Habari

Jumamosi, 30 Novemba 2013

Wananchi wa Cheke Chake walia na hali mbaya ya Chinjio.

Na Is-haka Mohammd, PEMBA.                                                                                  Baraza la Mji wa Chake Chake limeombwa kuchukua hatua za haraka kulifanyia matengenezo Chinjio la Ng`ombe liliopo Kisiwani Wilaya ya Chake Chake kutokana na Chinjio hilo kuwa katika hali mbaya.


Wakizungumza na Zenj FM baadhi ya wenye Mabucha na wananchi wa Chake Chake wamesema hali iliyopo hivi sasa katika Chinjio hilo linatishia usalama wa afya za wananchi wanaokula nyama iliyotoka katika chinjio hilo.
Wamesema kuwa chinjio hilo limekosa huduma muhimu kama vile maji kwa ajili ya kusafishia, jambo linalowalazimu wachinjaji kutumia maji ya bahari ambayo yenyewe huwapa usumbufu mkubwa hasa wakati wa maji yanapokuwa yametoka.
Aidha wamesema mashimo yaliyopo katika sakafu hiyo ni kero kubwa kwani hata pale maji wahudumu wa chinjio siku wanayopata kufanya usafi maji hubakia kwenye vidimbwi hivyo na kutoa harufu kali.
Wamesema kuwa kutokana na hali iliyopo hali za watumiaji wa nyama zipo mashakani na endapo hatua hazikuchukuliwa kunaweza kuleta madhara ya kiafya kwa wananchi wanaonunua nyama inayochindwa katika chinjio hilo la Kisiwani.
Katibu wa Baraza la Mji wa Chake Chake Nassor Suleiman Zahran amesema anafahamu kuwa Chinjio hilo halipo katika hali nzuri, hata hivyo amesema baraza limo katika mpango wa kulifanyia ukarabati hivi karibuni.
 Amesema miongoni mwa kero hizo ni pamoja na kutokuwemo kwa maji ya uhakika katika Chinjio hilo,ambapo amedai kuwa walichimba kisima lakini kimezidiwa na wanajamii wa kisiwani.
Hata hivyo amesema hatua ya kulifanyia marekebisho zipo njiani kukamilika na kuwataka wananchi hao kuwa na subra huku, baraza likiwa katika mkakati huo wa kulifanyia matengenezo.
Kwa upande mwengine Nassor amewata wachinjaji ng`ombe kuacha tabia ya kutumia mashoka bila ya kuweka magogo wanapovuja nyama za mifupa kwa vile ndiyo chanzo cha kuwepo kwa vishimo vinavyopelekea maji kutuwama.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni