Na Khamis Amani
JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, linawashikilia wahamiaji haramu 10.Wahamiaji haramu hao wametiwa mbaroni Septemba 19 na 20 mwaka huu katika maeneo tofauti ya mkoa huo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Mkadam Khamis Mkadam alithibitisha kukamatwa watu hao katika operesheni iliyofanywa na jeshi la Polisi.
Operesheni hiyo yenye lengo la kupambana na wahamiaji haramu wanaoishi nchini kinyume cha sheria, itaendelea ili kuondosha uingiaji holela wa wageni ambao wengi wao hujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa sheria.
Alisema miongoni mwa waliokamatwa wamo wanawake watano na baada ya upelelezi kukamilika watakabidhiwa Idara ya Uhamiaji kwa hatua zao.
Wakati huo huo, Kamanda Mkadam alisema kuwa Jeshi la Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Unguja linamshikilia mtu mmoja kwa kupatikana na vespa nne zinazoshukiwa kuwa za wizi.
Mtu huyo alikamatwa Septemba 17 mwaka huu katika operesheni yenye lengo la kuwasaka wezi wa vespa ambayo yameshamiri katika kipindi hichi pamoja na makosa mengine mbali mbali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni