Habari

Jumanne, 8 Oktoba 2013

UVCCM kuwafichua wanaotoa vyeti kiholela

na Mwandishi wetu, Zanzibar
JUMUIYA ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Zanzibar imesema itawataja watendaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Idara ya nyaraka, vizazi na vifo wanaotoa vyeti vya kuzaliwa kiholela.
Ilidaiwa na umoja huo kwamba watendaji wanaofanya hivyo wanalenga kuwapatia vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi, jamaa na ndugu zao wasio na sifa.
Akihutubia mkutano wa hadhara juzi kwenye Uwanja wa Garagara, Jimbo la Mtoni, Mkoa wa Mjini Magharibi, mjini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa umoja huo, Shaka Hamdu Shaka, alisema baadhi ya watendaji wa idara hiyo wanakiuka taratibu za ajira.
Alisema hutoa vyeti vya kuzaliwa kwa ushabiki wa kisiasa ili wapatiwe vitambulisho vya ukaazi hatua itakayowasaidia kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Kwa mujibu wa Shaka, idara hiyo ipo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria inayoongozwa na Waziri kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Aboubakar Khamis Bakari, imeajiri watendaji  wapya na kuhamisha wa zamani ili kupata mwanya wa kufanya upendeleo kwa mtazamo wa kisiasa.
“Tunayo majina ya watendaji wa idara hiyo wanaofanya mchezo  huo mchafu, wasipojirekebisha tangu sasa tutayataja majina yao, tunaitaka Wizara ya Katiba na Sheria ichukue hatua zinazostahili, huo ni mpango wa siri unaolenga kuleta vurugu na  upendeleo,” alisema.
Aidha, alimtaka Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, kuacha kuyadhihaki Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuimba nyimbo kwenye majukwaa ya kisiasa huku  matendo na matamshi yake hayaheshimu na kuenzi mapinduzi hayo.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya Zanzibar, Najma Murtaza Giga, aliwataka viongozi wa vyama vya upinzani nchini kutofikiria  kuwa CCM imechoka kiakili na inaweza kuburuzwa kama inavyofikiriwa na baadhi ya vyama hivyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni