TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wazazi wametakiwa kubadilika na kuwapokea tena katika jamii vijana walifanikiwa kuacha matumizi ya madawa ya kulevya.
Wito huo umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati alipokuwa akizungumza na vijana walioko katika makazi ya vijana walioamua kuacha madawa ya kulevya huko Limbani, Wilaya ya Wete Mkoa wa Kuskazini Pemba.
Katika risala yao kwa Rais vijana hao walieleza kuwa moja ya matatizo wanayowakabili baada ya kufanikiwa kuacha madawa hayo ni kukataliwa na wazazi na kutotazwa vyema na jamii.
“wazazi hawana budi kukumbuka kuwa vijana hao ni watoto wao waliowazaa, kuwalea na kwamba pale mtoto anapopotoka na baadae kujirudi ni wajibu wao kuwapokea tena na kuwapa upendo kama zamani” alisema Dk. Shein.
Rais alieleza kuwa ametiwa moyo na mipango mizuri ya vijana hao kuwa Serikali ina kila sababu ya kuwaunga mkono na ni wajibu wake kama mlezi wa raia wote.
“Serikali ina kila sababu za kuwasaidia katika maisha yenu.Tunahitaji kuwaleta, kuwaenzi na kuwapa huduma kama walivyo wananchi wengine”alibainisha Dk. Shein.
Alimpongeza mwanzilishi wa nyumba hiyo ambazo hadi sasa zimefikia saba kisiwani Pemba bwana Abdulwahid Salim kwa uamuzi wake wa busara baada ya kufaulu kujitoa katika matumizi ya madawa ya kulevya kurejea nyumbani kutoka nchini Kenya ili kusaidia ndugu zake walioathirika.
“Tunampongeza na kumshukuru ndugu yetu Abdulwahid ambaye mara baada ya kuyashinda madawa ya kulevya huko nchini Kenya alikokuwa akiishi aliamua kurejea nyumbani kusaidia ndugu zake walioathirika na madawa hayo”Dk. Shein alisema.
Alisisitiza kuwa si jambo la busara hata kidogo kuwalaumu vijana hao kwa yaliyowakuta badala yake jamii iwaunge mkono katika harakati zao za kurejea katika maisha yaoe ya kawaida.
Akijibu maombi ya vijana hao Rais aliahidi kuwapatia kompyuta mbili ndogo (laptop) na magodoro 30 pamoja kuielekeza Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kuangalia namna ya kuongeza bajeti ya huduma za nyumba hizo.
Halikadhalika Dk. Shein aliwaahidi kuwasiliana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuangalia namna ya kutekeleza ombi lao la kupewa fursa za kutoa elimu dhidi ya matumizi ya madawa ya kulevya maskulini.
Kuhusu suala la kuwezeshwa aliwataka vijana hao kutumia fursa zinazotolewa na Serikali za uwezeshaji kwa njia ya mikopo ili nao waweze kufaidkka na huduma hizo kama wananchi wengine.
Akizungumza kabla Kiongozi wa Nyumba hiyo Bwana Abdulwahidi Salim alieleza kuwa kazi wanayoifanya katika nyumba hizo ya kiroho ya kuwarejesha vijana maisha yao ya kawaida na kuacha tabia ambazo zinaikera jamii ambazo ndizo zinazoifanya jamii kuwachukia na hata kukata kuwapokea tena katka jamii.
“Tumekuwa tukifanya kazi ya kuwafanya vijana hawa sio tu kuacha madawa lakini pia kuacha tabia chafu inazoichukiza jamii kama wizi, mauaji, ugomvi na uzinzi ambao unasababisha kusambaza virusi vya ukimwi” Alieleza Abdulwahid na kuvuta hisia za wananchi na viongozi waliokuwepo.
Awali akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji Tume ya Uratibu na Udhibiti wa Madawa ya Kulevya Bi Kheriyangu Mgeni Khamis alieleza kuwa Ofisi yake kwa kushirikiana na uongozi wa nyumba hizo wanaandaa muongozo wa namna ya kuendesha nyumba hizo ili kuweka taratibu na mwenendo unaofanana.
Alieleza kuwa katika kukabiliana na tatizo la jamii kuwakataa vijana hao wameanzisha mpango wa kutoa ushauri nasaha kwa jamii kwa kuwatumia vijana hao ili kuivuta jamii kuona kuwa vijana hao bado ni sehemu ya jamii na wana mchango kusadia jamii yao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni