Habari

Jumanne, 10 Desemba 2013

MGOGORO WA MAENEO WADAIWA KUSABABISHA KUHUJUMIWA KWA MIUNDOMBINU YA MAJI


Wilaya ya Micheweni.
Watu wasiojulikana wameharibu miundombinu ya maji safi na salama kwa kupasua mabomba zaidi ya saba yanayopeleka maji katika Shehia za Kiuyu Mbuyuni na Maziwa Ngombe Wilaya ya Micheweni Pemba.


Sheha wa Shehia ya Maziwang`ombe amesema si vyema kwa wananchi kutumia migogoro yao kwa kuhujumu huduma za umma ikiwemo mbiundombinu ya maji kwa vile yanatumiwa na watu wengi.
Akizungumza na Zenj FM Radio Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Juma Abdalla Ali amesema Kuwa hujuma hizo hakuna shaka zimefanywa na baadhi ya watu wa Micheweni kutokana na mgogoro uliokuwepo baina ya watu wa Kiuyu na Micheweni.
Amesema  kuwa si vyema wananchi wa maeneo hayo na mengine kuchukua hatua za kuhujumu miundombinu ya Umma kwa kisingizio chakuwakomoa watu wengine kwa vile hatua hiyo huleta athari kwa watu wengi na hata wale wasiohusika.
Mkuu huyo wa Wilaya amekilaani kitendo hicho kwa kusema ni cha kinyama,na kuwataka wananchi kutotumia migogoro ya maeneo yao kuhujumu mbiundombinu ya umma,bali wakae pamoja na kutafuta suluhu za migogoro yao.
                                                                                                                                  Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar Tawi la Pemba Juma Ali Othman amesema kitendo hicho kimewasikitisha sana,hasa katika kipindi hiki ambapo serikali ipo katika juhudi za kuwasogezea wananchi wake huduma za maji safi na salama katika maeneo mbali mbali.

Amesema hujuma kama hizo zinapofanywa katika jamii zimekuwa zikirejesha nyuma juhudi za ZAWA za kufikisha huduma ambazo bado wananchi hazijawafikia, sambamba na gharama zisizo tarajiwa.


Zaidi ya Mabomba 7 ya nchi sita yametobolewa kwa kutumia sururu na kupelekea maji kumwagika, kwa kile kilichodaiwa kufanywa kutokana na watu wa Kiuyu kuwazuia watu wa micheweni wasiende kuchukua matofali katika vijiji hivyo.

Imedaiwa kuwepo kwa mgogoro kati ya watu wa Kiuyu Mbuyuni na Micheweni unaoezewa kuwa unahusiana na watu wa Kiuyu kukaa kuchimbiwa matofali katika maeneo yao, kutokana na uharibifu unaosababishwa na uchimbaji huo wa matufali.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni