Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2013,Nd,Juma Ali Simai,akijitambulisha kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,(kulia) wakati alipofika Ikulu Mjini Unguja leo kwa mazungumzo.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.].
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 06 Disemba, 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka vijana waliokimbiza Mwenge wa Uhuru mwaka 2013 kuienzi heshma waliopewa na taifa kwa kutumia uzoefu walioupata wakati wakikimbiza mwenge kwa kuelimisha vijana wenzao juu ya mshikamano, upendo na mapenzi ya watanzania kwa nchi yao.
Aliwaambia vijana waliokimbiza Mwenge wa Uhuru mwaka 2013 kutoka Zanzibar waliomtembelea Ofisi kwake Ikulu leo kuwa fursa ya kukimbiza mwenge ni heshma ya kipekee kwa kuwa wako vijana wengi nchini ambao wangependa kupata fursa hiyo lakini wao ndio waliobahatika.
Aliwaeleza vijana hao walioongozwa na aliyekuwa kiongozi wa mbio hizo Juma Ali Simai kuwa safari ya kuizunguka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupeleka ujumbe wa Mwenge lilikuwa jukumu kubwa na zito lakini limewapatia uzoefu mkubwa katika historia ya maisha yao.
“Ni dhamana kubwa kwa taifa na si kila mtu anaweza kuipata na kupewa kati ya watu zaidi ya milioni 44.”Dk. Shein aliwaambia vijana hao na kuongeza kuwa watabaki sio tu katika kumbukumbu za historia ya mbio za Mwenge wa Uhuru lakini kwa upande mwingine wamejitengenezea historia yao wenyewe.
Alibainisha kuwa dhamana ya kukimbiza mwenge iliwapatia fursa vijana hao ya kuwawezesha kuifahamu vyema Tanzania na kujionea maisha na kujifunza mila, utamaduni na silka za watanzani wa maeneo mbalimbali ambapo pamoja na tofauti walizoziona bado wanaishi kwa upendo, mshikamano na kuheshimiana.
Aliwapongeza vijana hao pamoja ndugu zao wengine kutoka Tanzania Bara kwa kufanikisha mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2013 kwa kuonesha uadilifu, uaminifu na ari ya kulitumikia Taifa hadi kukamilisha mbio za mwenge hapo tarehe 14 Oktoba, 2013 walipoukabidhi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
“Hongereni sana na nimefurahi kuwaona tena hapa tangu siku ile ya tarehe 6 Mei, 2013 nilipowakabidhi Mwenge. Hakika mnastahili pongezi kwa kazi nzuri” Dk. Shein aliwaambia vijana hao.
Aliwashukuru kwa kupeleka Ujumbe wa Mwenge kama ulivyotakiwa ukiwemo maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aliwataka vijana hao ambao ni pamoja na Luteni Zuwena Gulam Abdalla na Mgeni Said Mgeni kuwapelekea salamu zake za pongezi kwa vijana wenzao walioshirikiana kukimbiza Mwenge mwaka 2013.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Ustawi wa Jamii, Vijana, wanawake na Watoto katika Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Mshamu Abdalla Khamis alisema kuwa Wizara yake imetiwa moyo sana na uamuzi wa Mheshimiwa Rais kuwakaribisha Ikulu vijana hao.
Alifafanua kuwa Wizara yake imekuwa makini sana katika kuteua vijana kushiriki mbio za mwenge na wamekuwa wakitumia utaratibu wa kutoa matangazo kuwataka vijana waombe fursa hizo.
Kwa hiyo aliahidi kuongeza umakini zaidi katika kuchuja na kuteua vijana wa kukimbiza mwenge ili waweze kuonesha uwezo kubwa kama walivyofanya vijana wa mwaka 2013 pamoja na kuufanya Mwenge wa Uhuru kuendelea kuwa ishara ya umoja wa watanzania na chombo cha kuleta matumaini nchini.
Awali akizungumza kwa niaba ya wenzake aliyekuwa kiongozi wa mbio hizo Juma Ali Simai alisema katika kipindi cha kukimbiza mwenge huo wamejifunza mengi na kukutana na changamoto nyingi lakini walipata moyo kutokana na upendo wa watanzania kwa Mwenge wa Uhuru.
“Watanzania wanaupenda na kuuenzi Mwenge wa Uhuru kwani kila tulipopita wananchi walijitokeza na kuushangilia pamoja na viongozi kutupa ushirikiano wakati wote wa mbio hizo”Kiongozi huo alieleza.
Alibainisha kuwa moja lililowavutia na kujifunza wakiwa huko Tanzania Bara ni kuona skuli nyingi zimeanzisha klabu za mapambano dhidi ya rushwa kitu ambacho kinawajenga vijana tangu mapema utamaduni wa kupiga vita rushwa.
CHANZO-http://www.zanzinews.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni