Habari

Jumanne, 17 Septemba 2013

Zaidi ya Bilioni Moja Zatengwa Kupunguza Makali ya Ajira. Juhudi Zachukuliwa Kuwapatia Ajira Zenye Staha Vijana Nje.



ZAIDI ya shilingi bilioni moja na milioni mia moja zimetengwa na serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya kuwasaidia vijana kujiajiri wenyewe na kujikwamua na umasikini.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mwanakwerekwe katika kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi Zanzibar, Waziri wa Kazi na Utumishi wa Umma Zanzibar, Haroun Ali Suleiman, alisema vijana wengi wamepata elimu ya kujiunga na vikundi vya ushirika ambavyo kwa kiasi kikubwa vimeweza kuwakomboa kujiingiza katika vitendo viovu.

Aidha Waziri Haroun alisema kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuwawezesha vijana kuweza kujiajiri wenyewe na kuondokana na dhana potofu ya kutegemea ajira kutoka serikalini.

Alisema katika kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa, tayari kila wizara imepewa jukumu lake la kuunda mbinu mbadala na kuwapatia taaluma vijana na kuwahamasisha kujiunga katika vikundi vya ushirika ili kufikia lengo lililokusudiwa la kupunguza umasikini nchini.

Alifahamisha kuwa fedha zinazotolewa na uwezeshaji kwa watu ambao wanataka kujiendeleza kwa sasa hawatopewa fedha kutokana na kuzitumia vibaya na badala yake watapewa vifaa ambavyo ndivyo vitakuwa lengo kujiajiri.

Hata hivyo alisema kuwa tayari Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeshawapatia vijana zaidi ya 400 kazi katika mahoteli mbalimbali.

Pia alifahamisha kuwa katika kujivunia miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar Serikali itaendelea kuboresha suala la maslahi mazuri kwa wafanyakazi wake ili kuondoa manung’uniko ya hapa na pale kwa wafanyakazi.

Waziri Haroun akizungumzia suala la kuwapatia vijana ajira za Nje ya Nchi, alisema wameshaingia mikataba maalum na falme za kiarabu na tayari vijana zaidi ya 300 wameshapatiwa kazi zenye staha na heshima kwa lengo la kuondokana na umasikini na hivi karibuni wanatarajia kuingia mkataba mwengine na nchi ya Oman ili kuhakikisha vijana wanafanya kazi bila ya manyanyaso.

Hata hivyo alitoa wito kwa wananchi kuwa waangalifu na mawakala kabla ya kufanya maamuzi ya kuwapeleka vijana wao nje ya nchi kupita wizarani kwani imeonekana kuwa mawakala hao wamekuwa wakikiuka taratibu za kazi na kuwapatia vijana kazi zisizokusudiwa.

Sambamba na hayo aliwasihi vijana kutovutiwa na kufanya kazi nje ya nchi na kuweka uzalendo mbele kwani maisha ni nyumbani.
Na Khamisuu Abdallah.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni