NA ASIA MWALIM
KATIKA jamii yoyote yenye misingi ya usawa na haki, ushiriki na ushirikishwaji wa watu wote ikiwemo watu wenye ulemavu kwenye masuala ya kijamii bila ubaguzi ni nguzo muhimu ya maendeleo endelevu.Kwa bahati mbaya hapa kwetu kushiriki na kushirikishwa watu wenye ulemavu kwenye masuala ya kijamii halijapewa kipaumbele na mara nyingi familia huwatolea maamuzi.Hata hivyo, historia inaonesha kuwa kundi hili limekuwa likikumbwa na changamoto za kijamii ikiwemo kukosa urithi wa mali, kushindwa kushiriki sherehe za harusi, vikao vya familia, misiba, michezo na mikutano.Watu wenye ulemavu ni sehemu ya jamii yenye uwezo, ndoto, na mchango mkubwa katika nyanja mbalimbali za maisha lakini wengi wao wamekua wakilalamika kukuosa fursa hiyo.TAKWIMU ZA WATU WENYE ULEMAVUKwa mujibu wa ripoti ya Mtakwimu Mkuu wa serikali kupitia, sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2022, watu wenye ulemavu kuanzia miaka 7 na kuendelea, ni asilimia 11.4 ya watu wote waliohesabiwa Zanzibar.Ripoti ya Takwimu inaonesha, kiwango cha hali ya watu wenye ulemavu kimeongezeka kwa asilimia 3.9 kati ya sensa ya mwaka 2012 na sensa ya mwaka 2022 kwa kipindi cha miaka 10.Pia mkoa wa kaskazini Pemba una kiwango kikubwa cha watu wenye ulemavu kwa asilimia 13.3 na mkoa wa kaskazini Unguja una kiwango kidogo cha asilimia 10.3 ya watu wenye ulemavu.Matokeo ya sensa yanaonesha kiwango cha hali ya ulemavu kipo juu zaidi kwa wanawake ikilinganishwa na wanaume katika Mikoa mingi ya Zanzibar.Wanaume wenye ulemavu Zanzibar ni asilimia 10.3 na wanawake ni asilimia 12.3 ikiongozwa na Mkoa wa Kaskazini Pemba wenye idadi kubwa ya wanawake wenye ulemavu kwa asilimia 14.1 ikilinganishwa na wanaume wenye ulemavu asilimia 12.2.Mkoa wa Kaskazini Unguja wanaume ni asilimia 9.5 na wanawake ni asilimia 11.2.Mkoa wa Kusini Unguja unaonesha kuwa, wanaume asilimia 10.7 wanawake asilimia 12.4, Mkoa wa Mjini Magharibi wanaume asilimia 9.6 na wanawake asilimia 12.0, na Mkoa wa Kusini Pemba wanaume 11.3 asilimia na wanawake asilimia 12.8.HALI YA WATU WENYE ULEMAVU ZANZIBARFakihat Omar Abubakar (24) kijana wa kike mwenye ulemavu wa viungo anasema ameshuhudia, familia nyingi haziwashirikishi watu wenye ulemavu kwenye shughuli za kijamii hata zile zinazowahusu.Anasema bado familia zimebeba mitazamo hasi juu ya watu wenye ulemavu kuwashirikisha ipasavyo kwenye masuala ya kijamii ikiwemo sherehe zinazojumuisha watu wengi, misiba, vikao, mikutano n.k.“Ni kweli hata mimi nilihudhuria sherehe ya harusi ya kifamilia, lakini watu wengi walistaajabu kuniona, wakisema maneno ya kunidhihaki kwa sauti ya chini nilijisikia vibaya na sikuwa na la kufanya” alisema.“utawasikia wanasema, Eti ilikuaje huyu kumleta hapa harusini si wangemuacha atulie awalindie nyumba” alieleza baadhi ya maneno ya kejeli aliyotupiwa.Kuonekana mtu mwenye ulemavu kwenye mikusanyiko linachukuliwa tofauti kwenye jamii wengi wamezoea kuwaficha na kutowashirikisha harakati za kijamii kama sherehe za harusi.Fakihat anasema kuna changamoto nyingi zinapaswa kutatuliwa ikiwemo kukosa wakalimani wa lugha katika hospitali hasa kwenye huduma za uzazi ambako watu wenye ulemavu wa uziwi wanasumbuka wakati wakujifungua.“Jambo la kukosa mkalimani katika vituo vya afya linapaswa kuchukuliwa hatua za haraka ili kundi la watu wenye ulemeavu kueleza yanayowasibu” alisema.Hidaya Suleiman Rashid, (45) mwanamke mwenye ulemavu wa viungo anasema watu wenye ulemavu wanapaswa kuheshimiwa, kusikilizwa, na kupewa nafasi ya kuchangia.“Ikiwa familia haziwashirikishi kwenye vikao watapata fursa ya kuchangia na kutoa mawazo yao?” aliuliza.Kwenye suala la heshima kumeharibika zaidi wanaonekana hawana ulewa wa kutoa maamuzi yanayofaa kwa sababu zisizo na msingi.Changamoto nyengine ni watu wenye ulemavu kutelekezwa, pia kukoseshwa huduma za msingi na kutopewa urithi.JAMII YA ZANZIBARNasra Khatibu Suleiman anasema, kutoshirikishwa watu wenye ulemavu kwenye masuala ya kijamii ni pengo kati ya watu wenye ulemavu na jamii na kuzuia maendeleo ya pamoja.Anasisitiza jamii kutilia mkazo suala la watu wenye ulemavu mambo yanayowahusu, ili kushiriki shughuli za kijamii ikiwemo elimu, ajira, siasa na michezo. Anaiomba serikali kuhakikisha mazingira, sera, na huduma zinakuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu ili kushiriki kikamilifu harakati za kijamii bila vikwazo.Rajabu Mohammed Abdallah na Mwanaisha Miraji wanasema Jamii ina nafasi ya kuhakikisha watu wenye ulemavu hawakumbwi na unyanyapaa. BARAZA LA TAIFA LA WATU WENYE ULEMAVUKatibu wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Ussy Khamis Debe anasema wanafuatilia utekelezaji wa mikakati ya ushiriki na ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu, ikiwemo kuwezesha uundwaji wa sera rafiki.Baraza limekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, hasa kupitia ushawishi wa kisera na utekelezaji.JUMUIYA YA WATU WENYE ULEMAVU ZANZIBAR (JUWAUZA)Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Salma Saadat anasema Jumuiya hiyo ina utaratibu wa kuandaa warsha na makongamano ya kuhamasisha ushiriki na ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu,kuendesha kampeni za kupinga unyanyapaa na ubaguzi.SHERIA YA WATU WENYE ULEMAVU ZANZIBARKatika sheria ya watu wenye ulemavu Zanzibar inaeleza kuzuia ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu, kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya, elimu, na ajira, kuweka masharti ya miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu, kutoa adhabu kwa taasisi au watu wanaokiuka haki za watu wenye ulemavu.HitimishoUshiriki na ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika shughuli za kijamii si suala la hisani, bali ni haki ya msingi ya binadamu Zanzibar ina fursa ya kuwa mfano wa jamii jumuishi barani Afrika.Jamii inapaswa kuendelea kubadilika, kuondoa vikwazo, na kuhimiza usawa ili kujenga Zanzibar jumuishi, yenye mshikamano, na inayothamini kila mwanajamii bila kujali hali yake ya kimwili au kiakili.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni