MAELEZO YA SERIKALI JUU YA HOJA MBALIMBALI ZA KAMATI YA PAC YA BARAZA LA WAWAKILISHI KUHUSU SHIRIKA LA UMEME LA ZANZIBAR (ZECO)
1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Itakumbukwa kwamba katika Mkutano wa Saba wa Baraza la Nane la Wawakilishi, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa kuchaguliwa na wananchi wa Jimbo la Kiwani, Mheshimiwa Hija Hassan Hija kwa kutumia haki yake chini ya Kanuni za Baraza ya 27 (1) (m), 27 (3), 48 (1) na 49 (1) Toleo la 2011 aliwasilisha hoja binafsi kwa mujibu wa Kanuni ya 117 ya Kanuni za Baraza na kulitaka Baraza liridhie kuunda Kamati Teule kwa ajili ya kulichunguza Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO).
Mheshimiwa Spika, Vilevile itakumbukwa kwamba Baraza lako Tukufu lilikubaliana kwamba hoja hiyo ya Mheshimiwa Hija Hassan Hija ifanyiwe kazi kupitia Kamati ya Kudumu ya Baraza ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC) na Mheshimiwa Hija mwenyewe kuingizwa katika kamati hiyo ili kusaidia katika uchunguzi huo.
Mheshimiwa Spika, kufuatia uamuzi huo wa Baraza, Kamati ya PAC ikimjumuisha Mheshimiwa Hija ilianza kufanya kazi hiyo rasmi tarehe 30 Aprili, 2012 na kuwasilisha ripoti yake Barazani katika Kikao cha Baraza kilichofanyika Mwezi wa Machi, 2013. Baada ya kuwasilishwa, Serikali iliahidi kuifanyia kazi ipasavyo Ripoti hiyo ya PAC na baadae kuwasilisha taarifa rasmi katika Baraza lako hili.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepokea Ripoti ya Kamati ya PAC ya Baraza lako kuhusu Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) kwa moyo mkunjufu na kuifanyia kazi kwa umakini mkubwa na uadilifu wa hali ya juu ili kuona mapungufu yaliyoonyeshwa katika Ripoti hiyo yanafanyiwa kazi kwa maslahi ya nchi yetu na vile vile wale walioguswa wanafanyiwa haki na uadilifu kufuatana na matakwa ya Sheria za nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukushukuru kwa dhati wewe mwenyewe binafsi kwa kukubali hoja ya Mheshimiwa Hija Hassan Hija kufanyiwa kazi na PAC. Aidha, nawapongeza kwa dhati Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Kamati ya PAC kwa kazi kubwa na nzuri walioifanya katika kuchunguza utendaji wa Shirika la Umeme la Zanzibar na kuwasilisha vyema kwa Baraza taarifa yao. Aidha, niwashukuru Wajumbe wote kwa michango yao na kufikia mapendkezo yenye ufanisi. Kwa kweli taarifa hii imetuonesha mambo mengi ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi na Serikali ili kuimarisha utendaji wa Shirika kwa maslahi ya Taifa letu. Muelekeo huu wa mashirikiano miongoni mwa mihimili mikuu ya Serikali ndio hasa utakao tusaidia katika kujenga mustakbali mwema wa nchi yetu na kuimarisha dhana ya utawala bora na kupambana na vitendo vyote viovu ndani ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar .
Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Baraza lako Tukufu kwamba Serikali tayari imeshaanza kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Baraza la Wawakilishi na kuchukua hatua stahiki katika baadhi ya maeneo yaliyopendekezwa na Wajumbe.
2.0 MAELEZO KUHUSU HOJA MBALIMBALI ZILIZOTOLEWA KATIKA RIPOTI YA KAMATI YA PAC
Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa maelezo hayo ya utangulizi sasa naomba uniruhusu kutoa ufafanuzi wa Serikali juu ya hoja mbali mbali zilizojitokeza katika Ripoti ya Kamati ya PAC kama ifuatavyo:
Hoja Nambari 1: Wateja kupewa risiti zenye kiwango kidogo kuliko malipo halisi waliyolipa.
Mheshimiwa Spika, katika Ripoti ya Kamati ilionyeshwa kasoro ya baadhi ya wateja wa Shirika kupewa risiti zenye kiwango kidogo kuliko malipo halisi waliyolipa wateja hao na hivyo Kamati kupendekeza kuwa watendaji wote waliohusika wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria.
Mheshimiwa Spika, maelezo ya Serikali kuhusu hoja hii ni kwamba Serikali inakubaliana na mapendekezo yaliyotolewa na Baraza lako Tukufu na tayari hatua imeshachukuliwa na Shirika la Umeme kwa kuliarifu Jeshi la Polisi kuanza kuchukua hatua za kufanya uchunguzi wa malalamiko ya wateja waliolalamikia kulipa fedha nyingi lakini risiti walizopewa zimeandikiwa fedha kidogo. Aidha, Serikali imelitaka Jeshi la Polisi liwatake wateja hao kuwabainisha watendaji waliohusika na suala hili ili liwachunguze na iwapo watabainika kuwa wamekiuka sheria na taratibu wachukuliwe hatua za kisheria.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kifungu Nam . 44 cha Sheria ya Shirika la Umeme Nam . 3 ya mwaka 2006, Serikali imemuagiza Waziri anaehusika na Sekta ya Nishati kuunda Kamati ya Rufaa za Wateja ili kushughulikia malalamiko ya wateja. Napenda kuwaarifu kwamba, hatua za kuunda Kamati ya Rufaa za wateja zinakaribia kukamilika. Mambo ya msingi yanayozingatiwa katika uundaji wa Kamati hii ni namna itakavyotekeleza majukumu yake. Hivi sasa Shirika la Umeme limo katika jitihada kubwa ya kushughulikia manung’uniko ya wateja na kutoa huduma zake bila upendeleo na kuepusha kuwepo hisia za mianya ya rushwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Fundi Salum Saad Khamis, naomba kuliarifu Baraza lako Tukufu kwamba mfanyakazi huyo tayari amesimamishwa kazi ili kuruhusu hatua za uchunguzi ziweze kuchukuliwa dhidi yake.
Mheshimiwa Spika, Vilevile napenda kuliarifu Baraza lako Tukufu kwamba Shirika la Umeme tayari limeshaliandikia Jeshi la Polisi kukumbushia kuhusu kesi yenye Nambari RB1250/2012 iliyopo Kituo cha Polisi Chake Chake na RB302/2013 ya Kituo cha Polisi Konde zinazomuhusu Ndugu Abeid Mohammed Abeid ili Jeshi hilo liharakishe uchunguzi haraka iwezekanavyo na upelelezi utakapokamilika na kukidhi vigezo vya kisheria hatua za kisheria zichukue mkondo wake dhidi ya mtuhumiwa huyo. Aidha, Kamishna wa Polisi Zanzibar ametakiwa kusimamia kwa karibu ili utekelezaji wa suala hili uende haraka.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwajulisha Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwamba tayari barua za onyo zimetolewa kwa Meneja Mkuu na Meneja wa Tawi la Pemba kwa kutokuwa makini katika kusimamia majukumu yao na kushindwa kuwasimamia vyema watendaji walio chini yao . Barua hizo za onyo zimetolewa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Nambari 2 ya 2011. Na bado Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mienendo ya watendaji hao ili kuona wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria za utumishi wa umma. Iwapo wakibainika kwenda kinyume, hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao .
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imetoa onyo la mwisho la maandishi kwa Ndugu Ahmed S. Yussuf kwa kitendo chake cha kujifanya wakala wa wateja wanaotaka kuungiwa umeme wakati yeye ni mfanyakazi wa Shirika. Aidha, Serikali haitomvumilia mtendaji yeyote wa Shirika atakaekwenda kinyume na maadili ya kazi yaliyowekwa.
Hoja Nambari 2: Fedha za Malipo ya kuungiwa umeme kuingizwa katika Akaunti ya Mtendaji wa Shirika, Ndugu Zakia Juma Azan
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Kamati ya PAC ilipendekeza kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu dhidi ya mhusika Ndugu Zakia Juma Azan kwa kutokuwa muadilifu katika utekelezaji wa majukumu yake. Ndugu Zakia alijihusisha na uwakala wa mteja wa kuungiwa umeme wakati huo huo akiwa ni mfanyakazi wa Shirika la Umeme. Hatua hiyo inapelekea kuwa na mgongano wa kimaslahi baina ya Ndugu Zakia na Shirika la Umeme. Kutokana na hali hiyo, Serikali inakubaliana na pendekezo hilo la Kamati na tayari hatua ya kumhamisha Ndugu Zakia kutoka Shirika la Umeme imechukuliwa. Hatua hizo za kinidhamu zimechukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Nambari 2 ya mwaka 2011. Mfanyakazi huyo amehamishwa kutoka Shirika la Umeme kwenda Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati na huku akiangaliwa utendaji wake.
Hoja Nambari 3 na 6: Kuwepo kwa makisio ya aina mbili kwa mteja mmoja.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Serikali inaishukuru Kamati kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kugundua mapungufu haya ambayo yalichangia kulikosesha Shirika la Umeme mapato kutokana na udanganyifu wa baadhi ya watendaji wa Shirika kutoa makisio ya aina mbili kwa mteja mmoja. Serikali imelitaka Shirika la Umeme kuwa makini katika utendaji wake na kuzingatia sheria na taratibu za kazi na Wizara husika imetakiwa kuwa karibu zaidi kulisimamia Shirika ili mapungufu kama haya yasitokee tena. Aidha, Shirika limetakiwa kuanzia sasa kuwa wazi kwa kuweka bayana vigezo na viwango bila ya kuwepo mwanya wa ubabaishaji ili kila mteja anaetaka kuunga umeme aweze kujua gharama zake. Vile vile, Shirika limetakiwa kuwa makini katika kufanya tathmini ya gharama za wateja wakati wa kuwaungia umeme na kutoa makisio na maelezo sahihi ya aina na sifa za vifaa vinavyotakiwa (Specifications) kwa mteja ili kuepuka wateja kununua vifaa visivyokuwa na viwango vinavyotakiwa au visivyohitajika.
Hoja Nambari 4, 17 na 18: Ushiriki wa Mohammed & Bashir kwa niaba ya Sana Express katika zoezi zima la uungwaji wa umeme katika Hoteli ya Misali.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja ya Kamati juu ya ushiriki wa Duka la Mohammed & Bashir ambalo halimo katika orodha ya maduka/makampuni yaliyopewa kibali na Shirika cha kuuza na kusambaza vifaa vya umeme. Shirika tayari limeiandikia rasmi Kampuni ya Mohammed & Bashir kusitisha mara moja biashara ya uuzaji wa vifaa vya umeme na kwamba Shirika halitosita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Kampuni yoyote itakayoendesha biashara inayohusu masuala ya umeme bila ya kibali cha Shirika. Aidha, Serikali imeliagiza Jeshi la Polisi na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kufanya uchunguzi wa kina kwa Kampuni hiyo ya Mohammed & Bashir kuhusu tuhuma za kutumia risiti za Kampuni ya Sana na kwa kufanya hivyo kuna uwezekano wa mhusika kukwepa kulipa kodi. Vile vile, Serikali imelitaka Shirika kuanzia sasa kuhakikisha linajiandaa kuwa na vifaa vya kutosha vinavyokidhi mahitaji ya wateja wanaotaka kuungiwa umeme sambamba na kuhakikisha kuwa vifaa vya umeme vinavyotoka nje ya nchi vinakuwa na viwango bora kwa kuvifanyia ukaguzi unaostahiki kabla havijaanza kutumika kwa kushirikiana na taasisi inayohusika na ubora wa viwango (Zanzibar Bureau of Standards-ZBS)
Hoja Nambari 5: Namna ya upatikanaji wa vifaa vya uungwaji wa umeme katika Hoteli ya Misali.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja hii ya vifaa vilivyotumika kuunga umeme kwenye Hoteli ya Misali vilivyochukuliwa kutoka katika ghala la Shirika, kumejitokeza mgongano wa maelezo yaliyotolewa. Hivyo, Serikali imemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kufanya uchunguzi zaidi wa suala hilo . Baada ya uchunguzi huo wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, Serikali itachukua hatua muafaka kwa kuzingatia ushahidi utaopatikana.
Hoja nambari 7: Fundi Abeid Mohammed Abeid si Mfanyakazi wa Shirika lakini anafanya kazi za Shirika kinyume na utaratibu.
Mheshimiwa Spika, tunakubaliana na hoja ya Baraza lako Tukufu kuwa fundi Abeid Mohammed Abeid si mfanyakazi wa Shirika la Umeme na kwa kutambua hilo, Serikali imelitaka Shirika kuwa makini na watu kama hao ambao wanafanya kazi za Shirika lakini si waajiriwa wa Shirika hilo na kupelekea kulihujumu Shirika. Shirika tayari limeliandikia Jeshi la Polisi na kulitaka kufanya upelelezi wa kina kwa suala hili na kwa wahusika wote na kuchukua hatua muafaka za kisheria dhidi ya wale wote watakaobainika kuhusika na makosa hayo.
Hoja Nambari 8: Kukiukwa agizo la Bodi ya Wakurugenzi kuhusu mgongano wa maslahi katika ushiriki wa Ndugu Hamidu Saidani Ali na Ndugu Ali Abeid Haji katika ZECO na GECCO.
Mheshimiwa Spika, Suala la kuwepo kwa mgongano wa maslahi (conflict of interests) kuhusu baadhi ya wafanyakazi wa ZECO pia kuwa ni wafanyakazi wa Kampuni binafsi ya GECCO ni jambo ambalo halikubaliki hata kidogo. Ili kuondoa mgongano wa maslahi, Serikali imechukua hatua ya kuwahamisha wafanyakazi hao na kuwapeleka sehemu nyengine.
Hoja Nambari 9: Watu walioungiwa umeme kinyume na utaratibu, na baadhi ya Wateja kutumia huduma hii bila ya kusajiliwa na hivyo kutumia umeme bure. (Hawamo katika orodha ya Wateja wa Shirika).
Mheshimiwa Spika, Serikali inakiri kwamba lipo tatizo la baadhi ya watendaji wa Shirika ambao si waadilifu huwaungia umeme wateja kinyume na utaratibu uliowekwa na Shirika kwa maslahi yao binafsi. Hivyo, Shirika tayari limeshaliandikia Jeshi la Polisi kuanza uchunguzi wa kina kwa wale wote waliotajwa katika Ripoti ya PAC kuwa wameungiwa umeme kinyume na utaratibu na kuwataka watu hao kuwataja watu waliowaungia umeme huo. Baada ya uchunguzi hatua za kisheria zichukuliwe kwa watakaobainika wana makosa.
Hoja Nambari 10: Mkurugenzi Mkuu wa ZBC aliruhusu Kampuni Binafsi ya Zanzibar Data Com kutumia umeme kutoka katika mnara wa ZBC kinyume na utaratibu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Serikali inaendelea kulifuatilia suala hili kutokana na kukosekana kwa taarifa zitakazowezesha kutoa maelezo sahihi.
Hoja nambari 11 na 25: Ndugu Mohamed Hashim Ismail aliagiza kurudishwa umeme kwenye mnara wa Kampuni ya Zanzibar Data Com. kinyume na utaratibu.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya PAC ilimuona aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Ndugu Mohammed Hashim Ismail kuwa ameliingiza Shirika katika hasara kwa kuagiza kurudishwa umeme katika mnara unaotumiwa na Kampuni ya Zanzibar Data Com kinyume na utaratibu. Serikali imefuatilia hoja hii na kuona kwamba hakuna hasara iliyopatikana kutokana na amri ya Mwenyekiti wa Bodi, kwa sababu wakati wa kurudishwa umeme huo Shirika liliiwekea Kampuni hiyo mita ya TUKUZA na deni lake lote la nyuma liliingizwa katika mita hiyo. Kwa sababu hiyo Serikali imeona hakuna sababu za kumchukulia hatua za kisheria Mwenyekiti huyo wa zamani wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme.
Hoja Nambari 12: Bodi ya Wakurugenzi ya ZECO ikiongozwa na Mwenyekiti wake Ndugu Mohamed Hashim Ismaili iliichagua Kampuni ya CRJE badala ya Salcon iliyoshinda zabuni katika ujenzi wa misingi ya majenereta 32 na baadae kuvunja mkataba na CRJE uliopelekea Shirika kulipa fidia ya Dola za Kimarekani 20,786.00 na kulitia hasara Shirika.
Mheshimiwa Spika, ni kweli Bodi ya ZECO iliichagua Kampuni ya CRJE badala ya Kampuni ya Salcon iliyoshinda zabuni ya ujenzi wa misingi ya majenereta 32 na baadae kulazimika kuvunja mkataba na Kampuni hiyo ya CRJE. Hata hivyo fedha zilizolipwa hazikuwa za fidia ila ni malipo ya kazi iliyowahi kufanywa na CRJE. Aidha, Serikali baada ya kulichunguza suala hili pia iligundua kwamba Kampuni ya MANTRAC walilipwa fedha zao za ujenzi kama kwamba Kampuni ya CRJE haikulipwa kabisa. Hivyo, Serikali imeliagiza Shirika la ZECO liliandikie MANTRAC kulipa fedha za CRJE.
Hoja Nambari 13: Tofauti ya malipo kwa kazi inayofanana, au wakati mwengine kazi kubwa kuwa na malipo madogo katika uungaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Shirika kutoza malipo tofauti kwa kazi zinazofanana Serikali imelitaka Shirika liwe makini katika kufanya tathmini za gharama za wateja wakati wa kuwaungia umeme. Vile vile Shirika limeagizwa kuweka viwango vya bei vinavyoeleweka kwa ajili ya uungaji wa umeme ili kila anaehitaji huduma aweze kujua gharama halisi.
Hoja Nambari 14: Upendeleo katika uungwaji wa umeme ambapo baadhi ya wateja walioomba mwisho wanapewa kipao mbele kuliko wale walioomba mwanzo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa dhamira ya Shirika si kufanya kazi kwa upendeleo, hivyo Shirika litajtahidi kuepuka manung’uniko na litoe huduma bila ya upendeleo na liepushe hisia za kuwepo mianya ya rushwa.
Hoja Nambari 15: Malipo yanayolipwa na baadhi ya Wateja bila ya kupewa risiti kabisa. Baadhi ya wateja kuuziwa vifaa vya Shirika lakini hakuna risiti za mauzo hayo Mfano: Atlas Hoteli.
Mheshimiwa Spika, Serikali imelitaka Shirika la Umeme litoe elimu kwa wananchi kwamba kamwe wasikubali kulipa pesa mikononi kwa mtu yoyote kwa ajili ya kupata huduma za umeme, malipo yote yalipwe katika Shirika na walipaji wapewe risiti zinazolingana na kiasi cha fedha walizotoa. Shirika liwe makini kuhakikisha kwamba watu wote wasiowaaminifu na wasiokuwa watendaji hawatumii jina la Shirika kujinuafaisha binafsi. Programu ya kutoa elimu kwa wananchi tayari imeanza na itaendelea kwa kutumia njia ya redio, televisheni na kwa maofisa wa Shirika kutembelea maeneo mbalimbali ya wateja. Aidha, Serikali imeona hakuna haja ya kuchukuliwa hatua yoyote kwa Hoteli ya Atlas kwa vile upo ushahidi wa risiti wa kwamba hoteli hiyo imelipa gharama za vifaa vilivyotumika kwa kuungiwa umeme.
Hoja Nambari 16: Kazi kubwa ya kuunga umeme kwenye minara ya simu za mkononi kupewa Kampuni binafsi badala Shirika kuifanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii ya kazi kubwa kupewa Kampuni binafsi badala ya kufanywa na Shirika lenyewe, Serikali tayari imeliagiza Shirika la Umeme kuhakikisha kwamba kazi ya kuunga umeme katika maeneo yote inafanywa na Shirika lenyewe isipokuwa pale inaposhindikana ndio Shirika liidhinishe Kampuni binafsi kufanya kazi hizo. Aidha, Shirika lihakikishe kuwa sheria na taratibu zinafuatwa kikamilifu katika kuteua Kampuni binafsi na kwamba hakutakuwa na mgongano wa kimaslahi baina ya ZECO na Kampuni hizo, viongozi au kwa watumishi.
Hoja Nambari 19: Shirika kuendelea kuiruhusu GECCO kufanya Biashara ya Transforma wakati kuna agizo la Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika kufuta kibali cha biashara hiyo kwa Kampuni ya GECCO.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeshangazwa sana na kitendo cha ZECO kuwakataza GECCO kuuza transfoma huku Shirika hilo likiendelea kuzikubali transfoma za GECCO zinazoletwa na wateja na pia kutoheshimu maamuzi ya Bodi iliyolikataza Shirika hilo kupokea transfoma kutoka Kampuni ya GECCO. Kutokana na hali hiyo, Serikali imelitaka Shirika la Umeme Zanzibar kuheshimu maamuzi ya Bodi ya Wakurugenzi yanayotolewa kwa Shirika hilo. Serikali tayari imeshamuonya Meneja Mkuu wa ZECO kuhusiana na suala hili na kuliagiza Shirika kuchukua hatua za kinidhamu kwa wengine wote waliohusika na suala hili.
Hoja Nambari 20: Upotevu wa kumbukumbu za Mteja Ras Kichanga.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeliagiza Shirika la Umeme kufanya uhakiki kwa wateja wake wote wakubwa na wadogo ili kujua idadi halisi ya wateja na kuweka kumbukumbu zao. Aidha, Serikali imeliagiza Shirika la Umeme kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wafanyakazi waliohusika na kitendo cha kuyaacha majalada ya wateja wa Shirika hilo kuroa. Pia agizo limetolewa kwa Shirika hilo kuwachukulia hatua za kinidhamu wafanyakazi wote waliohusika na upotevu wa majalada ya wateja wakubwa wa Shirika pamoja na wateja wa vituo vya minara ya simu. Shirika tayari limeanza kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wahusika wote kwa kuwataka kutoa maelezo kwa nini Shirika lisiwachukulie hatua kwa makosa waliyoyafanya.
Hoja Nambari 21: Kutochukuliwa hatua za kisheria dhidi yaResidence Hotel ambayo ilivuta umeme kwa kutumia Kampuni ya CRJE badala ya ZECO. Na kuiruhusu Kampuni ya GECCO kufanyakazi ya uungaji wa umeme huku ikieleweka wazi kuwa sheria inakataza suala hilo.
Mheshimiwa Spika, Kuhusu hoja hii, Serikali imebaini kuwa kazi ya uungaji wa umeme katika Hoteli ya Residence imefanywa na ZECO na Kampuni ya CRJE imeilipa ZECO gharama za kazi ya uungaji (labour charge). Kampuni ya GECCO imeiuzia kampuni ya CRJE vifaa vya umeme vilivyotumika katika kazi hiyo.
Hoja Nambari 22: Kuruhusu uungwaji wa Umeme kwa Kendwa Beach Resort, Docrim Hotel na The Leisure Hotel bila ya kufuatwa taratibu.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kwamba masuala kama haya hayajirudii, Serikali imelitaka Shirika la Umeme kuhakikisha kwamba linawahakiki wateja wote wakubwa na wadogo ili kujua idadi halisi ya wateja na kumbukumbu zao, kazi ambayo tayari Shirika limeanza kutekeleza kwa kuandaa mfumo wa kumbukumbu za wateja “Data Base” ambao utakuwa unafanyiwa mapitio mara kwa mara. Aidha, Serikali imelitaka Shirika kuhakikisha kwamba kila mteja anaetaka kuungiwa umeme anajaza fomu ya maombi ya kuungiwa umeme na taarifa zake zinahifadhiwa vizuri ili ziweze kupatikana wakati zitakapohitajika.
Hoja Nambari 23: Kushindwa kuthibitisha wapi zimenunuliwa nguzo na transforma zilizotumika katika nyumba ya kupumzikia ya Ndugu Shumbana Amani Karume. Kushindwa kuthibitisha wapi imenunuliwa Transforma ya “The Sayyida Hotel” na wapi yamelipwa malipo ya gharama za uungwaji wa umeme wa Hoteli hiyo na taratibu zipi zilizotumika. Aidha, kusamehewa kodi ya VAT kwa Hoteli hiyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya ukaguzi wa eneo linalohusika na hoja hii na kubaini kwamba nguzo zilizotumika katika kupeleka umeme huo ni ishirini (20) na Shirika la Umeme ndilo lililopeleka nguzo hizo. Aidha, Serikali ilipeleka umeme kwa kuelewa kwamba eneo hilo ni eneo la Uwekezaji na tayari hoteli mbili (2) zimeshajengwa.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa hoja inayoihusu “The Sayyida Hotel”, napenda kuliarifu Baraza lako Tukufu kwamba hoteli hiyo ililipa kodi ya VAT kama ilivyohitajika. Aidha, hoteli hiyo haikuunga umeme kwa kutumia transfoma yake.
Hoja Nambari 24: Upatikanaji wa transforma ya hoteli ya Larosa Deivent na kwa nini taratibu za kawaida hazikufuatwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefuatilia suala hili na kubaini kwamba transfoma iliyowekwa katika Hoteli ya Larosa Deivent imenunuliwa na mmiliki wa hoteli hiyo kutoka kampuni ya OSAJU.
Hoja Nambari 26: Kampuni ya Zanzibar Data Com kwa mnara wa Mtoni inadaiwa kiasi gani? na italipa kwa utaratibu gani na kwa muda gani?
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Zanzibar Data Com ilikuwa inadaiwa jumla ya Dola za Kimarekani 9,600 na hadi kufikia mwezi wa Oktoba, 2013 Kampuni hiyo ilikuwa imekwishalipa Dola za Kimarekani 3,600 na kubakia deni la Dola za Kimarekani 6,000. Shirika la Umeme limeingia makubaliano na Kampuni ya Zanzibar Data Com ambapo utaratibu ni kufanya malipo kila mwezi ambayo yanatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 24 kuanzia mwezi Machi, 2013.
Hoja Nambari 27: Suala la kuhamishwa “Internal Auditor” kutoka Pemba na kwa nini kwa muda mrefu Akaunti za hesabu za Pemba hazijafanyiwa ukaguzi wa ndani na wala wa nje?
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Baraza lako Tukufu kwambani kweli Mchunguzi wa Hesabu wa Ndani (Internal Auditor) wa Shirika la Umeme wa Pemba alipewa uhamisho. Hatua za kumhamisha mfanyakazi huyo zilichukuliwa kutokana na kutowajibika kwake ipasavyo, kitendo ambacho kilipelekea kutotoa ripoti za ukaguzi hata moja kwa kipindi chote alichokuwepo katika nafasi hiyo. Hivi sasa Shirika tayari limeshampeleka Mchunguzi wa Hesabu wa Ndani mwengine wa kudumu huko Pemba na pia Serikali imeiagiza Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuzifanyia ukaguzi hesabu za Shirika hilo huko Pemba.
Hoja Nambari 28: Hakuna ruhusa iliyotoka kwa Bodi ya Wakurugenzi kuhusu ajira ya wafanyakazi 16 walioajiriwa mwaka 2008.
Mheshimiwa Spika, Serikali inakubaliana na hoja ya Kamati ya PAC na kulitaka Shirika kutofautisha baina ya kuidhinishwa kwa bajeti na kuidhinisha kwa uajiri. Hivyo, Shirika limetenda kosa la kuajiri wafanyakazi 16 mwaka 2008 bila yakupata idhini ya Bodi ya Wakurugenzi, na hivyo Serikali tayari imempa onyo Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme na kumtaka awe makini zaidi katika utekelezaji wa majukumu yake na kufuata sheria.
Hoja Nambari 29: Kasoro zilizotajwa kuhusu uajiri kuanzia 2008 mpaka 2012.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kasoro zote zinazohusiana na masuala ya uajiri zilizotajwa katika hoja hii, Serikali imeliagiza Shirika la Umeme kufuata kwa ukamilifu sheria na taratibu zote za uajiri kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 2 ya mwaka 2011, ikiwemo kuzitangaza nafasi za kazi, kuweka vigezo sahihi, kufanya usaili na kuwepo mikataba ya ajira. Aidha, Shirika limetakiwa kuandaa mpango wake mkuu wa mafunzo utakaotekelezwa bila ya upendeleo.
Hoja Nambari 30: Uuzwaji wa Gari Land Rover SLS 1023 na Toyota Pick Up SLS 1045 ambazo ziliuzwa bila ya idhini ya Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja hii naomba kulieleza Baraza lako Tukufu kwamba barua iliyotoka Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo kuidhinisha kuuzwa mali za Shirika la Úmeme haikuidhinisha uuzwaji wa gari Nam. SLS 1023 Land Rover na SLS 1045 Toyota Pick Up. Gari hizo ambazo hazikuidhinishwa aliuziwa Ndugu Shaibu Hassan Kaduara. Hivyo, Serikali imeagiza kufanyika uchunguzi wa kina kubaini mazingira yaliyopelekea Ndugu Kaduara kuuziwa gari hizo. Serikali tayari imemuandikia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kulishughulikia suala hilo. Aidha, hatua za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa kwa waliohusika iwapo itabainika kuwa gari hizo ziliuzwa bila kufuatwa utaratibu.
Hoja Nambari 31: Uuzaji wa Mali za Shirika ambazo ziliuzwa na Uongozi wa Shirika badala ya Kitengo cha Manunuzi kama sheria inavyoelekeza (kifungu nam. 175(3) cha Kanuni za Sheria Nam. 9 ya mwaka 2005.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Serikali inakubaliana na mapendekezo ya Kamati ya PAC na hivyo imeiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika hilo kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa kupewa onyo wote waliohusika na kuuza mali za Shirika bila kufuata utaratibu uliowekwa na Serikali.
Hoja Nambari 32: Tofauti kati ya orodha ya vitu vilivyoidhinishwa na Bodi na vitu halisi vilivyouzwa na Shirika katika mnada wa tarehe 18/12/2011.
Mheshimiwa Spika, katika hali ya kawaida, tungetarajia kuwa kwa vile Shirika la Umeme Tawi la Pemba liliorodhesha idadi ya vitu walivyotaka kuviuza, Afisi Kuu ya Unguja ilipaswa kuorodhesha vifaa vyote vilivyoruhusiwa kuuzwa na vilivyokuwa havikuruhusiwa kuuzwa na mauzo yafanywe kwa mujibu wa ruhusa hiyo. Hivyo, kwa kuwa kuna vitu vimeuzwa bila ya kufuata utaratibu, Serikali inaendelea kufanya uchunguzi na hatua za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa kwa wahusika wote watakaobainika na makosa
kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma na Sheria ya Manunuzi.
Hoja Nambari 33: Transforma ya KVA 1500 ambayo haimo kwenye vifaa vilivyopigwa mnada iliondolewa katika eneo iliyokuwepo na haijulikani ilikopelekwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja hii, Serikali imeiagiza Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kulifanyia uchunguzi ili kubaini uhalisia wa suala hili. Hatua za kisheria na kinidhamu zitachukuliwa kwa wale watakaobainika kuhusika na upoteaji wa transfoma hiyo.
Hoja Nambari 34: Kukodi gari kwa mtu binafsi kwa ajili ya kazi za Shirika na kutumia pesa nyingi badala ya kununua gari yake kama hiyo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli muda wa miezi tisa (9) ni mrefu kwa kukodi gari ya mtu binafsi kwa kufanya kazi za Shirika. Hivi sasa Shirika la Umeme tayari limeshapata gari zake na hivyo limeachana kabisa na utaratibu wa kukodi gari za mizigo za watu binafsi. Aidha, Shirika limetakiwa wakati wote kuweka mawazo ya kibiashara na kuepuka kulitia hasara Shirika.
Hoja Nambari 35: Licha ya kuwepo na mkataba baina ya Shirika na Mtu Binafsi (Mwenye gari) kwa nini alikuwa anatiliwa mafuta kutoka katika vituo vya mafuta vya Shirika? Fedha alizokuwa akikatwa zilikuwa zinakwenda wapi?
Mheshimiwa Spika, Serikali ilifuatilia hoja hii na kuona kwamba ni kweli baadhi ya siku gari lililokodiwa lilitiwa mafuta na Shirika baada ya kukosekana mafuta katika vituo vya mafuta. Gharama za mafuta aliyokuwa akitiliwa zilikuwa zinakatwa katika malipo ya mwenye gari hiyo na fedha kurudi katika Shirika kwa faida kwa vile Shirika lilikuwa linanunua mafuta hayo kwa bei ya jumla na kumkata mwenye gari hiyo kwa bei ya reja reja. Hivyo, hakukuwa na upotevu wa fedha za Shirika.
Hoja Nambari 36 na 37: Majenereta 32 ya Shirika la Umeme yaliyopo Mtoni yalipatikana kwa fedha za MDRI au Mfadhili na taratibu gani zilotumika katika kuyanunua?
Mheshimiwa Spika, Napenda kutoa ufafanuzi kwamba Majenereta haya hayakununuliwa kwa fedha za MDRI bali yalinunuliwa kwa fedha za Wahisani na Serikali. Aidha, ununuzi huu ulifanywa kwa mashirikiano baina ya Wahisani na Serikali chini ya Mshauri wa Mradi wa Umeme Vijijini aliyekubalika na Wahisani hao. Ununuzi huo ulifanyika chini ya utaratibu wa manunuzi katika hali ya dharura ambao ulikubalika na pande zote mbili.
Hoja Nambari 38: Mpango wa Shirika la Umeme Zanzibar wa kuyatumia majenereta 32 ya dharura kwa ufanisi na kwa kutumia gharama nafuu.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja ya kutakiwa Shirika kuwa na Mpango wa matumizi wa majenereta 32 ya dharura, Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati tayari imeandaa mapendekezo kuhusu majenereta hayo ya dharura na Serikali itajadili mapendekkezo hayo na itatoa maelekezo kwa Wizara husika hivi karibuni.
3.0 MTAZAMO WA SERIKALI KUHUSU RIPOTI YA KAMATI YA PAC
Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa ufafanuzi juu ya hoja mbalimbali zilizotolewa katika Ripoti ya Kamati ya PAC yapo mambo ambayo Serikali imeona ni vyema kutoa mtazamo wake ili kuwa na uchambuzi unaostahiki (balanced scrutiny) na kuweka mwelekeo mwema wa baadae. Aidha, mtazamo huo wa Serikali una nia ya kutoa ushauri juu ya masuala yaliyojitokeza kwa Kamati wakati ikitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria. Hatua hii itatusaidia pale itakapotokea haja ya kuwa na Kamati Maalum au Kamati Teule inayoundwa kuchunguza jambo ili kamati hiyo iweze kufanya kazi zake kwa uadilifu na bila ya kuonekana kuwa na upendeleo (bias).
Mheshimiwa Spika, Serikali inashauri katika kazi zijazo za Kamati ni vyema ripoti zikaonesha kwa uwazi maelezo kamili yanayotolewa na watendaji. Aidha, Serikali inashauri kwamba Baraza liangalie Kanuni ya 120 na kuona uwezekano wa kuifanyia marekebisho ili mjumbe anaetoa hoja asiwe mjumbe wa Kamati itakayoundwa kuchunguza hoja hiyo.
4.0 HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar naomba kwa mara nyingine tena kuchukua fursa hii kukushukuru wewe binafsi kwa jinsi unavyosimamia kazi za Baraza kwa umakini na umahiri mkubwa na kuniwezesha kuwasilisha taarifa hii ya Serikali kwa Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako. Vile vile naomba nichukue fursa hii kwa mara nyingine tena kumshukuru sana Mheshimiwa Hija Hassan Hija, Mwakilishi wa Wananchi wa Jimbo la Kiwani kwa ujasiri wake na uzalendo wake wa kuibua hoja ambayo kwa kweli imetuonesha mapungufu tuliyokuwa nayo katika Shirika, mapungufu ambayo Serikali imeweka nia ya dhati ya kupambana nayo si kwa Shirika la Umeme tu bali kwa taasisi zote za Umma.
Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuwashukuru na kutoa pongezi kwa Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Mheshimiwa Omar Ali Shehe na Wajumbe wote wa Kamati hiyo kwa kazi kubwa na nzuri iliyoibua mambo mengi muhimu yenye mustakbali mwema katika kulijenga Shirika letu na kuimarisha uchumi wa Taifa letu. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi kwa kuridhia kamati ya PAC kufanya kazi hii ambayo sote faida yake tumeiona na kwa kufuatilia kwa utulivu na umakini mkubwa maelezo ya Serikali niliyoyatoa. Pia nawashukuru wale wote waliyosaidia Kamati ya PAC kufanya kazi zake kwa kuwapatia taarifa walizozihitaji. Ni imani yangu kuwa viongozi na watendaji serikalini pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi sote kwa pamoja tutaitumia fursa hii ya kuibuka kwa hoja hizi kujifunza na kubadilika kwa dhati na kuachana na tabia ya kufanyakazi kwa mazoea ili kuzidi kuijengea heshima nchi yetu, kuendelea kujenga imani kwa wananchi wetu na kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi yetu. Haya yote yanawezekana, sote tushirikiane na tutimize wajibu wetu.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni