Habari

Ijumaa, 14 Februari 2014

Nyerere alitaka Shirikisho lenye serikali tatu



J.Mihangwa,
“MUUNGANO huu unatubana mno…..na Muungano ni kama koti tu, likikubana unalivua”. Haya ni maneno ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar na mwasisi wa Muungano, hayati Abeid Amani Karume aliyoyatamka mwaka 1968, miaka minne kabla ya kifo chake akionyesha kukerwa na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Kauli hii haikumfurahisha Baba wa Taifa la Tanzania [la Tanganyika na Zanzibar?], Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyetaka Muungano ulindwe kwa nguvu zote, tofauti na Karume alipoonekana kuchoshwa na Muungano kutokana na kile alichokiita “kupelekwa puta kwa Muungano unaokiuka makubaliano”.
Tangu mwanzo, Karume alielewa kwamba, alilazimika kuingia Muungano kwa shinikizo na ghiliba. Aliwahi hata kutishia kutohudhuria sherehe za kubadilishana “Hati za Muungano” na kutangazwa rasmi kwa Muungano huo, mjini Dar es Salaam Aprili 26, 1964.
Na kwa sababu hizo hizo, aliendesha Zanzibar atakavyo, kana kwamba haikuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati Nyerere alizidi kuimeza Zanzibar kwa kuongeza mambo ya Muungano kwa imla, kutoka 11 ya mwanzo hadi 16 wakati wa kifo cha Karume.
Uhasama kati ya viongozi hawa wawili ulifikia hali ya kutisha kuelekea kipindi cha kifo cha Karume kiasi cha wawili hao kutoongea ana kwa ana kwa zaidi ya mwaka mmoja. Mawasiliano yao yalikuwa kupitia wapambe wao, Bhoke Munanka kwa upande wa Nyerere, na Aboud Jumbe kwa upande wa Karume. Kisa? Mfarakano juu ya Muungano!
Kuna wakati Mwalimu Nyerere [mwaka 1968], alikuwa karibu kusalimu amri. Akiandika katika gazeti la “The London Observer” la Aprili 20, 1968, alisema kwa kulalama: “Kama umma wa Wazanzibari, bila ya kurubuniwa kwa hoja za nje, na kwa sababu zao wenyewe, wataona Muungano si wa manufaa kwa uhai wao [na kuamua kujitoa], sitawapiga mabomu kuwalazimisha waendelee na Muungano”.
Yote haya yalitokana na kutekeleza Muungano wenye muundo tata. Wakati Karume aliamini aliingia Muungano wenye Shirikisho lenye Serikali tatu – Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali Kuu ya Muungano, Nyerere kwa upande wake, alitaka Muungano wenye Serikali mbili – Serikali ya Muungano [ambayo pia ndiyo Tanganyika] na Serikali ya Zanzibar, lengo likiwa kuelekea Serikali moja kwa sababu maalumu kama tutakavyoona baadaye.
Na hiyo ndiyo sababu ya kuongezwa kwa mambo ya Muungano kinyemela, kinyume na matakwa ya Mkataba wa Muungano wa Aprili 22, 1964.
Siku moja kabla ya Karume kuuawa Aprili 7, 1972, aliyekuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Salim Rashid, alikwenda kumuaga kwamba alikuwa anajiuzulu kazi serikalini. Karume alimsihi asifanye hivyo na kumhakikishia kwamba [yeye Karume] alikuwa anakusudia kuvunja Muungano siku chache baadaye. Hata hivyo [Karume] hakubahatika kuifikia siku hiyo kuweza kutekeleza alilokusudia, kwa sababu ya kifo.
Wachambuzi wa mambo ya siasa za Muungano wanaamini kwamba, kama Karume angeishi mwaka mmoja zaidi ya 1972, Muungano huu ungevunjika haraka, kwa adha na kwa hali ya kutisha. Lakini pamoja na hayo, kifo chake hakikuzika mzimu wa kero za Muungano tangu hapo hadi leo, mambo yameendelea vile vile.
“Tunang’ang’ana kujadili Muungano kijuujuu bila kugusa Mkataba wa Muungano. Kwa nini hatujadili Mkataba wa Muungano? Hii ndiyo hati pekee inayohalalisha Muungano na ni msingi na chimbuko kuu la Katiba. Kwa nini tumefanya kujadili Mkataba wa Muungano kuwa dhambi?
Migogoro, mikanganyiko na mitafaruku yote juu ya Muungano inatokana na kukataa kujadili Mkataba huo ambao ndio “Cheti cha kuzaliwa cha Muungano”. Ni maneno ya Rais wa awamu ya pili Zanzibar, Aboud Jumbe akihoji Kikao Maalum cha Halmashauri Kuu [NEC] ya CCM iliyomwita kumhoji na hatimaye kumvua nyadhifa zote za uongozi kwa kuhoji muundo wa Muungano, Dodoma, Januari 24 – 30, 1964: Soma Mhtasari wa Kikao hicho, ukurasa 116 – 117].
Jumbe, kama Karume, alikuwa ameanza kubaini jinsi utekelezaji wa Muungano ulivyopelekwa puta bila kuzingatia Mkataba wa Muungano kwa mtizamo wa Muundo wa Serikali mbili kuelekea Serikali moja, na kuzua hofu miongoni mwa Wazanzibari kwamba “nchi” yao ilikuwa inamezwa taratibu na Tanganyika.
Na hiki ndicho kilichomsukuma Jumbe kutumia haki yake ya kikatiba kutaka kuhoji kwenye Mahakama Maalumu ya Katiba kupata ufafanuzi juu ya Muundo sahihi, ridhaa inayopatikana kwa kila Mtanzania chini ya ibara ya 125, 126 na 128 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977.
“Awali ya yote, niweke wazi kuwa, chini ya Mkataba wa Muungano, uhusiano wa kisiasa uliokusudiwa ni wa Shirikisho. Mkataba wa Muungano haukufuta Tanganyika wala Katiba na Sheria za Tanganyika”, alisema Jumbe kwa kutoa changamoto kwa NEC ya CCM iliyomwita kumhoji.
Akaendelea, “Ule ukweli kwamba Tanganyika ilikabidhi mambo yake kwenye Muungano, haimaanishi kwamba Tanganyika ilikufa. Huu ulikuwa mpango wa muda tu kusubiri Katiba ya Muungano”,
Kwa hili, bila shaka, Jumbe alikuwa ananukuu ibara ya 5 ya Mkataba wa Muungano na kifungu cha 8 (1) cha Sheria ya Muungano, Namba 22 ya 1964, vinavyotamka kuwa; “Kuanzia siku ya Muungano na kuendelea, Sheria za Tanganyika na Sheria za Zanzibar zitaendelea kuwa na nguvu katika nchi hizo kwa mambo yote yasiyo ya Muungano”,”.
Mwalimu akacharuka, akasema: “Sasa mkanganyiko wa mawazo umezuka. Makamu [Makamu Mwenyekiti wa CCM - Jumbe] anasema kuna Serikali tatu; mimi nasema mbili. Ni suala la Mkataba wa Muungano. Na kesi imeandaliwa kwenda Mahakamani kwa Serikali ya Mapinduzi kuishitaki Serikali ya Muungano kwenye Mahakama [maalumu] ya Katiba. Ukuu wa Chama. Kwa kosa gani Serikali ya Zanzibar iishitaki Serikali ya Muungano?….. Makamu, jiuzulu sasa hivi”, Mwalimu akamwagiza Jumbe kikaoni.
Jumbe akajiuzulu [kwa shuruti?] nyadhifa zote za Chama na Serikali kwa dhambi ya kuhoji Muundo wa Muungano. Na kuanzia hapo akawekwa chini ya Ulinzi nyumbani kwake “Mji mwema” kwa miezi mingi.
Mwalimu alikuwa muumini wa Serikali tatu.
Kama tutakavyoona baadaye, tangu mwanzo, Mwalimu hakuwa muumini wa Serikali mbili, bali wa Shirikisho. Kwake Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulivyo, ulikuja kama ajali tu.
Ulitokana na shinikizo la nchi za Magharibi enzi za vita baridi, zikimtumia Nyerere “aimeze” Zanzibar ndani ya tumbo kubwa la Tanganyika baada ya Shirikisho la Afrika Mashariki kushindwa ili isiangukie mikononi mwa Wakomunisti kufuatia Mapinduzi ya Kikomunisti Zanzibar ya Januari 12, 1964.
Mwanzoni, Nyerere alikuwa mpinzani mkubwa wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, pale wazo hilo lilipowasilishwa kwake na Balozi wa Marekani, Februari 1964; na tena Machi 7, 1964 na Naibu Waziri wa Nchi wa Marekani [Mambo ya Afrika], Jimmy Trimble. Lakini taratibu, alianza kuona hatari mbele yake kwa Zanzibar ya Kikomunisti [hakupenda Ukomunisti mwanzoni] kuwa mlangoni mwa Tanganyika, huku nchi za Magharibi nazo zikimshinikiza achukue hatua juu ya jambo hilo.
Alianza kutambua udhaifu wa Serikali yake na wa nchi zingine za Kiafrika dhidi ya hatari kutoka nje. Si hivyo tu, tangu mwaka 1960 kabla ya uhuru, alihofia Zanzibar kuwa karibu na Tanganyika akatamka wazi wazi akisema: “Kama ningekuwa na uwezo wa kukisukuma kisiwa kile [Zanzibar] hadi katikati ya bahari ya Hindi, ningefanya hivyo. Sitanii. Nina hofu [kwamba], huko mbele kitakuja kutuumiza kichwa”.
Juhudi zote za Nyerere kuona Shirikisho la Afrika Mashariki [EAF] likiundwa, zilikuwa ni kuhakikisha Zanzibar inamezwa ndani ya Shirikisho, na pale Shirikisho hilo liliposhindwa, akaona njia pekee ya kuondokana na hofu yake [na sasa kwa kupewa nguvu pia na Marekani na Uingereza ambazo nazo zilikuwa na hofu ya Ukomunisti kuenea Afrika Mashariki kupitia Zanzibar] ni kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika.
Kuhusu Muundo wa Serikali mbili alioendeleza, tofauti na Serikali tatu za Mkataba wa Muungano, unalenga Serikali moja kwa kuongeza taratibu [kinyemela] mambo ya Muungano ili hatimaye Zanzibar ijikute imenyang’anywa mambo yote kuwa chini ya Serikali ya Muungano ambayo ndiyo Tanganyika pia. Ugomvi wa Karume na baadaye Jumbe juu ya Muungano umejikita hapo. Na hivi karibuni, Rais wa Zanzibar, Dakta Mohamed Shein, amewakemea wote wanaodhani Zanzibar siyo nchi yenye mamlaka kamili waache uzandiki huo.
Nyerere alisalimu amri kwa shinikizo
Vitisho na shinikizo la Marekani na Uingereza vilimfanya Mwalimu akubali Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kukidhi matakwa ya Mataifa hayo. Vitisho vipi?. Kwanza, alikuwa bado na kumbukumbu yenye hofu jinsi alivyonusurika kupinduliwa na Jeshi lake mwenyewe, Januari 20, 1964; na jinsi alivyookolewa na Jeshi la Waingereza ambao ndio pia walioshinikiza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Na hata kama angekataa kuungana, Uingereza na Marekani, chini ya mpango wa kivita ulioitwa “Zanzibar Action Plan” [ZAP], zilikuwa tayari kuivamia Zanzibar kijeshi, kama Karume angekataa Muungano.
Uhakika ni kwamba, majeshi ya Uingereza, chini ya Kamanda wa Jeshi la Anga – “Royal Air Force” [RAF], Brigedia Jenerali I. S. Stockwell, na Kamanda wa Jeshi la Ardhini nchini Kenya, Brigedia Jenerali I. H. Freeland, yalipewa Amri [Joint Operation Instruction] Namba 2/64 kuvamia, huku yakitarajia upinzani na kipigo kutoka Jeshi la Zanzibar [Zanzibar Liberation Army – ZLA] chini ya Uongozi makini wa Kanali Ali Mahfoudh, na pengine kwa msaada kadhaa wa silaha kali kutoka China na Urusi.
Pili, Mwalimu bado alikuwa akikumbuka kwa hofu, kuuawa kwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Kongo, Mwanamapinduzi Patrice Emery Lumumba, na Rais Sylivanus Olympio wa Togo, waliouawa kikatili chini ya kile kilichoitwa “mchezo mchafu wa nchi za Magharibi dhidi ya Viongozi wanamapinduzi barani Afrika”.
Kwa hili, Nyerere aliona lazima achukue hatua haraka badala ya kusukumwa na kujiweka rehani kwa ugomvi wa mataifa makubwa ya Magharibi na Mashariki. Na hii ilikuwa Baraka pia kwake kumaliza “hofu” yake juu ya Zanzibar huru.
Muungano huo, ambao ulibuniwa baada ya kuvunjika kwa mpango wa EAF mjini Nairobi, Aprili 10, 1964, ulikuwa njia pekee ya kumzuia aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Mambo ya Nje wa Zanzibar wa wakati huo na Mkomunisti, Abdulrahman Mohamed Babu na mawakala wenzake wa Wachina [Chicoms] na Warusi, asidhibiti na kuhodhi madaraka ya Serikali ya Mapinduzi Visiwani.
Kuna dhana isiyo kweli kwamba Machi 1964, Mwalimu na Karume walikutana Ikulu Dar es Salaam ambapo Mwalimu alipendekeza kwa Karume juu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na eti kwamba Karume alikubali mara moja akisema: “Ita waandishi wa magazeti; waambie kwamba sisi tuko tayari sasa hivi”.
Dhana hii imepotoshwa. Maneno ya Mwalimu yalikuwa hivi: “Tazama, nimewaeleza wazi wazi Waziri Mkuu [Jomo] Kenyatta na Waziri Mkuu [Milton] Obote kwamba, wao wakiwa tayari kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki, sisi [Tanganyika] tuko tayari. Na sasa nakwambia na wewe [Karume, kama nilivyowaambia Kenyatta na Obote], kwamba Zanzibar mtakapokuwa tayari kuunda Shirikisho [hilo], sisi [Tanganyika] tuko tayari”.
Ukweli ni kwamba, alichomwambia Karume ni juu ya uundaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki na si Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Ingekuwaje hivyo wakati muda huo Nyerere alikuwa akifukuzia Shirikisho la Afrika Mashariki kuliko kitu kingine chochote, hadi juhudi hizo ziliposhindwa Aprili 10, 1964 na kugeukia Zanzibar?
Nani anasema Mwalimu alitaka Serikali mbili?
Tumesema, Mwalimu tangu kale hakuwa muumini wa Muungano wenye Serikali mbili ila kwa Tanganyika na Zanzibar kwa lengo maalumu. Kwenye Mkutano wa nchi huru za Afrika mjini Cairo, Julai 1964, alionyesha wazi wazi kutopendelea Muundo huo aliposema, “Muundo wa Serikali moja [Unitary System of government] haufai kwa Afrika kwa sasa; Muundo bora ni ule wa Shirikisho la Nchi”.
Akitetea hoja hiyo baadaye, aliandika makala ndefu kwenye Gazeti la “Africa Forum” [Vol.1 No. 1] mwaka 1965 akisema: “Mfumo bora ni ule wa Shirikisho lenye Serikali Kuu ya Muungano na Serikali za nchi zinazoungana, kila moja ikiwa na Mamlaka juu ya Mambo yasiyo ya Muungano”. Msimamo wake huo ameurudia pia katika Kitabu chake: “Uhuru na Umoja” [Freedom and Unity] ukurasa 300 – 304.
Na hivyo ndivyo alivyoamini Mzee Karume. Akitoa taarifa kwa Serikali yake kwa simu ya maandishi [telegraph], aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini Zanzibar kabla na baadaye kidogo kufuatia Muungano, jasusi la CIA, Frank Carlucci, Aprili 23, 1964 alisema, “Karume ametia sahihi [Aprili 22, 1964] Hati [Mkataba] ya Muungano akiamini kwamba ameingia Mkataba wa kuunda Shirikisho lenye Serikali tatu”.
Na siku za karibuni kabla ya kifo chake, baada ya kuchoshwa na kero za Muungano zisizoisha, Mwalimu alitambua utata wa Muundo wa Serikali mbili alisema muundo huo yafaa ujadiliwe kuondoa utata hata kama yeye alikwishatoa msimamo wake wa Serikali mbili.
Ukweli Mwalimu alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa, kama isingekuwa kwa “mambo fulani fulani” juu yake, asingemvua Jumbe madaraka kwa kuhoji Muundo wa Muungano.
Je, hawa wanaojifaragua, hivi sasa, kwamba kujadili Muundo wa Muungano nje ya Serikali mbili ni kumsaliti Mwalimu, wanatoa wapi ujasiri huo kuuhadaa umma? Kama ni kumsaliti Mwalimu, tusemeje juu ya hao hao waliohujumu Azimio la Arusha na Ujamaa; waliobinafsisha mali za umma bila kujali ili kuwapa ulaji mawakala wa ubepari? Je, si wasaliti, hao hao wanaokigeuza Chama cha Mwalimu [CCM] kichaka na kimbilio la mafisadi wasiotaka kujivua gamba?.
Sio siri tena kwamba Wazanzibari wengi hawapendelei Muungano wa Serikali mbili au moja, mbali na wanaotaka uvunjwe. Lakini Wahafidhina wa siasa za makundi, kwa unafiki mkubwa, wanajifanya kutoliona hili.
Ni hao hao waliopinga mchakato wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Visiwani, wakiwamo Wajumbe wa NEC ya CCM, mpaka Rais wa wakati huo, Amani Abeid Karume akatishia kuwaumbua.
Uhafidhina huo na unafiki wao wa kutaka kuona migogoro na kero za Muungano zikiendelea ndio unaofanya waishi kwa gharama ya amani na umoja wa Kitaifa wa nchi yetu.
Sasa, ifike mahali waambiwe wazi wazi, waache demokrasia na mawazo ya wananchi juu ya Muundo wa Muungano wautakao yatawale badala ya ubinafsi wao. Na tunaposhinikiza mambo dhidi ya matakwa ya wengi tunatafuta nini, na nini hatima ya yote haya?
chanzo:raiamwema

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni