Mahakama kuu ya jimbo la Shandong mashariki mwa China imemruhusu mwanasiasa wa zamani wa ngazi ya juu wa nchi hiyo, Bo Xilai, kukata rufaa baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha jela. Bo Xilai alitiwa hatiani mwezi uliopita na mahakama ya Jinan kwa makosa ya uhalifu na matumizi mabaya ya madaraka. Maisha yake ya siasa yalikatizwa mwaka jana na kashfa ya mauaji ambapo mke wake, Gu Kailai, alipatikana na hatia ya kumuua kwa sumu mfanyabiashara wa Uingereza, Neil Heywood, aliyekuwa rafiki wa familia yao. Katika taarifa fupi kwenye tovuti yake, mahakama hiyo imesema Bo Xilai anaweza kukata rufaa lakini haikutoa taarifa zaidi wala kusema ni lini rufaa hiyo itakaposikilizwa. Ingawa Bo Xilai ana haki ya kukata rufaa, hukumu dhidi yake huenda isibatilishwe kwa kuwa mahakama zinadhibitiwa na chama tawala cha kikomunisti, ambacho kilisema ana hatia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni