Dodoma. Wakati mjadala mkali ndani ya Bunge Maalumu la Katiba ukitarajiwa kuwa muundo wa Muungano, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesisitiza Serikali mbili.
Akifungua semina ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM jana, Pinda alihoji sababu za baadhi ya watu kudai kufa kwa Serikali ya Tanganyika wakati ilishatoweka miaka 50 iliyopita.
Pinda alisema Tanganyika ilidumu kwa miaka mitatu baada ya uhuru, kuanzia mwaka 1961 hadi 1964 na kuungana na Zanzibar.
Alisema kwa msingi huo, Watanzania wengi hawajui lolote kuhusu Tanganyika kwa sababu baadhi yao walikuwa hawajazaliwa. “Suala hili najua litaleta mvutano mkali katika Bunge la Katiba. Binafsi hata ukinikurupusha usiku nitakwambia nataka Serikali mbili,” alisema.
Alisema hata Rais wa Awamu ya Kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kueleza wazi kwamba, alikuwa kiongozi wa Tanganyika kwa muda mfupi na ilikuwa Tanganyika ya wakoloni ndiyo maana likaibuka wazo la kuungana na Zanzibar.
“Hivi sasa tuna miaka 50 ya Muungano wetu lakini wapo watu wanadai Tanganyika, hivi hiyo Tanganyika wanayoida ni ipi, unalalamika kuikosa Tanganyika ipi,”alihoji.
Alisema kasoro zilizopo katika Muungano zinaweza kujadiliwa na ikapatikana suluhu ya kudumu.
Tayari CCM imeshatoa waraka maalumu kwa wanachama wake ikisisitiza msimamo wake wa Serikali tatu, msimamo ambao pia wataingia nao bungeni wakati wa kujadili rasimu ya Katiba ambayo imependekeza muundo wa Serikali tatu.
Rushwa
Akizungumzia rushwa Pinda alisema, “Jumuiya inatakiwa kuwa mstari wa mbele kusimamia uendeshaji wa chaguzi ndani ya chama kwa misingi ya maadili kwani wanaomwaga fedha ili kupata uongozi ndani ya chama wanatuvuruga na hiyo siyo njia ya kukijenga chama.”
Alisema viongozi wanaopatikana kwa njia ya rushwa siyo viongozi bora na kuhoji, “Hivi mtu anayetumia fedha kuingia madarakani akipata madaraka fedha hizo atazirudishaje.”
Katika hotuba yake Pinda aliwagusia wanachama wa CCM wanaopanga nani agombee na nani asigombee na kufafanua kuwa hali hiyo hujenga makundi ndani ya chama hicho.
Chanzo-Mwananchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni