Habari

Jumatano, 25 Septemba 2013

Wananchi wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya wameombwa kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha maomboleo

Wananchi wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya wameombwa kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha maomboleo ambacho Taifa lao limekubwa na shambulio la kigaidi lililotokea katika Kituo cha Biashara cha Westgate Mjini Nairobi Nchini Kenya wiki iliyopita.
Shambulio hilo la kigaidi linalotuhumiwa kufanywa na kikundi cha ugaidi cha  Al-Shabaab chenye amakao makuu yake Nchini  Somali limesababisha mauaji ya watu wasiopungua 61 wakiwemo raa wa kigeni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa ombi hilo wakati akitoa mkono wa pole mara baada ya kuweka saini kitabu cha maombolezo kwenye ofisi ya Ubalozi wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya Nchini Tanzania uliopo mtaa wa Kaunda Mjini Dar es salaam.
Balozi Seif alisema inasikitisha kuona wananchi wa Kenya wanakumbwa na balaa jengine katika kipindi ifupi wakitanguliwa na lile la kuungua kwa moto kwa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyata Mjini Nairobi.
Alisema mtihani huo uliowapata wakenya unawagusa wana jumuiya wote wa Afrika Mashairiki na Serikali za Mataifa hayo zinapaswa kusaidia kwa namna yoyote ile hatua za kukabiliana na janga hilo la uvamizi wa jengo la kituo hicho cha biashara.
“ Sisi Watanzania na Zanzibar kwa ujumla  tuko pamoja na wenzetu wa Kenya  katika msiba huu mkubwa ambao utaendelea kukumbukwa  katika historia ya Afrika Mashariki “. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alifahamisha kwamba tukio hilo la pili kutokea  Nchini humo mbali ya kuleta mtikisiko wa usalama wa Kenya na uchumi wa Kenya lakini pia unaweza ukaathiri pia usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Balozi Seif aliwataka wananchi wa Kenya kupitia Kaimu  Balozi wao wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya Nchini Tanzania kuendelea na harakati zao za maisha wakati Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi vimeshajitahidi kudhibiti hali hiyo.
Naye Kaimu Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa Kenya Nchini Tanzania Balozi George Owuor  alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba vikosi vya ulinzi Nchini Kenya vimewaua wavamizi hao watano na na kuwashikilia wengine 11.
Balozi George alisema Serikali ya Nchi hiyo tayari imechukuwa  jitihada  za kulidhibiti eneo lote ya Kituo hicho cha Biashara cha Westgate Mjini Nairobi ambacho kilikuwa kikidhibitiwa na magaidi hao kwa takriban siku Nne.
Alisema watu wapatao 65 wamejeruhiwa katika tukio hilo na ghorofa ya Pili na ya Tatu ya Jengo la kituo hicho cha Biashara cha Westgate zimeharibika vibaya sana.
Balozi George alivishukuru vikosi vikosi vya ulinzi vya Nchi hiyo kwa ushirikiano mkubwa wa  kikosi cha makomandoo wa Israel  waliosaidia jitihada hizo za uokozi.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

25/9/2013.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni