Habari

Jumanne, 17 Septemba 2013

SHEKH KHALIL AWATAKA WAISLAMU KUACHA TOFAUTI KATIKA KUUENDELEZA UISLAMU.


Pemba,
Mufti Mkuu wa Oman Samahat Shekh Ahmed Bin Hamed Al-Khalil amesema tofauti za madhehemu zilizopo baina ya waislamu zinaweza kuepukwa ili kuendeleza mashirikiano  kwa maslahi ya Uislamu na Waislamu.
Amesema kuendeleza tofauti na kila dhehebu kujiona bora kuliko mwenzake kunatoa mwanya kwa maadui wa uislamu kuuhujumu na kuudhoofisha uislamu.
Shekh Khalil ameyasema hayo leo huko Tibirinzi Chake Chake katika kongamano lililoandaliwa na waislamu kisiwani Pemba, ambao pamoja na mambo mengine wamempa tuzo maalum ya kutambua Mchango wake mkubwa wa kusaidia maendeleo ya uislamu na waislamu kisiwani humo.
Amesema amefurahishwa na waislamu kisiwani Pemba kwa kuendeleza hisia za umoja na ushirikiano katika kuuhuisha uislamu bila ya kujali madhehebu, ambalo ndilo lengo kuu lililomo katika kitabu cha Allah (S.W).
Naye Naibu Mufti wa Zanzibar Sheikh Mahmoud Mussa mapema katika hafla hiyo, ameishukuru Oman na Mufti Khalili kwa mchango wao mkubwa kwa Zanzibar uliojumuisha ujenzi wa jengo la kudumu la ofisi ya Mufti.
Kwa upande wake Kiongozi wa Jumuiya Istiqama Pemba Sheikh Muhammad bin Suleiman Al-Tiwany, amesema Sheikh Khalili ana mchango muhimu kwa maendeleo ya Uislam na Waislamu.

Sheikh Khalili yuko Kisiwani Pemba kwa ziara ya siku mbili ya kikazi, ambapo hapo kesho atazuru Wete na kufungua msikiti. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni