Habari

Jumanne, 18 Novemba 2014

MASHEHA JIMBO LA OLE WAWAKIMBIA VIJANA WANAOTAKA FOMU ZA VITAMBULISHO VYA MZANZIBARI.


Na Is-haka Mohammed,Pemba.  
 Masheha katika jimbo la Ole Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba wameendelea kulalamikiwa kwa kuendelea kuwanyima fomu za kuombea vitambulisha vijana waliotimiza umri wa kupatiwa vitambulisho wa Mzanzibar Mkaazi jimboni humo.
                                                                                                            Wakizungumza na waandishi wa habari  Baadhi ya vijana wa jimbo hilo waliofika katika shehia mbali mbali kwa ajili ya kuchukua fomu za Vitambulisho wamesema kila wanapokwenda wamekuwa wakinyimwa fomu hizo huku wakielezwa kwenda siku nyengine.


Wamesema siku ya Ijumaa pekee ndiyo waliyoiweka  masheha wa jimbo hilo kutoa fomu lakini wanapofika huambiwa kuwa hakuna fomu au wanaambiwa warudi wende Ijumaa inayofuata na wasifuatano kwa makundi na wende mtu mmoja mmoja.
Vijana hao wameeleza kuwa masheha hao wamekuwa wakizungusha kila wanapokwenda kwa kisingizio kuwa fomu walizokuwanazo zimekwisha na kuwataka wafike Ijumaa nyengine hata hivyo wanapokwenda hukuta kufuli katika ofisi zao.

Hata hivyo Mwakilishi wa jimbo la Ole Hamad Massoud Hamad amesema masheha katika jimbo la Ole hawatoi fomu hizo kwa visingizio visivyoeleweka na wamekuwa wakitoa fomu hizo kwa ubaguzi na kudai kuwa utaratibu wa kutoa fomu hizo sikuza ijumaa sio utaratibu wa kisheria kwa vile wanatakiwa kuwapatia wananchi wakati wowote ule.
Amewata masheha hao kuacha kutoa vitabulisho hivyo kwa misingi ya itikadi za vyama kwa vile wananchi wote wana haki sawa ya kupewa fomu hizo kwa vile kila Mzanzibari mwenye sifa anatakiwa kupata kitambulisho.
Wakizungumzia kuhusu lawama hizo baadhi ya masheha wa jimbo la Ole wamesema kuwa fomu wanazitoa kutokana na utaratibu waliojiwekea wa siku moja katika wiki.
Sheha wa Mjini Ole Khamis Shaaban Hamad amesema amekuwa akitoa fomu hizo lakini kikwazo kikubwa ni pale wananchi wanapokwenda kwa makundi na kusema hupatwa na wasiwasi kuwa kuna shinikizo lanalowasukuma kwenda kudai fomu hizo.
Licha ya siku ya Ijumaa vijana kufika kwa wingi katika ofisi za maisha kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo baadhi ya Ofisi hizo ikiwemo ya Kianga,Kiuyu Kigongoni na Minunguni masheha hawakuwepo na ofisi zao zilikuwa  zimefungwa kwa kufuli.
                                 MWISHO.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni