Habari

Jumamosi, 22 Februari 2014

Warioba ampa somo Werema


Dodoma.                                                                                                                                                      Siku moja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kusema wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wanaweza kubadili chochote, isipokuwa tunu za Taifa, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ameonya kuwa jambo hilo linapaswa kufanywa kwa uangalifu mkubwa.
Jaji Warioba alipingana na kauli hiyo ya Jaji Werema na kusisitiza kuwa Katiba ni mali ya wananchi, hivyo mawazo na mapendekezo  yaliyokusanywa na tume yake kupitia Mabaraza ya Katiba “yanapaswa kuheshimiwa”.
Jaji Warioba alitoa kauli hiyo alipotakiwa na gazeti hili kufafanua kile kinachoonekana kama mkanganyiko wa kauli za viongozi hao wakuu kuhusu majukumu ya Bunge la Mabadiliko ya Katiba.
“Katika hili mimi ndiyo msemaji wa mwisho. Kwenye mchakato huu, sisi sote ni washauri  tu, someni vizuri sheria mtajua. Tangu mwanzo, wananchi  ndio waliotoa maoni yao, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikayakusanya na kutengeneza rasimu ya kwanza,” alisema Jaji Warioba na kuendelea: “Baadaye tukairudisha rasimu hiyo kwa wananchi wenyewe, baada ya kuiboresha kupitia mabaraza ya katiba ya wilaya. Wakaibadili wenyewe, kuridhia na hatimaye tukapata Rasimu ya Pili ya Katiba. Hivyo hata hii rasimu itakayojadiliwa bungeni, bado ni mali ya wananchi.”
Jaji Warioba alisema tofauti na nchi nyingine ambako Bunge la Katiba linaruhusiwa kufanya mabadiliko kwenye rasimu, utaratibu tuliouchukua hapa nchini, ni Bunge hilo kuliondolea mamlaka hayo.
“Hii ni kutokana na ukweli kwamba wenzetu Bunge lao linakuwa na uwakilishi wa wananchi  waliochaguliwa kwa ajili ya katiba tu. Kwa maana hiyo ni wananchi wenyewe. Lakini sisi  kwenye Bunge letu tumechanganya wajumbe wa Katiba na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wale wa Baraza la Wawakilishi ambao kimsingi, hawakuchaguliwa kwa kazi hiyo,” alisema. Aliongeza: “Kwa utaratibu huu wa kwetu, wananchi wana mamlaka zaidi juu ya Katiba yao kuliko Bunge. Bunge na sisi wengine wote tunashauri tu, ndiyo maana hata Tume ilipotengeneza rasimu ya kwanza, ilibidi iirudishe tena kwa wananchi.
Jaji Warioba alienda mbali zaidi na kufafanua kazi ya Bunge hilo kuwa ni kuboresha Katiba.
“Ukiangalia kwa undani, huwezi kuboresha bila kubadili, ila unaboresha kwa kiwango gani na mamlaka yako ya kuboresha yainaishia wapi. Ndiyo maana sisi kwenye Tume tulipoboresha maoni ya wananchi na kutengeneza Rasimu ya Kwanza ya Katiba, tukairudisha kwa wananchi,” alisema.
Alisema kazi ya Bunge Maalumu la Katiba ni kuiboresha rasimu hiyo kwa kutoa ushauri na maoni yake ambayo hata hivyo si lazima yakubalike na wananachi ambao ndio wenye Katiba yao.
 Alichosema Werema
Akijibu maswali ya wajumbe wa Bunge Maalumu juzi, Jaji Werema alisema Bunge Maalumu linaweza kubadili vifungu mbalimbali vilivyomo katika Rasimu ya Katiba, isipokuwa vilivyotajwa katika kifungu cha 9 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Chanzo-Mwananchi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni