PEMBA. Hali ya Unyanyapaa imeezwa kuwa bado ni changamoto inayowakabili watu wanaoishi na virusi vya
Ukimwi kisiwani Pemba.
Wakitoa
michango yao baadhi ya washiriki wa mafunzo juu ya Haki za Binadamu, huko Chake
Chake Pemba wamesema licha ya elimu iliyotolewa bado unyanyapaa limekuwa ni
tatizo katika maeneo mengi ya kisiwa hicho.
Hata hivyo
wamesema inaonekana watu wengi wanaowanyanyapaa watu wanaoishi na virusi vya
ukimwi hufanya kwa utashi na hakutokani na ukosefu wa elimu au uelewa juu ya
masuala ya VVU na Ukimwi.
Kwa upande
mwengine baadhi ya washiriki hao wamesema ipo haja kuwepo kwa mikakati ya
kuchukuliwa hatua kwa wale wanaoondeleza unyanyapaa kwa watu wanaoishi virusi
vya Ukimwi.
Akitoa
ufafanuzi juu ya suala hilo Kaimu Mratibu wa Tume ya Ukimwi Pemba Ali Mbarouk
Omar, amekiri kuwepo kwa suala la unyanyapaa katika baadhi ya maeneo ambapo
amesema elimu ya msingi juu ya Ukimwi haijawaingia wananchi hao.
Amesema Tume
ya Ukimwi inaendelea na mikakati ya kutoa elimu ya unyanyapaa na ukimwi katika
maeneo mbali mbali ya jamii, ili dhana
kamili ya ukimwi ieleweke kwa jamii yote ili kuleta mafanikio katika kuondosha
maambukizi ya VVU na Ukimwi nchini.
Mafunzo hayo
yaliyoandaliwa na Kituo cha huduma za Sheria Zanzibar katika ofisi ya Pemba
yamewashirikisha watu wanaoishi na virusi
vya ukimwi, na wadau wengine walio katika mapambano na VVU,
yamefunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Mwanajuma Majid Abadalla.
D.C huyo
amekipongeza kituo hicho kwa juhudi zake za kuwaelimisha wananchi juu ya
masuala mbali mbali yakiwemo ya haki za binadamu,usaidizi wa sheria na katiba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni