TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAADHIMISHO YA SIKU YA REDIO DUNIANI 2026
Siku ya tarehe 13 Febuari 2026, dunia inaungana kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Redio
siku iliyotangazwa na UNESCO mwaka 2011 na kupitishwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja
wa Mataifa mwaka 2013. Maadhimisho haya ni fursa ya kutafakari mchango wa redio
katika kuhabarisha, kuelimisha, kuburudisha na kuimarisha misingi ya demokrasia, haki
za binadamu na maendeleo endelevu.
Kaulimbiu ya mwaka huu, “Redio na Uaminifu” (Radio and Trust), inatukumbusha
kwamba uaminifu ndio muhimili mkuu wa taaluma ya habari. Redio haiishi kwa nguvu ya
mawimbi yake, bali kwa imani ya wasikilizaji wake. Bila uaminifu, hakuna ushawishi, bila
ukweli, hakuna uwajibikaji.
Kwa mujibu wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, kuna zaidi ya vituo 30 vya redio
vinavyofanya kazi hapa nchini. Ukuaji huu ni ishara ya kupanuka kwa sekta ya habari na
kuimarika kwa wigo wa mawasiliano. Hata hivyo, ukuaji wa idadi ya vituo haupaswi kuwa
kipimo pekee cha mafanikio. Mafanikio ya kweli yapo katika ubora wa maudhui, uhuru
wa uhariri, na uwezo wa redio kuwa sauti ya wananchi.
Redio imeendelea kuwa chanzo kikuu cha taarifa kwa wananchi wengi, hususan katika
maeneo ya vijijini. Katika jamii nyingi zinazoendelea, redio ndio chombo kinachowafikia
watu wengi zaidi kwa gharama nafuu na kwa lugha inayoeleweka.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova, aliwahi kusisitiza umuhimu wa
redio kwa kusema: “Radio is the mass medium that reaches the widest audience
worldwide. It is a powerful communication tool and a low-cost medium. (“Redio ndicho
chombo cha habari kinachowafikia watu wengi zaidi duniani. Ni chombo chenye nguvu
kubwa ya mawasiliano na ni cha gharama nafuu.”)
Kauli hii inathibitisha kuwa redio si chombo cha kawaida, bali ni muhimili wa mawasiliano
ya umma, hasa kwa makundi yaliyo pembezoni mwa maendeleo.
Hata hivyo, nguvu ya redio lazima iambatane na uhuru wake. Katibu Mkuu wa zamani
wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, aliwahi kusema:”No one should underestimate the
importance of a free media in a democracy.”(“Hakuna anayepaswa kubeza umuhimu wa
vyombo vya habari huru katika demokrasia.”)
Maneno haya yanabeba ukweli usiopingika: bila vyombo vya habari huru na
vinavyoaminika, misingi ya demokrasia hudhoofika.
Kwa muktadha wa Zanzibar, bado kuna changamoto za kisheria na kisera zinazoathiri
tasnia ya habari. Miongoni mwa changamoto hizo ni matumizi ya sheria zilizopitwa na
wakati kama Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar ya mwaka 1997 (iliyorekebishwa
2010) na Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu Na. 5 ya mwaka
1988. Aidha, bado kuna mapungufu katika ulinzi wa kisheria kwa waandishi wa habari na
katika utekelezaji wa haki ya kupata taarifa za umma.
Sambamba na hilo, Ibara ya 19 ya Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu (UDHR) ya
mwaka 1948 inaeleza kuwa “Kila mtu ana haki ya kuwa na maoni na kujieleza; haki hii
inajumuisha uhuru wa kutafuta, kupokea na kusambaza taarifa kupitia chombo chochote
cha habari… ”Hivyo basi, kulinda redio ni kulinda haki ya msingi ya binadamu.
Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Redio 2026, sisi wadau wa tasnia ya habari
Zanzibar tunatoa wito kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuharakisha mchakato wa
kupitisha Sheria Mpya ya Huduma za Habari inayozingatia viwango vya kitaifa, kikanda
na kimataifa vya haki za binadamu.
Kuanzishwa kwa chombo huru cha usimamizi wa vyombo vya habari kinachojitegemea
pamoja na kuhakikisha ulinzi wa kisheria na kiusalama kwa waandishi wa habari.
Kuimarisha utekelezaji wa haki ya wananchi kupata taarifa za umma na Vituo vya redio
kuwekeza zaidi katika uandishi wa uchambuzi na ufuatiliaji wa masuala ya wananchi
badala ya kujikita katika taarifa za matukio pekee.
Maadhimisho haya yasiishie kuwa tukio la sherehe. Yawe mwanzo wa hatua za mageuzi
ya kweli katika sekta ya habari. Kwa sababu kama alivyowahi kusema mwanahabari
mashuhuri Walter Cronkite:
“Freedom of the press is not just important to democracy, it is democracy.”
(“Uhuru wa vyombo vya habari si jambo muhimu tu kwa demokrasia - ndio demokrasia
yenyewe.”)
Wadau wa habari tunasisitiza kuwa Redio inapolindwa na kupewa uhuru wake kamili,
wananchi hupata sauti, wananchi wanapopata sauti, demokrasia huimarika, na
demokrasia inapoimarika, taifa hustawi. Kulinda redio ni kulinda mustakabali wa Zanzibar.
IMETOLEWA NA:
Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC),
Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ)
Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA)
Baraza la Habari Tanzania, Zanzibar (MCT, ZNZ)
Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Zanzibar (THRDC, ZNZ).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni