UBAKAJI umeorodheshwa katika nafasi ya kwanza miongoni mwa matendo makuu ya ukatili wa kijinsia Zanzibar, ukichukua asilimia 26.6.
Matendo mengine ni mimba za utotoni na ndoa za mapema (18%), umaskini (12.2%), ukosefu wa heshima (7.2%) na uwakilishi mdogo wa wanawake katika vyombo vya maamuzi asilimia 6.5.
Utafiti uliofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) katika shehia 18 za Wilaya ya Kusini, Magharibi na Wete Pemba ambako mradi wa GEWE II unatekelezwa na kuwajumuisha watu 120 wakiwemo viongozi wa dini na masheha, umeonesha hali ya udhalilishaji ni mbaya zaidi katika wilaya ya Kusini Unguja ambapo kwa mwaka 2012 hadi Machi 2013, kesi 104 za ubakaji zimeripotiwa.
Afisa kutoka TAMWA, Asha Abdi alisema, kesi 12 zinaendelea na upelelezi, nne zipo mahakamani na saba zimepatikana na hatia.
Aidha utafiti huo umeonesha kuwa bado kuna ucheleweshaji wa utolewaji hukumu kwa kesi za ubakaji ambapo kuanzia 2002-2010 hakuna kesi ya ubakaji iliyotolewa hukumu.
Mwaka 2011 kulikuwa na kesi moja lakini matokeo mazuri yameonekana mwaka 2013 ambapo kesi tatu za ubakaji zimetolewa hukumu katika mahakama ya Mkoa Chake Chake, ikiwemo ya kijana wa miaka 29 aliehukumiwa kifungo cha miaka 60 kwa kuwabaka mapacha.
Utafiti huo unaonesha kuwepo upungufu wa kijinsia hali inayosababisha udhalilishaji kuongezeka.
Upungufu huo ni uelewa mdogo wa wanajamii, tabia ya kuwahifadhi watuhumiwa, kutoripoti kesi za udhalilishaji, kutowajibika kwa taasisi za sheria na usiri.
Afisa huyo alisema utafiti umebainisha wanawake wanakabiliwa na changamoto kubwa zaidi kutokana na kuwa na kiwango nidogo cha elimu, kutoungwa mkono na vyama vya siasa, wenyewe kwa wenyewe kutoshirikiana na mfumo dume.
Mratibu wa TAMWA Zanzibar, Mzuri Issa, alisema wanawake wanakabiliwa na vikwazo vya kiuchumi ikiwemo upungufu wa mitaji,elimu ya ujasiriamali, ukosefu wa masoko na ufikiaji mdogo wa kupata mikopo.
Matokeo ya utafuti huo uliofanywa na TAMWA kwa kuwahusisha wataalamu wazalendo, yalitangazwa mwishoni mwa wiki mbele ya waandishi wa habari.
Na Juma Khamis
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni