Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji Nishati na Madini imeombwa kufikiria njia muwafaka ya kuyauza Majanareta yaliyopo katika kituo kikuu cha kupokelea Umeme Mtoni ili kuwepusha hasara endapo yataendelea kuwepo eneo hilo bila ya matumizi.
Majanareta hayo 30 yalikuwa yakitoa huduma za umeme wa dharura katika kipindi ambacho Zanzibar ilikuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa huduma ya nishati ya umeme kutokana na kinanzio chake ilichokuwa ikikitumia wakati huo kutokidhi mahitaji halisi ya huduma hiyo Nchini.
Mhandisi wa Maganareta katika Kituo Kikuu cha Umeme Mtoni Yussuf Reja alitoa ushauri huo wakati wa ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuangalia maendeleo ya uzalishaji wa huduma ya umeme Nchini kupitia miundo mbinu iliyopo katika kituo hicho.
Mhandisi Yussuf Reja alimueleza Balozi Seif kwamba Majanareta hayo yako katika kiwango bora lakini tatizo kubwa liliopo ni huduma ya mafuta ambayo ni maalum { IDO } na yana hitaji gharama kubwa za uendeshaji.
Alisema Shirika la Umeme lilikuwa likipata hasara ya zaidi ya shilingi Milioni 16,000,000/- kwa saa wakati maganareta hayo yalipokuwa yakiwashwa kusaidia huduma za umeme katika kipindi cha mgao wa huduma hiyo muhimu.
Mhandisi Yussuf Reja alifahamisha kwamba shirika la umeme lilikuwa likizalisha umeme kupitia Maganareta hayo kwa uniti moja yenye thamani ya shilingi 500/- ambayo ingelazimika kuwauzia wateja wake uniti moja kwa shilingi 700/- gharama ambayo ni mzigo kwa mwananchi wa kawaida.
“ Ukweli uliowazi gharama ya kuyaendesha Maganareta hayo kupitia shirika la Umeme ni kubwa mno na inaweza kuleta maafa kwa shirika hilo endapo yataendelea kutumiwa “. Alitahadharisha Mhandisi Yussuf Reja.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Madini Nd.Mustafa Aboud Jumbe alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Wizara hiyo tayari imeshapokea mapendekezo ya Shirika hilo kuhusiana na majanareta hayo ya Kituo cha Umeme Mtoni.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa Ardhi Mustafa Jumbe alisema Wizara hiyo inajipanga kuyafanyia kazi mapendekezo hayo na baadaye kuyawasilisha Serikali kuu kwa ajili ya kupatia ufumbuzi muwafaka.
Mapema Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } Thabit Salum Khamis alisema mfumo mpya wa kisasa wa huduma za umeme kwenye kituo kikuu cha Umeme Mtoni uitwao { SCADA } umewawezesha watendaji wa shirika hilo kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa.
Thabit Salum alimfahamisha Balozi Seif kwamba mfumo huo umepunguza kero kubwa ya kukatika katika kwa umeme kulikokuwa kukitoa usumbufu kwa wananchi walio wengi kwenye maeneo mbali mbali wakati inapotokea hitilafu.
Alieleza kwamba shirika la umeme limekuwa na vituo vikubwa vinavyosambaza umeme kutoka kituo kikuu cha Mtoni kwenda Welezo na Fumba ambavyo vimepangwa kusambaza huduma hiyo na kuacha mfumo wa zamani wa kutumia laini moja tuu.
Kaimu Meneja huyo wa Shirika la Umeme aliongeza kwamba matumizi zaidi ya umeme huongezeka kutoka Mega walts 33.16 nyakati za asubuhi hadi kufikia Mega Walts 48.1 kipindi cha jioni lakini huduma hiyo kuongezeka zaidi katika kipindi cha siku kuu na kufikia hadi Mega Walts 52.
Uwezo wa laini mpya ya umeme uliopo Zanzibar hivi sasa imefikia Mega Walts mia moja ambapo shirika limekuwa na hakiba ya umeme kwa zaidi ya asilimia 50% mbali ya ile laini ya zamani yenye uwezo wa mega walts 40 kutokana na kuchakaa kwake.
Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwatanabahisha watendaji wa shirika la umeme kwamba huduma ya umeme hivi sasa imekuwa nyenzo muhimu ya kiuchumi kwa vile inasaidia kipato cha mwananchi.
Balozi Seif alisema ni vyema kwa watendaji wa shirika la umeme kufanya kazi zao katika mazingira ya ushindani mfano wa kuwepo mashirika mengine yanayotoa huduma hizo hapa nchini kwa lengo la kupata ufanisi sambamba na kutoa huduma bora kwa wateja wake.
“ Watendaji lazima mfanye kazi kama mko katika ushindani wa kibiashara na mashirika mengine licha ya kwamba mpo peke yenu. Kila mkiamka lazima mfikirie mtaongeza vipi wateja wengine wapya “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha wafanyakazi wa shirika hilo kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya athari na hatari ya kutumia mafundi wa mitaani katika kuungiwa huduma hiyo jambo ambalo mara nyingi huleta hasara kutokana na hitilafu zinazojitokeza baadaye.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni