Na Ally Saleh
Tulipoambiwa tu kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba anataka kuzungumza na Wajumbe wote wa Tume, basi wengi wetu tulijua kuna kubwa limetokea. Na kubwa hilo wengi tuliamini ni la Dr Sengondo Mvungi. Maana tuliitwa kwa dharura.
Tokea tukio la kushambuliwa Dk Mvungi, Tume iliweka utaratibu wa kuwaarifu Wajumbe kila hatua inayofanywa kuhusiana na jitihada za kuokoa maisha ya mwenzetu huyo aliyeshambuliwa na wale walioitwa majambazi nyumbani kwake.
Uso wa Mwenyekiti Warioba haukuonyesha dalili yoyote. Na hii ilitokana na kuwa yeye ni mtu mzima lakini pia kwa nafasi yake ya kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa nchi amepitia matukio kama hayo mengi na kwa hivyo hakuna wakati ambapo anatakiwa aonekane kuwa mtulivu na anaeweza kutoa maelekezo na uongozi kama wakati huu wa kumpoteza mmoja ya Wajumbe ambao amefanya nao kazi kwa mwaka mmoja na nusu sasa.
Kwa wengi wa Wajumbe wa Tume, Dk Mvungi si Mjumbe tu bali ni mwanataalama aliyebobea katika fani ambayo kama alikuwa hajawahi kuifanyia kazi katika ngazi ya kitaifa basi alikuwa akiifanyia sasa katika kuwa na mchango wa uundaji wa Katiba Mpya ya Tanzania.
Dk Mvungi alisomesha, alivuta hewa na alikula Katiba. Tuliofanya nae kazi kwa muda huu tumemjua uwezo wake na kwa hakika tumeona jinsi ya kiwango cha uzalendo wake katika kuhakikisha kuwa Tanzania inapata Katiba Mpya ya kweli, haki na yenye kujali pande zote mbili za Muungano.
Mchango wake, kwa sababu ya uelewa wake ulikuwa muhimu kila wakati. Alikwamua, alielekeza na alitoa suluhu na mbadala kila ambapo Tume ilikuwa ikihitaji kufanya hivyo na kwa hakika alitumia elimu yake kadri ya uwezo wake kama kwamba alijua kuwa hii ni kazi yake ya mwisho.
Hata siku ambayo usiku wake alishambuliwa na majambazi, akiwa katika Kamati ndogo ya Tume, alizama katika mjadala na wenziwe na walipokwama alimwambia Mjumbe mmoja, “ Wacha leo hii kazi tuilaze, lakini Jumatatu tutaipatia suluhu.” Kumbe Mungu hakutaka afike Jumatatu, ila Mjumbe mwenziwe Awadh Ali Said, aliachiwa maandishi yake tu juu ya hoja waliokuwa wakiijadili.
Wakati wa kuapishwa Tume Ikulu, Rais Jakaya Kikwete alimdhihaki Dk Mvungi kwa kusema kuwa aliwahi kumkuta Dk Mvungi amejifungia hoteli moja Bagamoyo akitengeza Rasimu ya Katiba ambayo alikuwa ni moja ya michango ya yeye na wazaleondo wenziwe waliotaka kuifanya kuchangia hatma ya nchi hii.
Mimi binafsi niliwahi kuwa nae katika kundi la vyama vya kisiasa ambalo lilikuwa pia likifanya juhudi kama hiyo ya kuandika Katiba ambayo baadae ingepelekwa Serikali kwa sababu wakati huo mwaka 2004 Serikali haikuwa kabisa na nia ya kuiletea nchi hii Katiba mpya.
Kwa hivyo Dk Mvungi hakuwahi kukaukwa na kiu wala kukosa njaa ya Katiba. Na ndio maana busara ya Rais Kikwete ikaona kuwa elimu yake na uzoefu wake unahitajika sana katika Tume ya Katiba ambayo kwa sasa kila Mtanzania amejua umuhimu wake.
Tulikuwa nae Dk Mvungi katika hatua mbili za Katiba. Kwanza ni ile ya kwenda kwa wananchi kukusanya maoni na yeye akapendelewa kwenda katika Mikoa 5 kwa sababu akiwa na Mwenyekiti wa kundi lake Mjumbe Muhammad Yussuf Mshamba ambaye anakiri hajawahi kupata rafiki kama huyo maishani mwake.
“ Kwa kuwa nae kwa muda wa miezi 4 nilibahatika kufanya urafiki mkubwa na Dk Mvungi. Hakuwa mwenzangu katika kazi tu, lakini mwenzangu kwa kila kitu kwa sababu niliweza kumjua kwa undani tu ingawa nilijuana nae katika Tume.”
Mshamba anamuelezea Dk Mvungi kuwa ni mwana demokrasia, hodari wa kusikiliza, mcheshi na mkweli. Anasema hajawahi kumuona Dk Mvungi akikasirika na kama aliwahi kukasirika basi alikuwa hodari wa kuficha hisia zake, lakini daima alionekana kuwa ni mtu asieweka kinyongo.
Wengi wa Wajumbe walimjua Dk. Mvungi kwa wingi wake wa utani. Lakini nae hakujiweka katika daraja kubwa na kwa hivyo alitaniwa sana, ambapo ni kielelezo kuwa pamoja na kuwa Tume ya Warioba ilikuwa na kazi ngumu, lakini moja ya kitu kilichoifanya kazi yao iwe nyepesi na Wajumbe kushibana na kujiweka wote katika hali moja.
Moja katika utani ambao Wajumbe wa Tume walipenda kumdhihakia Dk Mvungi ni lile tukio lilotokea Wilaya ya Kusini Unguja pale wakati wa kukusanya maoni alipoinuka na kujitambulisha na badala ya kuiamkia hadhira kwa kusema “Assalam alaykum” basi yeye akaanza kwa kusema “ Alaykum salaam.” Kama ilikuwa makusudi au la, hio ilikuwa ni njia yake ya kupata kukubalika.
Lakini pia alihadhithia katika pirika hizo aliona jina lake halimkurubishi na hadhira ya Zanzibar. Na kwa sababu katika majina yake limo jina Hamis Mwarabu akaona ni bora ajitambulishe jina lake kuwa ni Hamis Mwarabu Mvungi. Maana jina kamili ni Edmund Sengondo Hamis Mwarabu Mvungi jina ambalo wana Tume tulijulishwa na mwenza wake mkubwa Professa Palmagamba Kabudi, ambaye yeye atakuwa ameumia zaidi kuliko Wajumbe wote wa Tume.
Dk Mvungi alikuwa mtu wa vitendo na mbunifu wa kweli. Alifanya kazi kubwa katika kipindi cha Mabaraza ya Katiba. Moja katika kitu ambacho kila nikikumbuka kinanisimamisha malaika ni ile fikra aliyokuja kuibuni ya kujaribu kuwaambia Wajumbe wa Mabaraza kuwa Katiba ni zaidi ya maandishi bali ni maridhiano ya watu na matabaka, matakwa, dhamira na uhai wao na kwa ujumla ni zaidi ya vyama.
Ili kuwatia hamasa Wajumbe wajadili Rasimu ya Katiba katika muktadha huo alikuwa akiwaambisha Wajumbe Wimbo wa Taifa wa Tanzania. Niliposikia nilitamani kila siku niwepo na Watanzania wenzangu hao kuimba Wimbo huo unaotuunganisha sote kama nchi, dola, watu, wazalendo na wenye miliki ya nchi hii.
Mimi binafasi nimemjua Dk Mvungi kwa sababu alikuwa ni mwalimu wangu wa somo la Katiba wakati nikiwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Lakini nimemjua zaidi ndani ya Tume ya Katiba ambapo hapakuwa na mpaka au kipingamizi baina yangu na yake kwa sababu yeye ni mwalimu na mimi ni mwanafunzi. Dk. Mvungi hakukasirika kukosolewa hata na watu kama mimi.
Kwa hakika kumbe kwake ni zaidi ya nilivyojifikiria na hilo nililijua wakati Mjumbe Simai Muhammed Said alipomuuliza kwa utani tu, “ Unamuonaje Ally Saleh…alikuwa mwanafunzi hodari au pocho?” nae akajibu, “ Alikuwa hodari. Na kwa kweli nimeshaMmbia kuwa nataka aje awe mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Bagamoyo.”
Baada ya miaka kadhaa ya kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam maisha ya Dk Mvungi yamemalizikia akiwa katika Chuo Kikuu cha Bagamoyo na bila ya shaka pengo lake litaonekana kama amewaacha wakati Chuo hicho ndio kwanza kinakwenda tata.
Wengi kwenye Tume tutamkubuka Dk Mvungi kwa moyo wake wa kujitolea. Hakatai kazi yoyote anayopewa na huomba hasa apewe ikiwa amehisi msaada wake au utaalamu wake utahitajika na kwa kweli kila wakati ulihitajika.
Nimefanya nae katika Kamati mbali mbali za Tume kwa muda mwingi na kuweza kumjua zaidi. Na nikiwa nae ndani Kamati hizo nimejifunza kuwa alikuwa ni mtu aliyekuwa na uwezo wa haraka wa kufikiri lakini kubwa zaidi ni utayari wake wa kutoa na sio kungojea kupewa.
Sote tunajua kuwa uundaji wa Katiba kwa sehemu kubwa ni maridhiano na Dk Mvungi alikuwa hodari sana kwa maridhiano kiasi ambacho simjui nani mwengine kama huyo katika Tume na hicho ndicho ambacho tutakikosa katika hatua hii muhimu na ya mwisho katika Rasimu ya Pili.
Dk. Mvungi alikuwa amejipanga kwenda katika Bunge la Katiba kusimamia matunda ya kazi yake na yetu na siku moja kwa mzaha alisema, “Nashona suti kwenda Bunge la Katiba,” maana aliamini kile ambacho na wenzake wamejaribu kulitengezea taifa.
Dk Mvungi hakuwahi kushona suti maana ni wiki ile ile aliyoshambuliwa lakini pia ni wiki iliyofuata Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipitisha Sheria ya kuitoa Tume isingie katika Bunge kufanya ufafanuzi wa Rasimu ya Pili baada ya kuwasilishwa kwa maana kuwa uhai wa Tume kumalizika mara baada ya uwasilishaji wake kwenye Bunge la Katiba.
Lakini nina hakika hilo halingekuwa muhimu kwake. La muhimu kwake lingekuwa kukamilisha kazi ya Rasimu ya Pili na Tume ya Katiba kuwa rekodi kuwa imeweza kuifanya kazi iliyopewa na taifa na kutoa mapendekezo ya namna bora zaidi ya kuidesha nchi hii kwa miaka mingi ijayo na katika zama mpya.
Japo amefariki lakini Dk. Mvungi ameandika jina lake na tutaishi nae katika zama mpya. Hataondoka, hatafutika nyoyoni mwetu, hatakimbia akilini mwetu kwa sababu Dk Mvungi ametuachia mengi ya kuyashika, kuyaenzi na kuishi nayo milele na milele.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni