingi ya kuimarisha uchumi wa taifa.
Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Mjini Seattle Jimboni Washington Nchini Marekani Nd. Yona Isimika alisema jumuiya yao iliyoanzishwa mwaka 2008 hivi sasa ina karibu wanachama Mia Nne.
Nd. Yona alisema Jumuiya yao iliyolenga kuuendeleza Utamaduni, Mila na Silka zao za Kitanzania iko katika mchakato wa kubadilisha katiba ili ikidhi matihaji yao hasa wakati wanapopatwa na matatizo.
Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Watanzania waoishi Seattle Washington alipongeza Ujumbe huo wa Zanzibar ulioongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa hatua yake ya kukutana nao ikiwa ni ugeni wa mwanzo tokea kuanzishwa kwa jumuiya hiyo mwaka 2008.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni