Habari

Jumamosi, 14 Septemba 2013

Padri alitishiwa kifo miezi mitatu kabla





Padri Joseph Magamba wa Kanisa Katoliki Parokia ya Machui Zanzibar aliyemwagiwa tindikali akisaidiwa kushuka kwenye ndege na Padri Thomas Assenga(kushoto) wa Kanisa la Mtakatifu Joseph Zanzibar baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Julius Nyerere Dar es Salaam jana kuelekea katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.Picha na Fidelis Felix 

Siku moja baada ya Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Cheju, Mkoa wa Kusini Unguja, Joseph Mwang’amba kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana, imebainika kuwa alitishiwa kuuawa miezi mitatu kabla ya kukutwa na tukio hilo.
Wakati Padri huyo akieleza hayo, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, ameijia juu polisi kwa kushindwa kudhibiti matukio ya viongozi wa dini na serikali visiwani humo, kushambuliwa kwa kumwagiwa tindikali huku akilitaka kuwakamata waliohusika na tukio hilo.
Kiongozi huyo wa dini, aliyejeruhiwa maeneo ya usoni, mikononi na kifuani baada ya kumwagiwa tindikali hiyo alisafirishwa jana na ndege ya kukodi ya Shirika la Coastal kutoka visiwani humo hadi Dar es Salaam na baadaye kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Dk Shein alisema Polisi inatakiwa kuongeza nguvu za uchunguzi ili kukabiliana na matukio ya kikatili ya umwagaji wa tindikali, yanayoshamili visiwani humo hivi sasa.
“Hatuwezi kuviacha vitendo hivi viendelee … ni lazima Jeshi la Polisi lijitahidi kuwatafuta wahusika ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema Dk Shein.
Dk Sheni alisema, kitendo hicho ni cha kikatili na kisichovumilika na kuongeza kuwa wahusika lazima wasakwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake, Padri wa Parokia ya Mtakatifu Joseph, Zanzibar, Thomas Assenga aliyefuatana na kiongozi huyo mpaka MNH, alisema siku za nyuma Padri Mwang’amba alitolewa vitisho na mtu ambaye hamfahamu wakati akienda kutoa huduma katika kituo cha wazee cha Welezo.
Alisema kabla ya kufika kituoni hapo, kuna eneo ambalo nyakati za asubuhi watu hufanya mazoezi barabarani ambapo kuna mtu mmoja alimtolea maneno ya vitisho.
“Unajua kawaida ya watu wa Zanzibar hufanya mazoezi barabarani, sasa kipindi anapita eneo hilo katika kilima, kuna mtu alimwambia atamfanyia kitu kibaya ambacho hatujui ndiyo hiki au la,” alisema Padri Assenga na kuongeza:
Alisema Juni mwaka huu mara baada ya kupewa vitisho hivyo alikwenda kutoa taarifa kwa Sheha wa eneo hilo na kituo cha polisi.
“Mara baada ya kutolewa vitisho hivyo Juni mwaka huu, alichukua jukumu la kwenda kutoa taarifa kwa mkuu wa eneo hilo (Sheha) na kituo cha polisi.”
Akielezea tukio la kumwagiwa tindikali Padri Mwang’amba, alisema alimwagiwa saa 9:45 alasiri juzi wakati akizungumza na simu nje ya internet cafĂ© iliyopo eneo la Mlandege.
CHAZO: CAZETI LA MWANANCHI.
.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni