“TUMBEZE Rais Jakaya Kikwete katika maeneo mengine aliyoshindwa kutimiza ahadi zake, lakini hili la mchakato wa Katiba mpya amejitahidi kutumia nguvu zake zote, japo anapata upinzani mkubwa ndani ya Chama chake cha CCM.”
Haya ndiyo maneno niliyowaeleza marafiki zangu mwishoni mwa wiki wakati tukipata moja baridi na moja moto katika hafla moja ya jioni na kujikuta tukijadili mustakabali wa taifa letu, hususan mchakato wa Katiba mpya unaoendelea.
Marafiki zangu hao niliwataka kwanza watambue mambo kadhaa kila wanapotaka kujadili mchakato huo badala ya kumvisha lawama zote Rais Kikwete.
Mosi, niliwaambia kuwa katika hili Kikwete ni sawa na mtu aliyejifunga mabomu kwani anatekeleza jambo ambalo halikuwamo katika ilani ya chama chake iliyomwingiza madarakani.
Pili, nilisema kuwa wenzake ndani ya CCM hawapendi kusikia habari za Katiba mpya, hata sasa wapo ambao wanalazimika tu kushiriki mchakato huo kwa vile hakuna jinsi tena, maana rais alishafungua milango hiyo.
Tatu, nikawataka waelewe kwamba washauri muhimu wa masuala ya Katiba, yaani Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, walisema hadharani kuwa Katiba mpya haitakiwi kwa sasa.
Kwa mawazo yao, wananchi hawahitaji Katiba mpya kwa vile hii iliyopo hawaijui na kwamba ni bora ya sasa ikafanyiwa marekebisho na kuwekewa viraka kwenye kasoro zinazolalamikiwa na wapinzani.
Nne, nikawaomba watambue kuwa Rais Kikwete hafanyi uamuzi mwenyewe, bali kuna wasaidizi na washauri wake katika nyanja tofauti ndio wanampatia taarifa za yanayojiri na nini kifanyike, kwamba pale anapojiridhisha anaidhinisha.
Tano, nikawauliza kuwa, sawa tunamlaumu Kikwete katika hili lakini wanadhani mchakato huu ungekuwaje kama rais angekuwa ama Wassira, Jaji Werema, Kombani, Mathias Chikawe au William Lukuvi?
Nilichoambulia katika swali langu ni kicheko, ambacho hata hivyo nilikitafsiri kuwa walinielewa kwamba licha ya Kikwete kuzungukwa na watu wenye masilahi binafsi katika mchakato huu, walau amethubutu kujifungua minyororo na kufika tulikofikia.
Nimeanza na simulizi hiyo fupi nikitaka kuonesha kuwa mchakato huu wa Katiba umetawaliwa na unafiki, ubinafsi na uongo wa hali ya juu. Kwa bahati mbaya sasa wengi wanasahau kuwa penye ukweli uongo hujitenga.
Biblia Takatifu katika kitabu cha Yoshua Bin Sira (sura 20: 24-26) anasema kuwa: “Uongo ni waa la unajisi katika mtu; utakuwemo daima kinywani mwa mjinga.
“Afadhali mwivi kuliko mwongo wa daima lakini wote wawili watarithi maangamizi. Sifa ya mwongo ni fedheha, na aibu yake inadumu daima.”
Ebu sasa taratibu tuyatumie maneno haya matakatifu kujitafakari wenyewe kama kweli tunahitaji Katiba mpya ama tuamini kauli za viongozi wachache niliowataja wakidai nchi haihitaji Katiba mpya.
Mwaka 1995, hayati Mwalimu Julius Nyerere alihutubia Mkutano Mkuu wa CCM wa kumteua mgombea urais wa chama hicho. Moja ya maneno mazito alilolizungumza kati ya mengi ni mabadiliko ya nchi.
“Watanzania wanahitaji mabadiliko, wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,” alisema Mwalimu na kushangiliwa na wajumbe, lakini akawafariji kuwa rais bora atatoka CCM.
Nina hakika Rais Kikwete aliwasikia mawaziri wake kwa kauli zao kabla ya mchakato na hata baada ya hatua hii ya muswada wa sheria unaopigiwa kelele.
Naamini alipima hoja zao kisha akawapuuza baada ya kuona vinywa vyao vimejawa woga wa kukosa vyeo, uongo na ubinafsi, ndiyo sababu ya yeye kuamua vile alivyoona inafaa kwa masilahi ya umma.
Ukipitia vizuri uthubutu wa Rais Kikwete kuikubali hoja ya wapinzani ya kuandika Katiba mpya, utagundu kuwa alitambua maneno ya Mwalimu Nyerere kuwa Watanzania sasa wanahitaji mabadiliko.
Kama Kikwete angechukua ushauri wa kina Werema, Kombani, Wassira na wengine wa kupuuza hitaji la mabadiliko ya kuandikwa kwa Katiba mpya, hakika leo Watanzania hawa wangeyatafuta mabadiliko hayo nje ya CCM.
Kumbe hata hizi sinema tunazoziona bungeni za kuletwa muswada wa sheria ukiwa na kasoro kibao pamoja na uchakachuzi wa vifungu huku Wazanzibari wakiwa hawajashirikishwa ni mbinu zilezile za kutaka kumhadaa Kikwete kuwa mchakato huo wananchi hawautaki.
Twende mbele, turudi nyuma, mashariki au magharibi, rais wetu amelemewa katika mchakato huu wa Katiba mpya.
Chama chake hawataki kabisa kuona ikiandikwa mpya ili waweze kuendelea na mambo yao yaleyale.
Wakati mwingine rais analazimika kuamua kwa mtazamo wa kisiasa ili kuwafurahisha Wana CCM wenzake, lakini moyoni anasukumwa na dhamira moja kwamba akizembea mchakato ukavurugika historia itamhukumu.
Jambo moja analopaswa kulisimamia Rais Kikwete ili kuondoka madarakani akiwa ameandika historia nzuri ya kuwapatia wananchi Katiba ni kulinda kiapo chake cha “kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila woga.” Tafakari.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni